Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba kuanzia Chalinze kesho

Simba 40x640.png Simba kuanzia Chalinze kesho

Tue, 18 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Rasmi Uongozi wa Simba SC umetangaza kuzindua Kampeni za Hamasa kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mabingwa watetezi Wydad Casablanca ya Morocco.

Simba SC itacheza dhidi ya Wydad Casablanca Jumamosi (April 22) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikiwa na lengo la kufuzu kuelekea Nusu Fainali ya Michuano hiyo kwa mara ya kwanza.

Meneja wa Habari na Mawasilino Simba SC Ahmed Ally amezungumza na waandishi wa Habari leo Jumanne (April 18) na kusema: “Furaha ya Wanasimba haijakamilika, wanatudai nusu fainali. Tunawaomba Wanasimba tushikamane, pamoja na ubora alionao Wydad lakini tukisimama kama Simba hakuna linaloshindikana.”

“Lazima tukawaadhibu Wydad, lazima tuwaonyeshe yaliyomo yamo. Itakuwa ni siku ya Eid siku hiyo, njoo umeshiba pilau lako, umewaka uje tuhakikishe Wydad wanakaa.”

“Kuhusu hamasa tumeshaanza, mara nyingi tunakuwa na uzinduzi, uzinduzi utafanyika kesho mkoani Pwani, wilaya ya Chalinze kwenye tawi la Wekundu wa Chamazi.”

“Kwa Wanasimba ambao wanataka kwenda Chalinze kwenye uzinduzi tutaondoka kutokea Ubungo sheli kesho saa 3 asubuhi. Tutasimama kidogo Mbezi Mwisho, Kibaha, Mlandizi alafu tunakwenda kufanya balaa Chalinze.”

Kuhusu Tiketi za mchezo, Ahmed Ally amesema tayari wameshaanza kuuza tiketi hizo, hivyo amewataka Mashabiki na Wanachama kuchangamkia Fursa kwa kununua tiketi kwa wingi mapema, ili kuepuka usumbufu.

“Tunazo tiketi za Simba Executive, hii ni imekuja kwa ajili ya makampuni, taasisi, mashirika kupata tiketi kwa ajili ya wafanyakazi wao. Tiketi moja ni Tsh. 20,000 na wakinunua watapewa na gate pass ya kuingiza gari ambalo watalitumia kuja uwanjani.”

“Lakini pia tunayo Platinum, hii ni special package ambayo inapatikana kwa Tsh. 150,000 kwa ajili ya watu kuja uwanjani kushangilia Simba yao. Mpaka jana tulikuwa tumeshauza 32, kwa anayehitaji aweke oda yake sasa.”

“Mechi ya Simba na Wydad ndio mechi kubwa barani Afrika wiki hii sababu tunakutana na bingwa mtetezi lakini pia watu wanataka kuona Mnyama akivunja historia ya mwaka 2003 kumtoa bingwa mtetezi.”

“Wydad tunaenda kumfanyia balaa, hawataamini. Dhamira yetu ni kuvunja mwiko wa kuishia robo fainali, kumtoa Wydad. Tunakiri wametuzidi ubora lakini tunaamini tunakwenda kuwatoa. Safari hii tunaitaka nusu fainali.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: