Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba bado ilimhitaji Mkude

Mkude X Allende Simba bado ilimhitaji Mkude

Fri, 5 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Jonas Mkude ‘Nungunungu’ ni ‘Kuni ya akiba inayoivisha mboga.’ Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kuhusu kiungo huyo aliyedumu ndani ya Simba kwa misimu 13 na baadaye kuamua kujiunga na watani zao Yanga.

Ndani ya Simba kiungo huyo ametwaa mataji yote ya ndani isipokuwa ya michuano ya kimataifa ambayo amecheza hadi hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Mwaka 2017, Simba ilikuwa na kiungo, James Kotei ambaye alikuwa akicheza kwa ubora hadi kocha wa wakati huo, Joseph Omog alikuwa akimweka nje Mkude jambo ambalo mashabiki hawakukubaliana nalo, walipiga kelele za kutaka acheze na ilikuwa hivyo.

Baadaye akarudi katika kikosi cha kwanza lakini mwisho wa msimu uliopita mkataba wake ulipoisha, kiungo huyo alifanya uamuzi mgumu wa kusaini mkataba wa mwaka mmoja na Yanga, usajili ambao ulikuwa gumzo huku wengi wakihofia kama ataweza kupata nafasi chini ya kiungo Khalid Aucho kutokana na ubora na kujijengea ufalme katika eneo hilo.

Hofu hiyo ilidhihirika kwani Mkude hana namba ya kudumu kikosini na amekuwa akipata nafasi mara moja moja hadi Jumamosi iliyopita alipoibuka shujaa kwa kumudu kucheza dakika 90 kwenye mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Yanga ilipotoka suluhu nyumbani dhidi ya Mamelodi Sundowns.

Mwanaspoti limefanya tathimini kwa kuangalia viungo waliopita Simba kabla na baada ya Mkude kutimka na kubaini bado alikuwa anahitajika kwani ana uwezo wa kuendelea kushindana huku wengi wa viungo waliopita Msimbazi wakishindwa kuhudumu hata kwa miaka mitatu.

GERSON FRAGA

Simba ilimsajili Fraga Juni 25, 2019 kwa mkataba wa miaka miwili akitokea ATK ya Ligi Kuu India, akiwa miongoni wa Wabrazili waliosajiliwa msimu huo, akiwamo Tairone Santos na Wilker Henrique.

Fraga aliichezea Simba msimu wa 2019-2020 na kuifungia mabao matatu ya Ligi Kuu na moja kwenye nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) walipoifumua Yanga kwa mabao 4-1.

Hakuweza kumalizia msimu wake wa pili kama mkataba wake ulivyokuwa unamtaka (alikuwa na mkataba wa miaka miwili) kutokana na kupata shida kwenye goti. Majeraha hayo aliyapata kwenye mchezo dhidi ya Biashara United Simba ikiibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0.

Majeraha hayo yalimweka nje kwa muda mrefu hadi hapo Simba ilipoamua kuachana naye na msajili kiungo mwingine kutoka Rwanda, Taddeo Lwanga.

TADDEO LWANGA

Katika dirisha dogo msimu wa 2020/21 Simba ilimsajili Lwanga kama mchezaji huru akitokea Misri na mwanzo alipokuwa akitumikia kikosi hicho alionekana mchezaji wa daraja la kawaida.

Lakini baada ya kuonyesha kiwango bora, Lwanga alikuwa mchezaji wa kutegemewa katika nafasi ya kiungo mkabaji.

Ujio wa Lwanga ndani ya kikosi cha Simba ulimzima kabisa Mkude aliyekuwa na uhakika wa kucheza katika nafasi hiyo lakini baadaye alianza kuonekana mchezaji wa kawaida tu na hakuchukua muda kwani aliondolewa baada ya kupata majeraha na kukaa nje kwa muda uongozi uliamua kuachana naye.

SADIO KANOUTE

Ni usajili ambao ulifanyika dirisha kubwa la usajili na kudumu kwa misimu mitatu tofauti na wachezaji wengi waliopita eneo hilo kwa miaka ya hivi karibuni.

Kiungo huyo kutoka klabu ya Al-Ahli Benghazi ya Libya amehudumu kwenye eneo hilo kwa misimu mitatu sasa akijiunga na timu hiyo msimu wa 2021/2022.

Ubora wake kwenye eneo hilo ulithibitishwa kwenye misimu miwili ya mwanzo sasa amekuwa ni mchezaji ambaye anabadilishwa namba chini ya Kocha Abdelhak Benchikha, raia wa Algeria ambaye anamtumia maeneo mawili akicheza kama kiungo wa chini mara nyingine akimsogeza mbele.

VICTOR AKPAN

Hakuna aliyekuwa anatarajia usajili huu ungeweza kufanyika ndani ya kikosi cha Simba lakini hilo liliwezekana kwa mamilioni ya fedha kuwatoka matajiri wa Simba kuinasa saini ya kiungo huyo kutoka Coastal Union.

Mnigeria huyo alisajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili kwa lengo la kuziba pengo la Lwanga ambaye alitemwa na Simba kutokana na majeraha ya muda mrefu yaliyokuwa yamemweka nje ya uwanja.

Akpan hakuwa na nafasi ndani ya kikosi cha Simba alihudumu kwa miezi sita tu na baadaye uongozi ukamtoa kwa mkopo kwenda Ihefu FC ambako ndio anacheza hadi sasa.

ISMAEL SAWADOGO

Baada ya Akpan kushindwa kuonyesha uwezo, kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alipendekeza usajili wa kiungo huyo ambaye hakuweza kufiti katika eneo hilo kwani alicheza miezi sita tu na kuonyeshwa mlango wa kutokea.

Sawadogo alisajiliwa Simba wakati wa dirisha dogo Januari 2023, kutokana na kushindwa kuendana na kasi ya timu hiyo, hivyo uongozi ulichukua uamuzi wa kuachana na kiungo huyo.

BABACAR SARR

Kijiti kilichomshinda Sawadogo kipo mikononi mwa Babacar Sarr ambaye tayari amejihakikishia nafasi kwenye eneo la kiungo mkabaji akimfanya Sadio Kanoute atapetape eneo la kucheza kulingana na mipango ya kocha.

Ubora wake unaendelea kumpa namba kikosini tofauti na viungo kama Sawadogo na Akpan ambao walikosa kabisa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza na kujikuta wakitumika kwa miezi sita tu Msimbazi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: