Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba SC wapewa mbinu za kuikabili Jwaneng

IMG 6374.png Kikosi cha Jwaneng Galaxy

Fri, 1 Dec 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Simba SC ikitarajia kushuka dimbani kesho nchini Botswana kucheza mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi B, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy, ushauri wa bure umetolewa kwa wachezaji na Benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Abelhak Benchikha.

Simba SC inakwenda katika mchezo huo ikiwa imevuna alama moja, kufuatia sare ya 1-1 dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast, hivyo inapaswea kusaka ushindi ama sare dhidi ya Jwaneng Galaxy ili kufufua matumaini ya kuwa moja ya timu mbili zitakazotinga Robo Fainali ya michuano hiyo msimu huu 2023/24.

Mtaalam wa soka Jonas Tiboroha amesema, ili Simba SC ikaambulie walau pointi moja dhidi ya Jwaneng inatakiwa kupaki basi ikijifanya kushambulia itakachokipata haitoamini jambo lililowaponza wababe wao Wydad waliolala 1-0 nyumbani mbele ya timu hiyo ya Botswana iliyowahi kumng’oa Mnyama kwenye mechi za mchujo za CAF misimu miwili iliyopita.

Tiboroha amesema Benchi la Simba linatakiwa kuwajaze wakabaji wote, Shomary Kapombe, Israel Mwenda, Che Malone Fondoh, Kennedy Juma, Henock Inonga, Mzamiru Yassin, Sadio Kanoute wakakabe na sio kushambulia, kwani wakijichanganya wanaweza kujitibulia kama Wydad.

“Jwaneng waliwasumbua nakumbuka waliwaondoa na wakati huo Simba SC iko vizuri, kwa Simba SC haipo kivile, hivyo wakipaki basi tu hakuna namna ni ushauri tu, wakiwa wanajipanga kufanyia kazi mapungufu katika Dirisha Dogo,” amesema Tiboroha aliyeamua kukaa mbali na soka kwa sasa, baada ya kufanya kazi na klabu za Young Africans na Azam FC.

Naye nyota wa zamani wa Simba SC, Fikiri Magoso amesema, timu hiyo inapitia katika wakati mgumu hivyo wenye kurejesha furaha ni wachezaji kuhakikisha wanapambana na kutambua thamani ya uwepo wao Msimbazi.

“Hakuna namna ni wachezaji kujitoa,” amesema Magoso.

Simba SC inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Kundi B, ikiwa na alama moja sawa na Asec Mimosas ya Ivory Coast, huku Jwaneng Galaxy ikiwa kileleni kwa kufikisha alama tatu.

Wydad Casablanca ya Morocco inaburuza mkia wa Kundi hilo. Baada ya kupoteza mchezo wake wa kwanza nyumbani kwa kufungwa 1-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: