Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba wasichukie Phiri, Baleke kuondoka

Bqleke Phirii00 Simba wasichukie Phiri, Baleke kuondoka

Fri, 19 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 imemalizika kinyonge kwa Simba baada ya kulikosa kwa kufungwa bao 1-0 katika mechi ya fainali dhidi ya Mlandege ambayo ilitetea ubingwa wa mashindano hayo.

Na ilitegemewa mashindano hayo yawe na neema au mkosi kwa baadhi ya wachezaji hasa wale ambao wamekuwa hawapati nafasi ya mara kwa mara kikosini kwani walipewa nafasi ya kuonyesha kama wanastahili kuendelea kuwepo kwenye timu hiyo au hawastahili.

Kabla hata ya mechi ya fainali, Simba ikafanya uamuzi wa kuachana na baadhi ya wachezaji ambao walionekana kutofanya vizuri hata katika mashindano hayo ikiwapa fursa ya kujaribu bahati yao kwingine na kufungua milango kwa nyota wapya ambao imewasajili katika dirisha dogo.

Hata hivyo, wachezaji hao ambao walipewa mkono wa kwaheri kabla Kombe la Mapinduzi halijafikia tamati, hawakushtua sana kwa vile walishaonyesha mapema dalili ya kutodumu katika kikosi cha Simba tangu mwanzoni mwa msimu kutokana na kutopata nafasi kubwa ya kucheza.

Kilichokuja kushtua ni kuachwa ghafla kwa washambuliaji wawili wa timu hiyo, Moses Phiri na Jean Baleke ambao wamewapisha Omar Jobe pamoja na Freddy Kouablan.

Phiri alikuwa kipenzi cha mashabiki wa timu hiyo kutokana na kiwango bora alichokionyesha mwanzoni mwa msimu uliopita kabla ya kupata majeraha wakati Baleke ndiye alikuwa mfungaji bora wa Simba katika Ligi Kuu msimu huu kwani hadi anaondoka tayari alishapachika mabao manane.

Kuna baadhi ya mashabiki wa Simba wameonekana kutofurahishwa na uamuzi wa kuwaacha wachezaji hao wote wawili kwa pamoja hasa wakitoa hoja kwamba wachezaji wawili walioingizwa kuchukua nafasi zao ni wageni hawajazoea mazingira ya Tanzania hivyo angebakizwa angalau mmoja ili ikitokea mambo yamekuwa magumu kwa wapya, yeye abebe jukumu.

Hata hivyo, wanachosahau ni kwamba uamuzi wa kuwatosa Baleke na Phiri umetokana na mapendekezo ya kocha Abdelhak Benchikha ambaye wakati anaanza kazi ya kuinoa timu hiyo, ni haohao mashabiki waliupa angalizo uongozi wao kwamba uhakikishe hawamuingilii kocha huyo katika majukumu yake na kila anachokiamua, uongozi ukifanyie kazi.

Baada ya fainali ya Kombe la Mapinduzi, Benchikha aliwalaumu wazi washambuliaji wake wa kati kwamba hawatimizi ipasavyo majukumu yake, hivyo ipo wazi kwamba yeye ndio ameamua kuwakata kwani tayari alishapoteza imani nao, mashabiki wavumilie tu. Watulie wanywe mtori, nyama ziko chini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: