Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba yaifunika Yanga, Azam ugenini

Simba X Yanga CAF Simba yaifunika Yanga, Azam ugenini

Mon, 11 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Ikicheza bila ya kocha mkuu, Abdelhak Benchikha, Simba juzi usiku ilipata ushindi wa mbinde wa mabao 2-1 mbele ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union, ikiendeleza moto wake kwa mechi za ugenini katika Ligi Kuu Bara.

Licha ya kucheza soka lisilovutia mashabiki katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga, bado Simba iliendeleza rekodi tamu iliyonayo kwa michezo ya ugenini ikiwa ndio kinara wa kupata matokeo bora kulinganisha na timu nyingine 15 za msimu huu.

Kama hujui, mechi ya juzi ilikuwa ni ya tisa kwa Simba ugenini na ushindi huo dhidi ya Wagosi wa Kaya, ulikuwa ni wa nane kwa timu hiyo, lakini ikiwa ni timu pekee iliyofunga bao katika mechi hizo zote za ugenini, licha ya mchezo mmoja kulazimishwa sare.

Mchezo pekee ambao Simba ililazimishwa sare ni ule dhidi ya KMC ulioisha kwa matokeo ya 2-2, lakini mechi nyingine zote nane zilizosalia imefunga angalau bao moja, huku kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Saido Ntibazonkiza akiwa ndiye kinara wa kutupia akifunga mabao manne katika mechi hizo.

Saido alifunga bao katika ushindi wa 3-1 iliyopata Simba mbele ya Tanzania Prisons jijini Mbeya, akafunga jingine ilipoifumua Singida FG kwa mabao 2-1, akatupia kwenye sare ya 2-2 na KMC na kufunga la mwisho wakati Mnyama akitafuna Sokwe la Kigoma, Mashujaa kwa bao 1-0.

Nyota anayemfuata Saido kwa kufunga mabao mengi ugenini ni Clatous Chama aliyefunga matatu, likiwamo moja wakati Simba ikiifunga Mtibwa Sugar mabao 4-2, akatupia dhidi ya Prisons na jingine alifunga wakati wakiwazamisha maafande wa JKT Tanzania kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.

Mabao waliyofunga Willy Onana na Freddy Michael juzi mbele ya Wagosi, yalikuwa ni ya pili kwa nyota hao wakishika nafasi ya tatu sambamba na Jean Baleke aliyetemwa katika dirisha dogo na kuibulia Libya.

Onana alianza kufunga katika ushindi dhidi ya Mtibwa, huku Freddy alifunga bao lake la kwanza akiwa na uzi wa Simba kwenye Ligi walipoitungua Tabora United kwa mabao 4-0 mjini Tabora, wakati Baleke alifunga dhidi ya Mtibwa na katika sare ya 2-2 dhidi ya KMC.

Wachezaji wengine saba, wakiongozwa na nahodha John Bocco na Mzambia Moses Phiri aliyeachwa katika dirisha dogo na kurejea kwao, wamefunga bao moja moja katika mechi hizo tisa za ugenini zilizopita Simba jumla ya mabao 20 na kufungwa saba.

Wengine waliofunga bao moja moja ni beki Fondoh Che Malone, viungo Sadio Kanoute, Babacar Sarr na Fabrice Ngoma pamoja na mshambuliaji mpya, Pa Omar Jobe.

Takwimu zinaonyesha katika mechi hizo tisa, Simba imevuna jumla ya pointi 25, huku ikizitema mbili tu na kuongoza klabu zilizovuna pointi nyingi ugenini ikiziacha hadi Yanga na Azam zinazofuata.

Yanga iliyocheza pia michezo tisa, imeshinda michezo saba, imetoka sare mmoja na kupoteza mmoja mbele ya Ihefu, huku ikifunga mabao 19 na kufungwa matano, ikiwa na tofauti nzuri ya mabao kulinganisha na Simba, japo imeambulia kuvuna pointi 22 kati ya 27.

Azam inakamilisha tatu bora ya timu zilizofanya vyema ugenini kwa kucheza mechi 10 ikivuna pointi 19 kutokana na kushinda tano, ikitoka sare nne na kupoteza moja, imefunga jumla ya mabao 16 na kufungwa sita katika mechi hizo ikishika nafasi ya pili kwa sasa katika msimamo wa Ligi Kuu nyuma ya Yanga.

Yanga itakayoshuka uwanjani leo inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 49 katika mechi 17, wakati Azam imecheza michezo 20 imevuna alama 44 na Simba yenye michezo 17 imekusanya pointi 39, zikiwa ndizo timu pekee zilizosalia kwenye mbio za kuwania ubingwa msimu huu kwa sasa.

Licha ya Simba kuongoza kwa timu zilizopata matokeo mazuri ugenini, kwa upande mwingine ni moja ya timu zilizofanya vibaya zikiwa nyumbani kwani inashika nafasi ya 10 ikicheza michezo minane na kushinda mara nne tu, huku mbili ikitoka sare na mingine kama hiyo ikipoteza na kukusanya jumla ya pointi 14, imefungwa mabao 10 na kufunga 14.

Azam ndio yenye matokeo mazuri nyumbani kwani katika mechi 10 ilizocheza imeshinda mara nane na moja imepoteza sawa na iliyotoka sare na imefunga mabao 29 na kufungwa tisa huku kwa upande wa pointi imekusanya 25, moja zaidi na ilizovuna Yanga inayoshika nafasi ya pili kwa mechi za nyumbani.

Yanga imecheza mechi nane nyumbani ikishinda zote na kukusanya pointi 24, imefunga mabao 23 na kufungwa manne, huku Tanzania Prisons ikifuata kwa timu zilizofanya vyema nyumbani ikicheza mechi 11, imeshinda tano, sare tatu na kupoteza pia tatu ikivuna pointi 18 na imefunga mabao 14 na kufungwa mabao 12.

Pamoja na Simba kuwa kinara kwa mechi za ugenini, lakini mara kadhaa kocha mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha amekuwa akikaririwa kulia na ubovu wa viwanja vya mikoani sawa na ilivyo kwa Miguel Gamondi wa Yanga ambao wanachuana kuwania, kuonyesha hali ni tofauti na wanachokisema.

Kabla ya kwenda Algeria kwa ajili ya ishu za mafunzo, Benchikha alikaririwa baada ya Simba kulala 2-1 mbele ya Prisons Morogoro, akiuponda Uwanja wa Jamhuri ambao klabu hiyo iliuchagua kuwa wa nyumbani kabla ya juzi TFF kutangaza kuufungia kwa ishu za matangazo ya wadhamini, Azam Media.

Simba inatarajiwa kurejea nyumbani kesho kuvaana na Singida katika mechi inayotarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, huku wageni wakiwa na rekodi mbaya katika mechi nane zilizopita wakicheza bila ushindi ndani ya Ligi Kuu, hali inayoweza kuwarahisishia kazi wenyeji kuendeleza ubabe wao kwao.

Tangu ipande daraja, Singida haijaweza kuishinda Simba katika mchezo wowote wa Ligi Kuu, zaidi ya kuambulia sare ya 1-1 msimu uliopita, huku michezo miwili ikipasuka.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: