Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba makundi CAFCL bila kocha mkuu, Yanga na hesabu kali kwa Waalgeria

Simba Wamkaribisha Gamondi Mazoezini Simba makundi bila kocha mkuu, Yanga na hesabu kali kwa Waarabu

Wed, 22 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally akipita kwenye matawi mbalimbali nchini kuhamasisha mashabiki kujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Jumamosi ijayo itakapocheza dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, timu hiyo bado inaendelea kunolewa na Kaimu Kocha Mkuu, Daniel Cadena akisaidiwa na Suleimani Matola na huenda ndiyo watakaoisimamia timu hiyo kwenye mchezo dhidi ya Waivory  coast hao.

Juzi, Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally alikuwa jijini Arusha na kutembelea matawi yote makubwa na kuhamasishana kwa ajili ya mchezo wao wa Novemba 25.

Ahmed alitembelea matawi ya Simba Duniani, Simba Raha Arusha, Arusha Terminal na Simba Burudani."Familia ya wanasimba Arusha tumemaliza kujadili hamasa ya mchezo wetu wa Novemba 25 dhidi ya Asec Mimosas.

Viongozi wa matawi yote Arusha wamenihakikishia kuwa watakuja uwanjani na watahamasisha wengine," alisema Ahmed.

Ahmed kwa sasa anatumia nguvu ya ushawishi wake kwenda moja kwa moja kwa mashabiki na matawi yao makubwa nchini kwa ajili ya kurejesha imani kwa wanachama na mashabiki walioipoteza kwa timu hasa baada ya kupokea kipigo cha mabao 5-1 kutoka kwa Yanga.

Baadhi ya mashabiki wamesema kuwa watakwenda uwanjani kuisapoti timu yao na kusahau yaliyopita, hata hivyo wengine wameonekana kuwa na wasiwasi kutokana na kutokuwa na Kocha Mkuu.

Wakati hayo yakijiri upande wa Simba, kwa upande wake, Kocha wa Yanga, Miguel  Gamondi amesema ameanza programu maalum ya kuwaongezea kasi na maarifa wachezaji wake kuweza kutumia  vyema kila nafasi watakayoipata kwenye michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Miguel, alisema anawafanyisha wachezaji wake mazoezi ya kufunga mabao ndani ya eneo la hatari kwa pasi mpenyezo zinazopigwa kutoka pembeni .

“Nataka kuona kila mchezaji anatumia nafasi vizuri ya kufunga kila anapopata nafasi ya kufanya hivyo, kwenye mashindano haya hatupaswi kuwa tunapoteza nafasi yingi za kufunga kama ilivyo sasa,” alisema Gamondi na kuongeza.

"Tunajaribu kila mbinu, kila mfumo kwa sababu tunakwenda kucheza mechi ngumu. Tumezoeleka mabao yetu mengi yanapatikana kupitia pembeni, hivyo natengeneza mifumo mingine ambayo tunaweza kubadili pale mmoja unaposhindikana," alisema Gamondi.

Yanga inajiandaa na mchezo wake wa kwanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria utakaochezwa Novemba 24  ugenini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: