Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba ni ile ile, wachezaji wale wale, mashindano tofauti

Simba Mtihani Mzito Dhidi Ya Jwaneng Galaxy Wikiendi Hii.jpeg Simba ni ile ile, wachezaji wale wale, mashindano tofauti

Tue, 28 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kama bao la penalti laini ya Saido Ntibazonkiza dhidi ya Asec Mimosas lingesimama kwa dakika zote tisini si ajabu mashabiki na viongozi wa Simba wangerudi katika dunia yao ya njozi kwamba bado wana timu bora kwa ukanda huu wa Afrika mashariki.

Si ajabu pia wangeendelea kuota ile njozi maarufu kwamba wao wanakuwa kitu tofauti linapokuja suala la michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika. Safari hii walikumbushwa tu kwamba timu yao ni ile ile tu ya kawaida ambayo wamekuwa wakiishuhudia katika miaka ya karibuni.

Ilianzia katika pambano dhidi ya Yanga. Lilikuwa ni suala la muda tu kabla Simba haijapokea kichapo kile cha mabao matano kutoka kwa mtani. Kibinadamu kama wachezaji wa Simba wangehisi kwamba wamewaangusha mashabiki wao basi wangejibu mapigo katika pambano lililofuata dhidi ya Namungo kwenye uwanja wa zamani wa Taifa.

Kuna wachezaji walishutumiwa kuhujumu mechi. Kuna wachezaji walionekana kulia baada ya pambano la mtani. Hawa wote walipaswa kujibu mapigo katika pambano lililofuata dhidi ya Namungo pale Shamba la Bibi.

Haikuweza kuwa hivyo. Pambano lilimalizika kwa sare. Kibinadamu mchezaji anawezaje kuhujumu mechi mbili mfululizo? Halafu sasa likaja pambano hili dhidi ya ASEC. Hii ni michuano ambayo Simba wanaamini kwamba ipo kwa ajili yao.

Pambano lilimalizika kwa sare Jumamosi jioni. Simba walifukuzwa kwa muda mrefu wa kipindi cha pili baada ya Saido kuipatia bao la kuongoza kipindi cha kwanza. Lilikuwa suala la muda kabla ya ASEC kusawazisha.

Wachezaji wa ASEC walionekana kuwa na stamina. Mchezaji mmoja wa ASEC angegombea mpira na mchezaji mwingine basi mchezaji wa Simba angeanguka tu. Lakini pia walionekana kuwa wazuri katika kuhamisha mpira kutoka nyuma kwenda mbele. Nafasi nyingi zilikuwa wazi kwao kuweza kufanya hivyo.

Bao lao lilikuwa linakuja kwa sababu Simba walionekana wamechoka kwa muda mrefu wa mchezo. Kama sio uhodari wa kipa wao Ayoub Simba wangeweza kufungwa hadi mabao matatu. Kumuweka nje Clatous Chota wala kumuingiza kipindi cha pili hakuna ambacho kilileta mabadiliko katika timu.

Simba walikuwa wazito wakiwa na mpira kama ambavyo walikuwa wazito wakiwa hawana mpira. Hili la kwanza sio tatizo sana, hili la pili lilikuwa tatizo sana kwao kwa muda mrefu. Ni Yanga ndio waliokuja kuwaonyesha udhaifu huu.

Baada ya kuitazama timu yao dhidi ya Namungo na kisha ASEC nadhani mashabiki watagundua kwamba timu yao haikuhujumiwa dhidi ya Yanga. Ni vile tu tangu wakati wa Robertinho walikuwa wana mwendo wa jongoo ambao wenyewe waliuita ‘muhimu pointi tatu’.

Jumamosi jioni baada ya matokeo, mashabiki wengi walitapika nyongo kuhusu kiwango cha timu yao. Kama unajua vile namna ambavyo siku hizi tuna waandishi wengi wa habari wanaoshika vipaza nje ya uwanja baada ya mechi kumalizika.

Safari hii mzigo ulihama kidogo kutoka kwa Murtaza Mangungu ambaye alishutumiwa mno katika pambano dhidi ya Namungo ukahamia kwa wachezaji wenyewe. Hatimaye wamefikiwa. Na hapa ndipo sisi wenye kazi ya uchambuzi inabidi tushughulike napo.

Kichekesho kilikuja wakati mabosi wa Simba walipokaa na wachezaji kwa zaidi ya saa tatu pale pale uwanjani baada ya mechi kumalizika. Kichekesho kingine kikaja juzi baada ya picha kuvuja kikionyesha mabosi wa Simba wakiwa na kikao na wachezaji.

Wanazungumza nini? Najua hizi za viongozi ni kama zile za mashabiki. Kwamba wachezaji hawajitumi. Sio kweli. Wachezaji wanacheza kadri ya uwezo wao lakini pale ndipo walipofikia. Iliwahi kusemwa tangu zamani kwamba kudra haizidi uwezo.

Viongozi wa Simba wameiona timu yao ikimung’unyuka kutoka katika usajili mbovu, kushuka kwa viwango vya wachezaji lakini zaidi pia kuna shida katika suala la kocha wa viungo pale Msimbazi. Yote haya yanalipiwa sasa hivi.

Sijui viongozi wa Simba wanafikiria nini kwa sasa lakini watu wa kwanza kushutumiwa ni wao. Inachosha kurudia mara kwa mara lakini kilichotokea Jumamosi jioni hakikunishangaza. Kwani Simba imeanza kushuka leo? Kuna madirisha mangapi ya usajili yanapita na viongozi wanaendelea kukosea?

Badala ya kumfuata Mudathir Yahaya aliyekuwa hana kazi pale Forodhani wao wakamfuata Ismael Sawadogo. Haya ni makosa mengi ya muda mrefu mpaka tukafika hadi huku kwa kina Essomba Onana. Wakati wao wakiwa katika hali hii hisia zikawa kubeza mafanikio ya watani wao kadri walivyokuwa wanajikusanya na kupanda juu.

Sawa, siku moja kabla ya hapo watani zao walikuwa wamepokea kichapo cha mabao matatu pale Algiers lakini ni bora ya Yanga waliokufa tatu Afrika Kaskazini kuliko Simba waliotoka sare pale Temeke. Waliotazama mechi zote mbili wanaweza kutoa ushahidi.

Simba wanahitaji kubadilika kwa haraka. Kubadili namna ya wanavyofikiri na kisha kujipanga upya. Tatizo langu ni kwamba tunahitaji Simba mpya kutoka kwa watu wale wale waliosababisha Simba ishuke.

Sare dhidi ya ASEC ilikuwa ni ukumbusho tu wa namna ambavyo maisha yao yatakuwa magumu bila ya kujali aina ya michuano wanayocheza. Historia ya kufanya vizuri katika michuano fulani inapaswa kuambatana na timu bora.

Kifuatacho ni ukweli kwamba waliokuwa wanaonekana ni vibonde wa kundi Jwaneng Galaxy wameshinda ugenini dhidi ya Wydad Casablanca. Hii inaonyesha kwamba wana timu nzuri. Simba wanawafuata hawa rafiki zetu pale Gaborone huku mwenyeji akiwa anajiuliza ‘Kama nimemfunga Mwarabu kwake nitashindwaje kumfunga Mtanzania hapa kwangu?’

Na baada ya hapo Simba atasafiri mpaka Casablanca kucheza dhidi ya Wydad. Hii itakuwa mechi ya pili kwa Simba kucheza ugenini. Watakutana na hasira za Mwarabu ambaye atakuwa anacheza mbele ya mashabiki wake kwa mara nyingine tena baada ya kufungwa mbele yao katika pambano la kwanza.

Sijali sana kuhusu mazingira ya mechi hizi. Kinachonitia wasiwasi ni Simba yenyewe jinsi ilivyo. Ingekuwa Simba ya wakati ule ningeweza kuwashikia dhamana lakini kwa Simba hii basi ratiba hii ni ngumu maradufu kwao na siwezi kuwashikia dhamana.

Labda tumuone kocha mpya anavyoweza kufanya ndani ya muda mrefu lakini ni wazi kwamba anaikuta Simba iliyoparaganyika ndani na nje ya uwanja. Kazi anayo kweli kweli.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: