Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba inahitaji mapumziko?

Cadena Simba Nm Simba inahitaji mapumziko?

Wed, 15 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa mujibu wa sheria za mchezo wa masumbwi ukipoteza pambano kwa Knock Out (KO), bondia hutakiwa kupumzika siyo chini ya miezi mitatu kabla ya kupanda ulingoni tena. Unajua kwa nini? KO mara nyingi huacha majeraha mwilini. Huacha vidonda. Huacha maumivu makali. Bondia anahitaji muda wa kutosha kujitibu na kujiandaa kimwili na kiakili kuelekea pambano lingine.

Kama sheria za ndondi au masumbwi zingetumika kwenye soka nadhani Simba walitakiwa kupumzika. Simba ni kama wamejeruhiwa sana na Yanga. Zile tano dhidi ya Yanga zimeacha majeraha makubwa sana kwa Mnyama. Zimeacha vidonda.

Mnyama anahitaji mapumziko. Mnyama anatakiwa kujitibu kwanza kimwili na kiakili kabla ya kurejea tena uwanjani. Hakuna kitu kigumu kwenye maisha kama kukubali wakati umeanguka. Huwa ni mtihani mkubwa sana.

Wako watu wanafilisika na hawataki kukubali kama maisha yamebadilika.Bado wanataka kuishi maisha yaleyale ya kitajiri. Usipokubali anguko lako ni vigumu sana kupona. Ni vigumu sana kurejea kwenye maisha yako ya awali.

Ukianguka kwenye jambo lolote kwanza kubali na kisha angalia unatokaje ulipoanguka. Simba wanatakiwa kutulia na kukubali kuwa walianguka dhidi ya Yanga. Wasipokubali na kujipanga upya, hiki kipigo kitawasumbua msimu mzima. Kipigo cha 5-1 dhidi ya Yanga kitawafanya wapoteze malengo yao yote ya msimu.

Ukitazama mchezo uliofuata wa Simba dhidi ya Namungo utagundua kuwa Simba wanahitaji mapumziko. Ni kama bado wana wenge la kufungwa na Yanga. Ni kama kidonda bado kibichi. Sio kwamba Namungo na timu rahisi, hapana.

Najua kuwa Namungo wana timu nzuri. Najua hata Yanga walishinda kwa mbinde sana dhidi yao. Najua Azam FC pia wamefungwa na Namungo msimu huu. Ni timu nzuri, lakini imecheza na Simba ambaye bado anaumwa. Simba ambaye kidonda chake bado kibichi.

Simba wanahitaji sana kanuni kwenye masumbwi kujiweka sawa. Kwa sasa karibu kila kitu pale Simba hakiendi sawa. Naona wameanza sasa kushikana uchawi. Huu ni muda wa Simba kujua walipoanguka, sio hiki kinachoendelea.

Tangu kufungwa tano kumekuwa na hisia kali. Nazisikia kelele za baadhi ya mashabiki kutaka mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu ajiuzulu. Nasikia pia sauti za kutaka marekebisho pia ya katiba yao.

Ukisikia hoja zote zinazotolewa unagundua kabisa kuwa Simba bado anaumwa ugonjwa wa 5-1 dhidi ya Yanga. Simba bado hajapona. Hata Mangungu akiondoka leo zile tano hazifutiki. Hata kama katiba kufanyiwa mabadiliko, bado zile 5-1 hazibadiliki.

Mnyama alifungwa kwa sababu za kiufundi kabisa uwanjani. Mnyama alifungwa kwa sababu ya kuzidiwa ubora na Yanga. Simba sio timu ya kwanza kufungwa bao tano na Yanga. KMC, JKT Tanzania ni baadhi tu ya timu zilizopokea kipigo kama hicho msimu huu.

Huko duniani kuna timu nyingi sana zilizofungwa mabao kama hayo na zaidi. Arsenal, Bayern Munich, Manchester United, Real Madrid ni baadhi ya klabu ambazo zimewahi kuchezea kichapo kama hicho na zaidi kwa nyakati mbalimbali. Kwenye mpira sio matokeo mageni.

Ni kweli kiongozi anaweza kuwajibika kwa sababu ya matokeo mabaya, lakini ni lazima uwe tayari umeshatambua tatizo. Tatizo la nchi yetu, siasa za mpira zina nguvu sana kuliko utaalamu.

Simba waliihitaji kanuni ya masumbwi kutuliza akili zao. Simba walihitaji kanuni ya masumbwi kujipanga upya. Wasipokubali kuwa mechi yao dhidi ya Yanga ya mzunguko wa kwanza imepita, watakuja kupigwa tano nyingine.

Soka ni mchezo wa wazi, kila mtu anaona ubora wa Yanga. Simba sio timu mbaya kama wengi wanavyodhani. Inahitaji maboresho kidogo sana na utulivu wa akili kufikia malengo yao msimu huu. Lakini kama siasa za nje ya uwanja hawatazikabili vizuri, wanaweza kuwa na msimu mbaya kwa mara nyingine.

Simba imecheza mechi nane za Ligi Kuu msimu huu ikishinda sita, sare moja na kupoteza moja. Siyo matokeo mabaya hata kidogo. Katika safari ya Ligi Kuu ina mechi 30, kupoteza mchezo dhidi ya Yanga hakuwezi kuwanyima ubingwa Simba kama watachagua kuuheshimu mpira.

Mambo ya marekebisho ya katiba, mambo ya kutaka Mangungu kuondoka sioni uhusiano wake wa moja kwa moja na Simba kufungwa 5-1. Wakati mwingine ni vyema kukubali ubora wa mpinzani wako na kumheshimu. Simba ingeweza kufungwa hata mabao 7-1 siku ile kwa Mkapa.

Soka ni mchezo wa makosa. Ukifanya makosa mengi dhidi ya mpinzani anayejua namna ya kutumia makosa hayo utaadhibiwa tu. Utapigwa nyingi. Mambo ya kunyoosheana vidole yanavunja sana mioyo wachezaji.

Kuna propaganda ya Shomary Kapombe na Mohammed Hussein 'Tshabalala' kuchoka. Naona imewaingia wengi. Tatizo letu kuna muda tunahitaji tu sura mpya. Mpira wa Tanzania una mechi chache sana kwa msimu. Ni wachezaji wachache wanafikisha mechi 40 mpaka 50 kwa msimu. Bado ligi yetu haitumii nguvu sana. Huwa sielewi hoja ya Kapombe na Tshabalala kuchoka inatoka wapi. Wanaweza kufanya makosa tu kama wanavyofanya wachezaji wengine lakini kwa mpira wetu, bado wana uwezo wa juu kabisa. Clatous Chama bado ndiye kiungo mbunifu zaidi kwenye ligi yetu. Hawezi kupotea tu kirahisi. Yule Saido Ntibanzonkiza ni mwaka jana tu alishinda Tuzo nne mwishoni mwa msimu. Huwezi kulala tu kuamka akawa amekwisha ubora.

Kama Simba watakubali kuwa mechi yao na Yanga imepita wanaweza kujikusanya na kusonga mbele. Kwenye timu ambayo ina washambuliaji kama Moses Phiri na Jean Baleke, haiwezi kupotea kirahisi. Simba sio timu mbovu hata kidogo, inahitaji tu marekebisho kidogo wakati wa Dirisha.

Kelele za kutaka mwenyekiti Murtaza Mangungu aondoke kwenye nafasi yake kwa sababu ya kufungwa na mtani nadhani ni kumuonea tu. Kutuhumu baadhi ya wachezaji kuwa walicheza chini ya kiwango kwenye mechi ile ni kuwakosea tu kama huwezi kuthibitisha tuhumu dhidi yao. Mchezo wa soka uheshimiwe. Ni kweli Simba imefungwa tano na Yanga, lakini haina timu mbovu kivile kama wengi wanavyodhani. Simba wanahitaji mapumziko tu kidogo ili kujitibu kimwili na kiakili, na kisha kurejea uwanjani kwa kishindo.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: