Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba SC mambo ni mawili tu

Simba Power Ms.jpeg Simba SC mambo ni mawili tu

Thu, 21 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba inarudi uwanjani leo ikitoka kupata sare ugenini kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Power Dynamos ya Zambia, itakapoialika Coastal Union kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar, huku kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akisema wana mambo mawili tu.

Timu hizo zinavaana kwenye mechi hiyo ya raundi ya tatu ya Ligi Kuu na huenda udugu baina yao utawekwa kando kuanzia saa 10:00 jioni kutokana na sababu kuu moja, nafasi ambayo kila timu ipo kwa sasa katika msimamo wa ligi hiyo.

Licha ya kupata ushindi katika mechi mbili za mwanzo dhidi ya Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji, wenyeji Simba wamejikuta wakiwa katika presha kubwa kutoka kwa wapinzani wawili wa mbio za ubingwa, Yanga na Azam FC zilizopo juu yake na namna pekee ya kukabiliana nao ni kupata ushindi ili isiwape faida ya kuongeza pengo la pointi

Coastal yenyewe imeanza vibaya msimu huu kwa kufungwa mchezo mmoja na Dodoma Jiji, kisha kutoka sare na Mtibwa Sugar jambo lililoifanya iwe nafasi ya 14 katika msimamo na pointi moja pekee.

Wenyeji Simba ambao awali waliiomba mechi hiyo ihamishiwe Azam Complex lakini ikakataliwa na Bodi ya Ligi (TPLB) kwa kukosa sababu za kufanya hivyo, itaingia kwenye mechi hiyo ikiwa na historia nzuri ya ubabe dhidi ya Wagosi na hilo linajidhihirisha katika michezo 10 iliyopita ya Ligi, Wekundu wameibuka na ushindi mara nane na mbili ziliisha kwa sare.

Ikumbukwe Coastal haijawahi kushinda dhidi ya Simba katika Ligi Kuu tangu iliposhinda 1-0 katika mechi iliyopigwa Machi 23, 2014 ikiwa ni sawa na miaka tisa na miezi mitano au siku 3,470.

Kana kwamba haitoshi, Simba inaingia katika mechi hiyo ikiwa na shauku ya kuendeleza rekodi nzuri ya kutopoteza mechi 25 mfululizo za Ligi Kuu, ikiisaka rekodi iliyowekwa na Yanga ya kucheza mechi 49 mfululizo bila kupoteza.

Katika mchezo wa leo, Simba itaendelea kuwakosa Aubin Kramo aliye majeruhi na Aishi Manula ambaye bado hajawa fiti baada ya kupona majeraha ya muda mrefu ya nyama za paja.

Kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alisema anaingia katika mchezo huo akiwa na malengo mawili ya kuvuna pointi tatu na kujiandaa na mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos.

“Nawaheshimu Coastal, wana wachezaji wazuri na wazoefu, lakini Simba tuna wachezaji wazuri. Malengo yetu ni kucheza vizuri na kupata ushindi, pia ninaweza kuitumia mechi hii kama kipimo cha mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Robertinho.

Kocha wa Coastal Union, Mwinyi Zahera alisema wamejiandaa vyema kukabiliana na Simba.

“Simba ni timu kubwa tunalifahamu hilo, ndio maana tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunacheza nao na kupata matokeo mazuri. Wachezaji wangu wako tayari kwa mchezo na morali yao iko juu,” alisema Zahera.

Mara baada ya mechi hiyo ya Uhuru, usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Azam FC itaikaribisha Singida Fountain Gate katika mchezo ukaopigwa kuanza saa 1:00.

Ni mechi ya kusaka nani zaidi kati yao mbali na hesabu za pointi tatu kwani mara mbili zilipokutana katika ligi, kila moja imeibuka na ushindi dhidi ya mwenzake.

Azam, ilianza kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 msimu uliopita na katika mechi ya marudiano ikachapwa bao 1-0.

Wageni Singida wanaingia katika mechi hiyo wakiwa na pigo la kung’atuka kwa kocha mkuu, Ernst Middendorp aliyeachana na timu hiyo kwa kile alichodai kuingiliwa katika majukumu yake na uongozi wa timu hiyo.

Wakati Azam ikiwa na mwanzo mzuri msimu huu, tofauti na Singida ambayo katika mechi mbili za mwanzo za Ligi Kuu.

Wenyeji wamepata ushindi katika mechi zote mbili, wakiifunga Tabora United kwa mabao 4-0, kisha kuilaza Tanzania Prisons kwa 3-1.

Singida yenyewe imeanza kwa suluhu katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Prisons na Tabora United.

Kocha wa Azam, Bruno Ferry alisema wanaingia wakiipa heshima Singida.

“Mwezi ujao tutakuwa na mechi nne, hivyo ni muhimu kuingia tukiwa tumefanya vizuri hivi sasa. Mechi hii itakuwa pambano kubwa, wana kocha mpya na tunaamini hiyo itakuwa chachu ya kuwapa hamasa wachezaji wao ili kumuonyesha wanastahili kupata nafasi, ila sisi tumewaonyesha wachezaji nini wanatakiwa kufanya,” alisema Ferry.

Nahodha wa Singida, Beno Kakolanya alisema pamoja na muda mfupi waliopata kujiandaa na mechi hiyo, watajitahidi kuhakikisha wanashinda.

“Tumetoka kucheza mechi ngumu dhidi ya Future, lakini kwa muda tuliopata tumejiandaa vizuri kwa mechi ya Azam. Kilichotokea kuhusu kocha hatuwezi kukiweka kichwani na tunachokiangalia ni kuisaidia timu kushinda,” alisema Beno Kakolanya.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: