Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yashika hatma ya Polisi

IMG 4108 Simba Training.jpeg Kikosi cha Simba kikiendelea na mazoezi

Thu, 18 May 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya Yanga kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara, vita kubwa sasa ipo mkiani kwenye msimamo wa ligi hasa timu zinazokwepa kushuka daraja.

Wakati Yanga ikiwa imetetea ubingwa, Ruvu Shooting ndiyo timu ya kwanza kushuka daraja baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Simba.

Simba ndiyo imeishusha Ruvu Shooting na mchezo ujao itacheza dhidi ya Polisi Tanzania na endapo Maafande hao watapoteza mchezo nao, itakuwa imekamilisha timu mbili zinazopashwa kushuka daraja msimu huu.

Polisi Tanzania ipo nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na alama 25 sawa na utofauti wa alama nne dhidi ya KMC na Mtibwa Sugar ambazo zipo hatarini kushuka daraja.

Maafande hao baada ya kumalizana na Simba itafunga pazia la msimu dhidi ya Azam Uwanja wa Azam Complex Mei 28 na michezo yote ya ligi itachezwa viwanja tofauti.

Mtibwa Sugar baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Polisi Tanzania juzi, sasa inaungana na KMC nafasi ya kucheza hatua ya mtoano.

Walima Miwa hao wamesaliwa na michezo miwili dhidi ya Geita na Kagera Sugar huku KMC ikiwa na kibarua kizito zaidi dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine kisha Mbeya City Uwanja wa Nelson Mandela. Ubaya kwa KMC timu zote mbili hazina uhakika wa kubaki ligi kuu huku ikiwa imepishana alama moja na Mbeya City yenye alama 30.

Mbeya City mchezo ujao itacheza na Yanga kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, huku Yanga ikiwa imepoteza michezo miwili pekee msimu huu, ikilala 2-1 kwa Ihefu kisha 2-0 kwa Simba. Endapo Yanga itashinda mchezo huo ambao itakabidhiwa kombe lake, basi Mbeya City itakuwa katika mazingira magumu zaidi.

Timu itakayomaliza nafasi ya 13 na 14 zitacheza hatua ya mtoano na itakayofungwa itakutana na timu ya Ligi ya Championship kati ya Mashujaa na Pamba zitakazomenyana hatua ya mtoano.

Afisa Habari wa Polisi Tanzania, Frank Lukwaro alisema bado hawajakata tamaa na wachezaji pamoja na benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Mwinyi Zahera limezidi kuwa na morali kubwa.

"Tunakwenda kukutana na Simba ambayo imekuwa vyema msimu huu lakini Polisi Tanzania ndio inauhitaji zaidi kuliko wao, hivyo tunatarajia kutua Dar es Salaam wikiendi hii," alisema Lukwaro.

Polisi Tanzania ilipanda daraja msimu wa mwaka 2020/21 pamoja na Namungo lakini msimu huu imekuwa na mwenendo mbovu zaidi kwenye ligi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: