Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba: Msiwe na wasiwasi, Tumejipanga

Simba Ndege Simba: Msiwe na wasiwasi, Tumejipanga

Thu, 30 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mratibu wa Simba, Abbas Ally amesema kitendo cha kubadilishiwa uwanja dhidi ya Jwaneng Galaxy Jumamosi walikishtukia kabla kwa hiyo hakitawatoa mchezoni. Awali walikuwa wacheze ule wa Taifa wa Botswana lakini sasa wamehamishiwa Obed Itani Chilume mjini Francistown ambako kuna umbali mrefu.

Alisema wao tayari walijipanga kukabiliana na changamoto zilizopo; “Suala la kubadilisha uwanja sisi tulishaanza kulipata toka awali hivyo tumejipanga kukabiliana na hilo, ingekuwa mchezo unachezwa nje ya mji wa Botswana tungesema mengine hivyo hatuwezi kutoka mchezoni kwa sababu ya aina hiyo.”

Lakini Kocha Mkuu wa Simba Mualgeria, Abdelhak Benchikha amesema kwa sasa jambo kubwa analofanyia kazi katika kikosi hicho ni kujenga wachezaji wa timu hiyo kisaikolojia kabla ya kucheza mchezo wa pili wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Jwaneng Galaxy.

Simba inashuka katika mchezo huo wa kundi ‘B’ ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1, dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast huku Jwaneng ikiingia kwenye mechi hiyo na morali baada ya kuishangaza Wydad Casablanca kwa kuichapa 1-0.

Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Benchikha alisema hakuna jambo kubwa atakalolifanya kwa huu muda mchache uliobaki ingawa atakachopambana nacho ni kuwajenga kisaikolojia wachezaji ili waweze kupata matokeo mazuri ugenini.

“Nafurahi kufanya kazi katika klabu hii kubwa hapa nchini na malengo yangu ni kuona inapiga hatua kama ambavyo nimefanya kule nilikotoka, kuhusu mpango wa mechi siwezi kuweka wazi bali nitaendelea na ripoti ya watangulizi waliopo,” alisema.

Aidha Benchikha aliongeza ili timu hiyo ipige hatua inahitaji ushirikiano mkubwa kuanzia kwa viongozi na wachezaji kwani hilo ndilo jambo kubwa litakalowafanya kufika katika malengo yao waliyojiwekea licha ya yeye kuingia katikati ya msimu.

Benchikha alitangazwa rasmi kukiongoza kikosi hicho Novemba 24, mwaka huu kwa mkataba wa miaka miwili akichukua nafasi ya Mbrazili, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyetimuliwa Novemba 7, baada ya kichapo cha mabao 5-1 dhidi ya Yanga.

Benchikha aliachana na klabu ya USM Alger ya kwao Algeria ambapo alitoka kuipa Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuifunga Yanga na CAF Super Cup mbele ya Al Ahly ya Misri iliyotwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: