Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba mpya, Onana heshima inarudi

Onan Pic Simba mpya, Onana heshima inarudi

Sun, 9 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Siku chache baada ya Simba kumtambulisha kuwa ni Mnyama, Leandre Willy Onana, amevunja ukimya akisema, anajua ana deni kubwa kwa mashabiki wa timu hiyo, kwani anajua ukubwa wa klabu hiyo ila anachoshukuru ni kwamba anaijua kazi yake vyema.

Winga huyo kutoka Cameroon ni mchezaji wa kwanza mpya kutambulishwa na Simba tangu dirisha la usajili lilipofunguliwa Julai Mosi, akitokea timu ya Rayon Sports ya Rwanda aliyoisaidia kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya nchini humo huku akiibuka Mchezaji na Mfungaji Bora akitupia mabao 16.

Winga huyo anayemudu kucheza nafasi zote za mbele kwa ufasaha ikiwamo ushambuliaji, amesajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili na akizungumza na Mwanaspoti ikiwa ni mahojiano ya kwanza tangu asajiliwe, alisema; "Naijua (Simba)kwa sababu ni moja ya klabu kubwa ukanda huo (Afrika Mashariki), nilifurahi kupata nafasi ya kujiunga nayo, naamini itanifanya kuonekana zaidi."

"Nipo tayari kutoa mchango wangu wote kuhakikisha tunafikia malengo ya timu, naomba mashabiki wasubiri waone nitakapoanza kuitumikia. Mie ni mchezaji ninayeijua kazi yangu," alisema kiungo mshambuliaji hiyo, huku Mwandishi na Mchambuzi wa Soka wa nchini Rwanda, Eric Ndagijimana ambako ametoka Onana alisema; "Anaweza kuongeza kitu kwenye timu lakini anatakiwa kupewa muda wa kuzoea mazingira yake mapya ya kazi,"

"Atakutana na presha kubwa pengine kuliko hata ilivyokuwa Rwanda, anakutana na wachezaji ambao aina yao na uchezaji ni tofauti ukilinganisha na huku (Rwanda), lakini pamoja na yote anaweza kuonyesha kitu."

MAPEMA TU

Mwanaspoti iliripoti mapema juu ya dili kukamilika siku chache zilizopita kabla ya nyota huyo kwenda kwao Cameroon kwa mapumziko mafupi, tukiweka bayana amepewa miaka miwili na angetambulishwa ndani ya wiki hii, kitu kilichoenda kama kilivyo.

Msimu uliopita Onana aliibuka Mfungaji Bora wa Ligi Kuu yaRwanda baada ya kufunga mabao 16 na kuasisti mengine matano kwa wenzake na kisha kushinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu na kumfanya aondoke nchini huyo kibabe kabla ya kuja kutua Msimbazi inayosaka mataji kwa sasa.

Simba imetoka kapa misimu miwili mfululizo mbele ya Yanga kwa kushindwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la ASFC na hata Ngao ya Jamii, huku kwenye michuano ya kimataifa iliishia robo fainali, wakati watani wao walienda hadi fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza kwa USM Alger kwa faida ya bao la ugenini kwani matokeo ya jumla ilikuwa ni sare ya mabao 2-2.

Akiwa ni igizo la kwanza jipya kwa Simba, anatabiriwa huenda akaiongezea nguvu timu hiyo kwa msimu ujao wa mashindano wa mwaka 2023-2024 kwa aina yake ya uchezaji, huku mashabiki wakisikilizia majembe mengine mapya yakiendelea kushushwa kabla ya kwenda kambini Uturuki.

Uwezo wake wa kucheza nafasi zaidi ya moja inamfanya kocha aliyempendekeza, Roberto Oliveira 'Robertinho' kuwa na machaguo mengi ya kumtumia kwenye kikosi chake na hapo chini ni sehemu ambazo Mcameroon huyo anaweza kuliamsha kwa raha zake na kuwapa burudani mashabiki.

WINGA YA KUSHOTO

Licha ya kuwa na uwezo wa kucheza winga zote mbili, eneo ambalo anaonekana kuwa na madhara ni upande wa kushoto na mabao yake mengi aliyofunga msimu uliopita yalitokea huko ni mwenye kasi na maamuzi ya haraka.

Msimu uliopita kwenye kikosi cha Simba, winga ya kushoto walionekana kucheza zaidi kwa nyakati tofauti Pape Sakho, Kibu Denis na muda mwingine ilipobidi walitumika Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza.

Sakho na Kibu walionekana kutokuwa na mwendelezo wa ubora hivyo walikuwa na ingia toka kwenye kikosi cha kwanza.

Onana atakuwa na kibarua cha kupigania namba mbele ya wachezaji hao, kasi na maarifa aliyonayo yanaweza kuongeza kitu hata Roberto Oliveira 'Robertinho' naye atakuwa na machaguo mengi upande huo.

FALSE NINE

Huyu ni mshambuliaji wa kati ambaye mara nyingi huanzishwa kama mshambuliaji wa mwisho 'namba tisa' kwa lengo la kuwahadaa wapinzani, ni ngumu kumuona akisimama sehemu moja kama ilivyo kwa mshambuliaji halisi wa kati lengo ni kutengeneza nafasi kwa wachezaji wengine.

Kinachomtofautisha 'false nine' na mshambuliaji halisi wa kati ni majukumu. Onana anaweza vizuri kutumika kwenye eneo hilo kwa ubora wa viungo washambuliaji wengine ambao wapo kwenye kikosi hicho kama vile Chama na Ntibazonkiza ni wazi kuwa Robertinho anaweza kupata kile ambacho anakihitaji kutoka kwa mfungaji bora huyo wa Ligi ya Rwanda. Lakini pia Onana anaweza pia kusimama kama mshambuliaji wa mwisho.

NAMBA 10

Haionekani sana kama anaweza kuja kutumika kama namba 10 kulingana na aina ya wachezaji ambao Simba ipo nao kwenye maeneno hayo lakini anaweza kutumika kama mshambuliaji pacha ikiwa Robertinho atataka kuwa na nguvu zaidi kwenye safu yake ya ushambuliaji.

Ipo michezo ambayo Robertinho amekuwa akihitaji nguvu zaidi kwenye safu yake ya ushambuliaji na kwa msimu uliopita kuna kipindi tuliona wakicheza pamoja Moses Phiri aliporejea kutoka majeruhi na Jean Baleke.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: