Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba kama inajitekenya

SIMBA 388 1140x640.png Simba SC

Mon, 3 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Dirisha la usajili limefunguliwa jana Jumamosi, Julai Mosi, sasa ni ruksa klabu kuanza usajili wa wachezaji ili kutibu udhaifu wa vikosi vyao kutokana na upungufu wa msimu ulioisha.

Tangu kumalizika kwa msimu huu na Yanga kutawazwa kuwa bingwa wa mara 29, viongozi wa Simba wamekuwa wakijinasibu kurudi kibabe kwa kufanya usajili mkubwa kwa ajili ya msimu ujao.

Kauli ya karibuni ya viongozi hao imetoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Simba, Salumu Abdallah ‘Try Again’ na tambo za msemaji wa klabu hiyo, Ahmed Ally kudai kwamba wakitangaza usajili wao, basi bahari itatawanyika na umeme kukatika.

Mbali na kauli hizo za kutamba kufanya usajili mkubwa lakini ukiangalia uhalisia wa maneno hayo hayakubaliani na hali halisi inavyoonekana ndani klabu hiyo. Simba yenye masikani yake Kariakoo jijini Dar es Salaam mpaka sasa imeshaachana na jumla ya wachezaji tisa.

TUANZE NA WAGENI

Kabla ya kufunguliwa kwa dirisha la usajili, Simba imewatema wachezaji wa kigeni wanne wakiwemo kina Mohamed Ouattara, Victor Akpan, Nelson Esor-Okwa na Augustine Okrah na kumbuka mwanzoni iliachana na straika Dejan Georgijevic.

Pamoja na wachezaji hao bado Simba imebakiwa na wachezaji tisa wa kigeni ambao ni Henock Inonga, Jean Othos Baleke, Joash Onyango, Clatous Chama, Saido Ntibanzokiza, Pape Ousmane Sakho, Sadio Kanoute, Peter Banda na Ismail Sawadogo.

USAJILI WATATU TU

Kama itabaki na wachwezaji hao wa kigeni basi itatakiwa kusajili wachezaji watatu tu wa kigeni ili kukidhi vigezo vya kufikisha 12 wanaotakiwa kikanuni. Usajili wa wachezaji watatu unaweza kuwa mkubwa na wa kutisha?

Lakini katika fununu za usajali, Simba inatajwa kumalizana na winga wa Rayon Sport ya Rwanda Mcameroon, Willy Onana. Pia, inatajwa kuwa mbioni kukamilisha usajili wa kipa kutoka Brazil.

Kama itakamilisha sajili hizo mbili, Simba itabakiwa na usajili wa mchezaji mmoja tu wa kigeni. Bado unaamini itafanya usajili mkubwa? Je, huyo mmoja atasajiliwa katika idara gani ili kukidhi matatizo ya kikosi hicho?

Kweli winga Onana, Mbrazili na mchezaji mmoja aliyebaki unaweza kuwa usajili mkubwa Simba?

SHIDA ZA SIMBA

Ifahamike Simba inatakiwa kupata beki wa kati, viungo wawili, mkabaji na wa ushambuliaji na straika mmoja. Yaani beki wa kumsadia Onyango, viungo wawili kuwasaidia Kanoute, Chama na Mzamiru Yassin bila ya kusahautraika kwa ajili ya kumpa changamoto Baleke.

Usajili huo unaweza kufanyika kama Simba itachaana na wachezaji wengine wawili wa kigeni kati ya tisa waliobaki kikosini.

Hapo itatatua shida ya msimu uliopita ya kukosa wachezaji wa kuamua mechi pindi, Kanoute, Mzamiru na Chama walipokosekana uwanjani. Lakini kwa kusajili wachezaji watatu wa kigeni sidhani kama itakidhi mahitaji ya kikosi hicho kiasi cha na kutamba kufanya usajili mkubwa.

KWANINI MKUDE?

Pia, Simba imeachana na wazawa wanne ambao ni Jonas Mkude, Gadiel Michael, Erasto Nyoni na Beno Kakolanya. Mashabiki wa Simba hawalalamiki timu hiyo kuachana na Gadiel na Nyoni lakini wanajiuliza kwanini Mkude? Simba haikufanya utafiti wa kutosha kumuacha Mkude kama ilivyokosea ilipoachana na Kakolanya.

Ni kwasababu hakuna wachezaji wazawa wanaoweza kuziba nafasi za Mkude na Kakolanya nje ya Azam FC, Yanga na Simba yenyewe.

DILI LA BAJANA

Kama Simba isingeachana na Kakolanya isingehangaika kusaka kipa wa kigeni, bali ingetumia nafasi ya mgeni kusajili mchezaji muhimu sehemu inazohitaji kwa ajili ya msaada kama kiungo au straika.

Pia, kama ingebaki na Mkude ingekuwa katika mikono salama pale Kanoute anapokusanya kadi zake za njano kwasababu Mkude anaweza kutoa ushindani dhidi ya timu kubwa kama Yanga, Azam na Singida Fountain Gate.

Kwa sasa Simba kama inahitaji kuziba eneo la kiungo wa chini baada ya kuachana na Mkude inapaswa kusajili mchezaji wa kigeni, gharama zake si ndogo.

Awali tetesi za usajili ziliihusisha Simba na kiungo wa Azam FC, Sospeter Bajana lakini dili hilo linaonekana kufa kibudu baada ya nyota huyo kuongeza mkataba Chamazi.

Baada ya dili hilo kufa viongozi wa Simba walipaswa kumeza mate ya akili na kuangalia namna ya kuishi na kubaki na Mkude.

Nungunungu kama anavyofahamika na wengi angeachwa tu kama Simba ingekuwa na mtu mwenye ukamilifu katika eneo analocheza.

MKUDE SHIDA NINI?

Mengi yanazungumzwa kuhusu kiungo huyo aliyedumu Simba kwa takribani miaka 13 lakini kubwa ni utovu wa nidhamu.

Simba ilipaswa kuangalia uwezo wa Mkude na mahitaji yao kwanza kabla ya kuangalia udhaifu wake wa kinidhamu. Mpira sio mchezo mtakatifu kiasi cha kudhani kuachana na mchezaji mtukutu ndio tiba ya kumaliza matatizo ndani ya Simba.

Kina Try Again wanapaswa kufahamu mtoto akijisaidia kwenye mkono hatukati kiganja. Pia, mwana umleavyo ndivyo akuavyo. Jambo la msingi,Simba ilipaswa kuanza usajili wakati Ligi Kuu ilipomaliza dulu la kwanza na sio kusubiri hadi msimu umeisha kabisa.

Mpaka kufika nusu ya msimu timu walitakiwa wawe washajua shida ya kikosi chao ilikuwa katika maeneo gani. Bado nausubiri usajili mkubwa wa Simba. Nimekaa pale!

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: