Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba Queens yaendeleza ubabe kwa Yanga WPL

Simba Queens 3 1.jpeg Simba Queens yaendeleza ubabe kwa Yanga WPL

Thu, 4 Jan 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Simba Queens imeendeleza ubabe wake kwa watani wao wa jadi, Yanga Princess baada ya jana Januari 3 kuifumua mabao 3-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake (WPL), ikiwa ni wiki tatu tangu ilipoinyoosha pia kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii uliopigwa mapema Desemba mwaka jana.

Katika mechi hiyo ya Ngao ya Jamii, Yanga ilipoteza mchezo kwa pointi 5-4 baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu ndipo leo jioni zikavaana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam na Simba kupata ushindi huo ulioifanya ibakie nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo ikifikisha pointi tisa sawa na vinara JKT Queens, lakini ikizidiwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Simba imefunga mabao 13, wakati JKT ikiwa na 16 bila yenyewe nyavu zao kuguswa na ushindi wa jana mbele ya Yanga ulikuwa ni saba kati ya mechi 11 walizokutana tangu 2018, huku Yanga ikishinda mara moja tu na michezo mitatu iliisha kwa sare tofauti.

Katika mchezo wa jana uliokuwa mkali na wa kusisimua, Simba ndio iliyokuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa winga Asha Mnunka dakika ya pili tu tangu kipyenga cha kwanza kipulizwe akipokea krosi kutoka kwa Riticia Nabbosa.

Wakati Yanga ikijiuliza jinsi ya kulisawazisha bao hilo, ikajikuta ikipachikwa bao jingine la pili kupitia nyota huyo huyo dakika ya 10 kabla ya Yanga kupata bao la kufutia machozi lililowekwa kimiani katika dakika ya 14 kupitia Neema Paul aliyemalizia faulo iliyopigwa na Precious Christopher.

Mabao hayo yalidumu hadi wakati wa mapumziko, licha ya kuwepo kwa kosa kosa za hapa na pale kwenye milango ya timu zote mbili.

Kipindi cha pili Simba ilirejea kwa kasi na kuendelea kupeleka mashambulizi kwa Yanga na dakika ya 49 wakapata bao la tatu likifungwa na Vivian Corazone kwa kichwa akimalizia kona iliyopigwa na Riticia.

Kwa matokeo hayo yanamfanya Asha Mnunka akae kileleni mwa orodha ya wafungaji akifikisha mabao matano chini ya mwenzake Asha Djafar na Precious Christopher waliofunga mabao matatu.

Akizungumzia ushindi huo, Kocha Mkuu wa Simba,Juma Mgunda amewapongeza wachezaji wake kwa kujituma uwanjani na kupata pointi tatu ziazowafanya waendelee kupigania malengo waliyojiwekea msimu huu.

"Kila mechi ina kasi yake, Yanga walicheza vizuri lakini sisi pia tulipambana na kucheza kwa kujua tunapambania nini nawapongeza wachezaji tunajipanga na mechi ijayo," amesema Mgunda.

Kocha Mkuu wa Yanga Princess, Charles Haalubono amesema matokeo waliyopata kwenye mchezo wa jana umewapa somo na watakwenda kujipanga na mechi ijayo. "Timu ilijitahidi kupambana na kuna makosa madogo nimeyaona ambayo nitaenda kuyarekebisha kiwanjani naamini mechi hii ijayo tutafanya vizuri," amesema Haalubono.

Simba inajiandaa kukabiliana na JKT Queens kwenye mechi itakayopigwa Januari 09 Uwanja wa Isamuhyo, ikirejea fainali ya Ngao ya Jamii ambapo Simba ilishinda kwa penalti 5-4 na kubeba taji hilo mbele ya maafande hao ambao ni watetezi wa WPL.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: