Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yampa nguvu Mbrazili

Robertinho Kambini Uturuki.jpeg Simba yampa nguvu Mbrazili

Wed, 27 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati maneno mengi yakizungumzwa juu ya mwenendo wa uchezaji wa kikosi cha Simba licha ya ushindi, uongozi wa timu hiyo chini ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ wamesema kocha Oliveira Roberto ‘Robertinho’ anawapa jeuri ya kuamini atafanya mambo makubwa zaidi msimu huu kutokana na rekodi alizonazo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Try Again alisema kipimo cha kocha mzuri ni matokeo na sio aina ya uchezaji huku akikiri kuwa matokeo mazuri ndio yanatwaa mataji na sio pasi nyingi.

“Malengo yetu ni kutwaa taji la Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na kufika nusu fainali Ligi ya Mabingwa, tuna imani kubwa na kocha ataweza kufikia malengo haya kwani tayari kajiwekea rekodi kubwa ya kushinda mechi licha ya watu kumjaji katika uchezaji wa timu;

“Kocha mzuri ni yule ambaye anaipa timu matokeo mazuri bila kuangalia sababu nyingine, matokeo ndio yanatwaa mataji na kufika hatua kubwa kimashindano hivyo kama viongozi tunatambua ubora wake na vigezo vya kuwa kocha wa Simba ni kuipa timu matokeo.” alisema Try Again.

Alisema Robertinho ameiongoza Simba kwenye mechi 14 za Ligi Kuu Bara hadi sasa bila kupoteza sasa ni kiongozi gani anaweza kufanya uamuzi mgumu wa kumuondoa kocha wa aina hiyo.

“Sio kila kinachozungumzwa kinachukuliwa na kufanyiwa uamuzi, tunawasikia, lakini jambo kubwa tunalolifanya sisi ni kumtaka kocha aendeleze ubora wake kwa kuhakikisha timu inapata matokeo na sio vinginevyo.

Katika michezo hiyo 14, ambayo Robertinho ameiongoza Simba katika Ligi Kuu tangu alipojiunga nayo Januari mwaka huu, timu hiyo imepata ushindi mara 12 na imetoka sare mbili tu.

Simba chini ya Robertinho, imefunga mabao 35 ikiwa ni wastani wa mabao 2.5 kwa kila mchezo na imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa tu ikiwa ni wastani wa bao 0.7 kwa mechi.

Robertinho alianza kwa ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mbeya City, akaja kuichapa Dodoma Jiji kwa bao 1-0, kisha akaibuka na ushindi wa mabao 3-1 mbele ya Singida Big Stars na mchezo uliofuata akalazimishwa sare ya bao 1-1 na Azam FC.

Baada ya hapo, Simba ikaibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, ikapata ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Ihefu na kuwafunga watani wao Yanga kwa mabao 2-0 na ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na Namungo FC.

Timu iliyofuata kuonja makali ya Robertinho ilikuwa ni Ruvu Shooting iliyochapwa mabao 3-0, kisha Polisi Tanzania ikafungwa mabao 6-1 ikifuatiwa na Coastal Union iliyochapwa mabao 3-1 na msimu huu ikaanza kwa kuifunga Mtibwa Sugar mabao 4-2, Dodoma Jiji 2-0 na imewafunga Coastal Union mabao 3-0.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: