Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Simba, Azam hii ni mechi haswa! Iko hivi

Simba Vs Azam Leo Simba, Azam hii ni mechi haswa! Iko hivi

Fri, 9 Feb 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Sahau kidogo matokeo ya jana usiku. Simba ipo Kirumba jioni hii dhidi ya Azam. Kwa mujibu wa wachambuzi, hii ndio mechi sasa.

Imebeba sura ya mbio za ubingwa wa timu zote mbili. Yeyote atakayepasuka anampa Yanga nafasi ya kupumua na kuzidi kupiga mluzi kileleni.

Ndio mechi ya Simba kuonyesha kwamba chini ya Abdelhak Benchikha si Azam wala Prince Dube anayeweza kuendeleza tambo za Mzizima. Hii ndio mechi sasa ya kuonyesha makali ya vifaa vipya baada ya kufungwa kwa dirisha dogo.

Ndio mechi ya Saido Ntibazonkiza kuwaziba midomo wanaomsema kwamba anashinda mabao ya penalti tu. Lakini ni mechi ya Feitoto kumuondoa Aziz Ki wa Yanga kileleni mwa wafungaji vinara.

Acha tuone dabi ya kwanza ya Mzizima kupigwa katika mechi za Ligi Kuu ikipigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba inakuwa na ladha gani. Ni saa 10:00 jioni.

Ni nadra sana, timu hizo kukutana kwenye mechi ya ligi na kucheza nje ya Dar es Salaam. Zimekutana mara 30 kwenye ligi tangu Oktoba 4, 2008, lakini ni mara moja tu mtanange baina yao umepigwa nje ya Dar es Salaam.

Ilikuwa Septemba 11, 2010 ambapo mwenyeji alikuwa Azam kikapigwa Mkwakwani, Tanga na hata hivyo ikalala kwa kuchapwa mabao 2-1 na Simba. Mechi nyingine zote zilipigwa Dar es Salaam kwenye viwanja vya Uhuru, Mkapa na Azam Complex lakini sasa Simba imeipeleka mechi hii CCM Kirumba Mwanza baada ya Uhuru na Mkapa kufungiwa kwa matengenezo.

MECHI YA UBINGWA

Simba mara ya mwisho kutwaa taji ilikuwa msimu wa 2020/2021 huku Azam ikilitwaa mara moja tu tena bila kupoteza mchezo msimu wa 2013/2014.

Yanga ndio imelitwaa taji hilo kwa misimu miwili iliyopita mfululizo pia imelitwaa mara nyingi zaidi (29), na msimu huu bado inalitaka lakini ushindani ni mkubwa kutoka kwa Simba na Azam na hadi sasa hakijaeleweka na mechi ya leo inaweza kumpunguza kasi mmoja na kumuongezea kasi mwingine baina ya Simba na Azam.

Ungechungulia msimamo wa ligi kabla ya mechi ya jana kati ya Yanga na Mashujaa, ungeona Yanga ikiwa kileleni na alama 34 baada ya mechi 13 sawa na Azam iliyo nafasi ya pili na pointi 31 huku Simba ikikusanya alama 29 katika mechi 12 ilizocheza.

Mchezo wa leo utakuwa wa 13 kwa Simba na 14 kwa Azam. Kama Simba itashinda mechi ya leo itafikisha pointi 33 na kuzidi kuiondoa Azam kwenye mbio za ubingwa, lakini ikishinda Azam itafikisha alama 34 na kuipa ugumu Simba kuwania ubingwa. Hii ndio mechi sasa.

NYAVU ZINATIKISWA

Mechi inayozikutanisha timu hizi mara nyingi nyavu hazilali njaa. Katika mechi 10 za ligi zilipokutana ni mchezo mmoja tu ulimalizika bila bao (0-0), mechi nyingine zote zimetoa mabao kwani yamefungwa jumla ya mabao 24 kwenye mechi hizo 10, ambapo Simba imefunga 14 na Azam imefunga 10 huku mechi iliyozalisha mabao mengi zaidi ikiwa ile ya Machi 4, 2020 ambapo Simba ilishinda 3-2 kwa mabao ya Erasto Nyoni, Deo Kanda na Meddie Kagere huku yale mawili ya Azam yakifungwa na Never Tigere na Shaban Chilunda. Wote hawapo kwenye timu hizo kwa sasa.

PATAMU HAPA

Leo Simba ndio ipo nyumbani huku Azam wakiwa wageni lakini namba za timu hizo zikicheza katika mazingira hayo zimeonekana kubalansi jambo linaloongeza ugumu kwenye mechi hii.

Msimu huu kwenye ligi Simba imecheza mechi sita nyumbani na Azam imecheza sita ambapo Simba imepoteza moja tu, ilipopigwa 5-1 na Yanga lakini imeshinda nne na kutoa sare moja sawa na Azam ambayo mechi za ugenini imecheza sita ikishinda nne, sare moja na kufungwa moja ilipochapwa 3-2 na Yanga.

Hata hivyo, timu hizo mbili kwenye mechi tano za ligi zilizopita zikicheza na timu tofauti kila kikosi kimefunga bao kwenye kila mchezo Azam ikiwa imepachika mabao mengi zaidi ikifunga 19 na kuruhusu mawili huku Simba ikifunga 11 na kuruhusu matatu. Hapa namba zinaibeba Azam.

Simba nayo inabebwa na rekodi ya mechi zilizopita timu hizo zilizopita hivi karibuni kwani katika michezo 10 imeshinda mara nne huku Azam ikishinda mara moja na kutoa sare mara tano.

VITA YA VIUNGO Licha ya kila timu kuwa na kikosi imara kwenye kila idara lakini mechi hii huenda ikaamuliwa na viungo kutokana na eneo hilo kuwa nguzo ya kila upande.

Babacar Sarr, Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin, Said Ntibanzokiza na Clatous Chama, ni wachezaji watano wa Simba wanaopata nafasi mara kwa mara kucheza eneo la kiungo na wamekuwa imara katika kujilinda na kutengeneza mabao ikiwemo kufunga.

Saido ana mabao matano, Kanoute ana mawili, Chama ana mawili, Ngoma moja yakiwa ni jumla ya mabao 10.

Kwa upande wa Azam eneo la kiungo wanacheza James Akaminko, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Sospeter Bajana, Kipre Junior na Djibril Sylla ambapo kwa ujumla wamezalisha zaidi ya mabao 15 kwani Sylla na Bajana kila mmoja amefunga mabao matatu, Kipre akifunga manne na Fei Toto akifunga manane jumla ikiwa 18. Hapo haujaweka asisti.

TAMBO SASA

Timu zote zinatamba kuibuka na ushindi kwenye mechi ya leo ambapo kocha msaidizi wa Simba Seleman Matola alisema watapanga wachezaji ambao wanaamini watashinda mechi ya leo.

“Tunajua ubora na ugumu wa Azam tunajipanga kuhakikisha tunapata pointi tatu safari ni ndefu tulilijua hilo na tumeweza kufanya wachezaji wote wako salama tunaamini tutakuwa tayari kwa mchezo na kufanya vizuri, mashabiki tunataka tuwahakikishie kwamba tutafanya kile kitu ambacho kila mwanasimba anakitarajia,” alisema Matola.

Kwa upande wa kocha wa Azam, Bruno Ferry alisema atawakosa nyota wake wanne, Sospeter Bajana, Andallah Heri, Malikou Ndoye na Allasane Diao lakini akisema wamejiandaa kushinda.

“Ni mchezo muhimu, tumejiandaa vizuri na tuko tayari kwa mchezo. Wapinzani wetu ni wazuri tunajua wana benchi zuri na wachezaji bora na tunafahamu ukiwa Simba una presha ya kushinda. Natumaini kesho mambo yatakwenda vizuri na mchezo utavutia,” alisema Ferry.

Manahodha wasaidizi, Mohamed Hussein wa Simba na Lusajo Mwaikenda wa Azam nao walizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzao.

“Timu msimu huu tulikuwa na malengo yetu, tutaingia na nguvu ile ile tunayotumia kwenye michezo mingine. Simba ni timu kama nyingine na sisi tuko tayari kucheza sehemu yoyote na tunaamini kwa ari tutakayoingia nayo itatusaidia kupata ushindi. Ninaamini mwalimu wetu ameandaa mbinu na mpango mzuri wa mechi na lengo letu sote itakuwa kupata alama tatu na hii itatusaidia kuona tunasimama wapi katika msimamo wa ligi,” alisema Mwaikenda.

“Kwetu wachezaji hakuna mwenye presha, maandalizi yameenda vizuri kabisa kuhakikisha tunapambania pointi tatu na kuzidi kupunguza pengo la pointi ambalo lipo, kwa hiyo kila mchezo ambao upo mbele yetu ni kama fainali,” alisema Hussein.

KIRUMBA IPO TAYARI

Meneja wa Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa, Lazaro Roman amesema kwa maboresho yaliyofanyika na yanayoendelea uwanjani hapo ana imani kwamba mchezo huo utachezwa katika mazingira bora na ya kuvutia.

Meneja huyo, alisema katika kuhakikisha uwanja unakuwa tayari, kukidhi vigezo na kuvutia, waliufunga kwa wiki mbili zilizopita na kusimamisha shughuli zote za kimichezo uwanjani hapo ili kurekebisha baadhi ya maeneo, ambapo walipanda nyasi sehemu zilizokuwa na vipara, kuweka mbolea na kupalilia pembezoni mwa uwanja.

“Sehemu korofi tulizopanda majani yameanza kuota na tuna wahudumu 10 wanaotusaidia kufanya usafi na mambo mengine hapa, kwa kinachofanyika tukija kufyeka kwa mara ya mwisho uwanja utapendeza na mashabiki watafurahi soka safi,” alisema.

Roman aliongeza, tayari Bodi ya Ligi (TPLB) na viongozi wa baadhi wa timu zinazohitaji kuutumia uwanja huo wameshakagua na kuridhishwa na kinachofanyika huku akisisitiza hadi kufikia siku ya mchezo dimba hilo litakuwa tayari kutoa burudani.

Mmoja wa wahudumu wa uwanja huo ambao Mwanaspoti liliwakuta wakisafisha kwa kupalilia nyasi, Halima Msindo, alisema wanaendelea kufanya usafi huku akiwahakikishia mashabiki wataburudika kwani wataukuta ukiwa katika mazingira safi.

Uwanja huo utaandaa mchezo huo muhimu ikiwa imepita miezi minne tangu mchezo wa mwisho wa ligi kuchezwa dimbani hapo Oktoba 7, mwaka jana ambapo Geita Gold iliikaribisha Yanga huku chama hilo la Wananchi likiibuka na ushindi mnono wa mabao 3-0.

CHUKUA HII

Unajua Simba na Azam ziliwahi kucheza mechi moja kwa siku mbili? Basi chukua hii! Machi 29, 2009 wababe hao walikutana katika mchezo wa ligi ambao ulichezwa kwa dakika 45 tu na kusimamishwa kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha. Wakati unasimama Simba ilikuwa ikiongoza kwa bao 1-0.

Mechi hiyo iliendelea kesho yake yaani Machi 30, 2009 na Simba kuendelea ilipoishia kwani ilipata mabao mengine mawili na dakika 90 za mchezo huo kumalizika Wanamsimbazi kushinda 3-0.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: