Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba SC isijifariji, ni lazima ijue tatizo kwanza

Simba Nguvu Moja Simba SC isijifariji, ni lazima ijue tatizo kwanza

Mon, 15 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Lazima uwe na huruma kwa kocha ambaye ametoka kutwaa Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), kukutana na hali ya matokeo yasiyoridhisha kama anayopitia kwa sasa Kocha Abdelhak Benchikha katika klabu ya Simba.

Si kutwaa Kombe la Shirikisho pekee, bali ametoka kutwaa ubingwa wa Super Cup na USM Alger ya kwao Algeria dhidi ya Al Ahly ya Misri katika mechiinayozikutanisha bingwa wa Afrika na bingwa wa Kombe la Shirikisho.

Wasifu wake umejaa mafanikio na makombe katika klabu alizopitia za Club Africain, UMM Salal, RS Berkane, ambayo alitwaa nayo ubingwa wa Super Cup mwaka 2022 na Difaa d’El Jadida.

Huyu ndiye kocha ambaye anasumbuka kwa sasa katika Ligi Kuu ya Tanzania akiwa na Simba, moja ya timu kubwa Tanzania na iliyojitengenezea jina kubwa Afrika kiasi cha raia huyo wa Algeria kushawishika anaweza kufanya makubwa iwapo ataongeza ujuzi wake ndani ya klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi.

Ameikuta klabu ikiwa imeanza kutekeleza mikakati ya mageuzi kutoka mfumo wa zamani wa umiliki wa klabu, uongozi na uendeshaji hadi mfumo wa kisasa ulioruhusu klabu kukaribisha wawekezaji kumiliki asilimia 49 ya hisa zake, huku ikibadili muundo wa uongozi na uendeshaji.

Simba sasa ina Bodi ya Wakurugenzi kama chombo kikuu kinachotakiwa kuwajibika kwa wawekezaji, kikiwa na jukumu la kupanga na kuelekeza, huku kikiwa na Sekretarieti inayoongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) ambaye anashughulikia shughuli za kila siku na ndiye anayetakiwa kuwajibika kwa bodi kuonyesha ni kiasi gani amefanikisha mipango na maelekezo yao.

Amekuta mpango huo wa mabadiliko ya muundo wa umiliki ukiwa umekwama baada ya Kamisheni ya Ushindani wa Haki (FCC) kukosoa baadhi ya vipengele, hasa cha chombo kilichoundwa kumiliki asilimia 51 ya hisa, Simba Sports Club Company, kilichoanza kubeba majukumu ya Simba Sports Club hata kabla ya mabadiliko kukamilika, huku mgawanyo wa hisa ukiwa tofauti na sharia za nchi.

Hadi sasa nguvu za Ofisa Mtendaji Mkuu kama kiongozi wa shughuli za kila siku hazionekani sana. Ni kama vile bado klabu inaongozwa na Kamati ya Utendaji ambayo Mwenyekiti ndio msimamizi mkuu wa sekretarieti.

Kila klabu inapofanya vibaya, mashabiki, hasa wale walioibuka kama ndio wasemaji wakuu baada ya kutengenezwa na vyombo vya habari vya mitandaoni (online TV) huvurumisha shutuma zao kwa Mwenyekiti wa klabu, Murtaza Mangungu wakati kiongozi huyo ni Mjumbe tu wa Bodi ya Wakurugenzi inayotakiwa iwe chombo kinachopanga na kuelekeza.

Katika hali ya kawaida, Mangungu alitakiwa awe ndiye wateuliwa mwenyekiti au ateue mwenyekiti wa kuongoza bodi kutokana na ukweli ndiye mwenyekiti aliyechaguliwa na wanachama wa Simba inayotakiwa imiliki hizo asilimia 51 za hisa. Lakini ni mjumbe tu ambaye hapaswi kubebeshwa lawama zozote binafsi zaidi ya kuwajibika kama wajumbe wengine wa bodi ya wakurugenzi.

Hana jukwaa jingine zaidi ya mkutano mkuu wa klabu ambao ni kama hauna tena nguvu juu ya timu ya soka ya Simba.

Lawama nyingine huelekezwa kwa Salim Abdallah Muhene, maarufu kama Try Again, ambaye aliteuliwa na Rais wa Heshima wa Simba, Mohamed Dewji, ambaye anatakiwa awe mmoja wa wawekezaji, kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi.

Pamoja na kwamba nafasi yake haimpi fursa ya kusimamia shughuli za kila siku, bado analaumiwa anahusika na kuboronga kwa Simba ingawa haielezwi anaboronga vipi.

Tuhuma za kusajili wachezaji wanaoitwa wabovu na zile za kula asilimia ya fedha zinazodaiwa kutolewa na mwekezaji, huwa hazimlengi mtu kwa jina wala nafasi, bali huelekezwa kwa watu wanaoitwa viongozi.

Pia iko Bodi ya Wakurugenzi ambayo ingestahili lawama zote zinazohusu mipango mibovu inayosababisha Simba iwe katika hali inayoelezwa sasa kuwa ni mbaya. Hii ni bodi ambayo imeepuka shutuma zozote wala sifa za timu kufanya vibaya. Haihusishwi na wajumbe wake kutumia fedha vibaya, au bodi kusajili wachezaji wabovu au kutoidhinisha fedha za kutosha kwa ajili ya usajili. Hii bodi ipo tu na haihusishwi na lolote linaloendelea klabuni.

Yupo pia mwekezaji Mohamed Dewji ambaye inasadikiwa ndiye anayetoa fedha za usajili, lakini wachezaji hawanunuliwi wale wanaotegemewa kufanya maajabu. Wakati msimu unaanza Mo ndiye aliyehusishwa na usajili wa Che Fondoh Malone kutokana na nguvu kubwa kuhitajika kumng’oa kutoka Cottonsport ya Cameroon.

Mwekezaji amekuwa akikaririwa kusema anatoa fedha za usajili na hivi karibuni alifanya mahojiano nje ya nchi na kutangaza alishainunua Simba miaka mitano iliyopita, wakati miezi michache kabla aliandika katika akaunti yake ya Twitter kuwa “Miaka sita imepita sasa, lakini mabadiliko hayakamiliki.”

Au kwa maana nyingine ya kauli yake ya hivi karibuni ni kuwa aliinunua Simba mwanzoni kabisa mwa mchakato wa mabadiliko, kitu ambacho kinaweza kusababisha utata mkubwa kutokana na baadhi ya watu kuamini hizo Sh20 bilioni zilizotakiwa ziwekezwe Simba, hazijaingia hadi sasa.

Kikosini kuna mambo yake pia. Kocha ameingia katika kipindi ambacho hakupata muda wa kuwasoma vizuri wachezaji na kujenga kikosi na hivyo kila mechi kwake ni fainali ambayo inahitaji nguvu kubwa kushinda; iwe mechi ya Ligi Kuu, ya Kombe la Shirikisho au ya Ligi ya Mabingwa.

Muda pekee alioupata ni wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2024 visiwani Zanzibar ambako Benchikha alitaka wachezaji wote wa kikosi cha kwanza wasiruhusiwe kupumzika ili apate muda wa kujenga kikosi.

Kweli alijaribu vijana kama Ladack Chasambi, Israel Mwenda, Hussein Kazi, Jimmyson Mwanuke na Shaaban Idd Chilunda.

Wakati akijaribu nyota hao chipukizi, alijikuta akiwapoteza wachezaji kama Jean Baleke, James Phiri na John Bocco, ambaye ameamua kujikita katika mafunzo ya ukocha. Kwa maana hiyo mradi wake wa kutumia Kombe la Mapinduzi kujenga kikosi ukaingia mushkeli.

Alichoachwa nacho ni kuendelea kutumia wachezaji wazoefu kuogopa kujiweka hatarini, lakini nao wamekumbana na tatizo la uchovu linaloweza kuwa moja ya sababu za timu kuendelea kufanya vibaya baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa.

Timu ilicheza kwa uchovu mechi dhidi ya Mashujaa mjini Kigoma na haikuonekana kuamka katika mechi iliyofuata dhidi ya Singida Black Stars ama Ihefu.

Bado wachezaji kama Saido Ntibazonkiza, Mzamiru Yassin, Fabrice Ngoma na Clautus Chama ni tegemeo katika kikosi cha kwanza, lakini umri walionao wa kuanzia miaka 30, unaonekana kuwaathiri katika mechi zenye ushindani, nguvu na maarifa makubwa.

Kwa hiyo, ukiangalia yote hapo juu utaona mkanganyiko mkubwa kila sehemu na katika hali kama hiyo ni vigumu kuwa na timu imara katika mazingira ambayo yamejaa utata. Hakuna mtu halisi wa kubebeshwa lawama kama muhusika mkuu au ameshindwa kuwajibika ipasavyo katika nafasi yake.

Kocha haonekani kuwa katikati ya lawama, ingawa zimeanza baada ya timu kutopata ushindi katika mechi nne mfululizo, matokeo ambayo ni nadra sana kutokea ghafla kwa klabu kubwa kama hiyo iliyotolewa kwa mbinde robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Benchikha anaonekana hakupata wachezaji wazuri na alianzia safari katikati hivyo kutopata muda wa kutosha kujenga timu, hasa kwa wachezaji waliopo.

Si kocha Benchikha na benchi lake la ufundi, wala Try Again, wala Mangungu, wala Bodi ya Wakurugenzi na wala si mwekezaji aliyekubali kubeba lawama kutokana na hali iliyopo sasa wala ile ya kushindwa kwa mara ya tano kwenda nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kuendelea kuburuza mkia nyuma ya wapinzani wao, Yanga, katika Ligi Kuu wala kutolewa na Mashujaa katika Kombe la Shirikisho.

Katika mazingira hayo ni vigumu kuliona tatizo na kuazimia kujipanga upya. Kauli za kujipanga upya bila kuonyesha kosa lilikuwa wapi zitaendelea kuwa kama hizo za wiki iliyopita kuwa mwekezaji ameahidi kufanya kazi na uongozi ili Simba irudishe makali yake. Lakini tatizo halionekani liko wapi.

Ni muhimu kwa Simba kutafakari hali hii na kuibuka na taarifa inayoonyesha kulitambua tatizo na azma ya kulirekebisha ili timu ianze mradi mpya na wa muda mrefu, la sivyo itakuwa ni kujaribu ujanjaujanja ambao ni lazima wakati fulani unafika mwisho na ukweli kujiweka bayana.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: