Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Shoo nne za moto Ligi ya Mabingwa

Simba Wydad Gd Mechi nne za moto Ligi ya Mabingwa

Fri, 21 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali inaanza wikiendi ijayo, ikiwa na sura tofauti na hatua ya makundi ambayo ilimalizika hivi karibuni. Hii ni hatua nyingine muhimu ambayo mashabiki wamekuwa wakiisubiri kwa hamu kubwa, kutokana na upinzani wa kila timu ambayo imeingia hapa.

Kwa hapa Tanzania, nchi itawakilishwa na Simba, wakati kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakilishi itakuwa Yanga ambayo imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali.

Katika michezo yote ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hakuna hata mmoja ambao unaonekana kuwa mwepesi kwa upande mmoja kutokana na ubora wa timu zote ambazo zimefanikiwa kutinga kwenye hatua hiyo.

Ni timu mbili tu ambazo zimetinga kwenye hatua hii zina rekodi ya kutotwaa ubingwa huu, Simba ambao walifika nusu fainali mwaka 1972, pamoja na CR Belouzdad ambaye ndiye mchanga zaidi kwenye michuano hii ikiwa iliondolewa kwenye hatua ya kwanza msimu uliopita.

Timu nyingine zina hazina kubwa ya makombe na kwa ujumla timu zote zimeshatwaa makombe 23, zikiongozwa na Al Ahly ambayo imetwaa ubingwa huu mara 10 ikifuatiwa na Esperance de Tunis ambao wameshaunyakua mara nne.

Wikiendi hii itakuwa ya kibingwa zaidi ambao kila mchezo una rekodi zake, hakuna ambao unaonekana kuwa utakuwa mwepesi kutokana na ubora wa timu zote nane.

Timu nne zitafanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ambapo kila timu itafanikiwa kujinyakulia kitita cha dola 875,000, zaidi ya shilingi bilioni 2, ambayo ni bajeti ya timu nyingi za Afrika kwa sasa.

AL AHLY VS RAJA CASABLANCA Huu umebatizwa kuwa mchezo wa wababe, ambao utapigwa Aprili 22, saa nne kamili usiku kwenye Uwanja wa Cairo, ukiwa unatajwa kuwa mchezo wenye msisimko mkubwa zaidi kuliko mingine ya hatua hii.

Raja na Al Ahly zote zina historia kuwa kwenye michuano hii lakini zikiwa na kundi kubwa la mashabiki lakini hapa ndiyo unakutana na timu yenye thamani kubwa zaidi, Al Ahly, ambayo thamani yake kwa mujibu wa mtandao maarufu wa Transfer Market ni bilioni 74.7, wakiwa wanakutana na Raja ambao thamani yao ni bilioni 38.6.

Takwinu zinaonyesha kuwa huu ndiyo mchezo ambao unazungumzwa zaidi kwenye mitandao tangu hatua hii ilipopangwa.

Timu hizo zimefanikiwa kukutana mara tatu kwenye michuano hii na jambo la ajabu ni kwamba Raja hawajapata ushindi hata mara moja, huku Al Ahly wakishinda mara moja na kutoka sare mara mbili.

Katika michezo ya msimu huu, Al Ahly wakiwa nyumbani kwao wamefanikiwa kushinda michezo mitatu, huku Raja wakiwa na rekodi ya kushinda michezo mitatu ugenini kwenye hatua ya makundi mmoja ukiwa ni ule walioichapa Simba mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Mkapa.

Ahly watatakiwa kuwa makini na mshambuliaji wa Raja Hamza Khaba ambaye ndiye anaongoza kwa mabao akiwa kinara kwa sasa baada ya kufunga mabao matano kwenye michuano hii msimu huu.

Lakini kwa Raja wao watatakiwa kuwa makini na straika wa Al Ahly Mohammed Manem akiwa tayari ameshafunga mabao manne kwenye michuano hii, huu unatazamwa kama mchezo ambao unaweza kutoa timu itakayotinga fainali msimu huu.

JS KABILE VS ES TUNIS Huu ni mchezo mwingine ambao utakutanisha timu mbili zenye upinzani mkubwa Afrika katika mchezo mkali utakaopigwa kwenye Uwanja wa Novembre 1954, nchini Algeria.

Hizi ni timu mbili ambazo zina rekodi tofauti, Kablie wenyewe wana rekodi ya kuchukua ubingwa huu mara mbili wakiwa waliutwaa mara ya mwisho mwaka 1996, lakini watavaana na wababe wa Tunisia, Esperance au Es Tunis ambao rekodi zao zinaonyesha wametwaa ubingwa mara nne, mara ya mwisho waliuchukua mwaka 2019.

Takwimu zinaonyesha kuwa Kablie ni timu hatari inapokuwa kwenye uwanja wa nyumbani, ikiwa imeshinda michezo mitano ya kimataifa hivi karibuni, lakini bado siyo kigezo cha kuwatisha Tunis ambao wameshinda mchezo mmoja ugenini kwenye hatua ya makundi.

Katika michezo nane ambayo wamekutana, Tunis wamefanikiwa kushinda minne, wametoka sare miwili na kupoteza miwili jambo ambalo linaendelea kuzua joto kubwa kwenye mchezo huu utakaopigwa Ijumaa, saa nne usiku.

Kablie siyo timu tajiri sana kama zilivyo nyingine za nchi za Kiarabu, kikosi chao kina thamani ya bilioni 7.5 ambapo watakuwa wakivaana na wabishi Esperance wenye thamani ya bilioni 19.8 zaidi ya mara mbili yao.

BELOUIZDAD VS MAMELODI Timu nyingi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika zilikuwa zinakwepa kuvaana na Mamelodi kutokana na ubora wao msimu huu, lakini wakajikuta wameanguka kwenye timu isiyo na mafanikio kabisa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Belouizdad.

Timu hii ndiyo ambayo haina rekodi kubwa kwenye hatua hii ikiwa na kumbukumbu ya kutolewa kwenye hatua ya kwanza mwaka 2022. Rekodi inaonyesha kuwa timu hizo zimekutana mara mbili na kila moja imeshinda mchezo mmoja jambo ambalo linaendelea kuwasha moto mkali kwenye mchezo huu.

Mamelodi ambao walikuwa timu ya mwanzoni kabisa kufuzu kwa hatua hii ni kati ya zile ambazo zinapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu, lakini haitashangaza kama mambo yatakuwa tofauti kuanzia kwenye mchezo wa kwanza utakaopigwa Uwanja wa Nelson Mandela nchini Algeria, Jumamosi saa 4 usiku.

Ni kama vile wakubwa wawili wanakutana, ambapo kwa thamani ya kikosi cha Mamelodi ni bilioni 69.5 ikiwa ni tofauti na Belouzidad ambao thamani ya kikosi ni bilioni 33.4, ikiwa imezidiwa mara mbili na Mamelodi ambao wanamtengemea mshambuliaji wao hatari Peter Shalilule huku Belouzidad wakiwa wanamtegemea zaidi staa wao Aribi.

Belouzidad pamoja na kutokuwa na heshima kubwa huku, msimu huu wamekuwa hatari zaidi wakiwa wameshinda michezo minne nyumbani kwenye michuano hii, lakini watakuwa na wakati mgumu kwa kuwa watakutana na Mamelodi ambao wameshinda michezo miwili ya ugenini katika hatua ya makundi.

SIMBA VS WYDAD CASABLANCA Huu ni mchezo mwingine ambao unaonekana kuwa hauna mzani sawa, lakini dakika tisini zinaweza kuwashangaza mashabiki wa soka wa bara la Afrika.

Simba ambayo kwa miaka minne imefanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa ikiwa imefika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara tatu na mara moja kwenye Kombe la Shirikisho imekuwa ikiutumia vyema uwanja wake wa nyumbani Kwa Mkapa sehemu ambayo imezichapa timu kadhaa kubwa, ikiwemo Al Ahly ya Misri.

Mchezo wa kwanza unaonekana kuwa ndiyo wenye dira ya Simba kwenye michuano hii kwani endapo itapata ushindi mkubwa nyumbani basi itakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kufuzu kwenda hatua inayofuata.

Ratiba inaonyesha kuwa mchezo huu unatarajiwa kupigwa saa 10 kamili jioni muda ambao unaonekana kuwa rafiki zaidi kwa Simba kwenye mchezo huu. Bado Wydad wanaweza kuwa na hofu na Simba kutokana na kiwango ambacho wamekionyesha kwenye michezo ya mwishoni ya hatua ya makundi ikiwa ni pamoja na kuwachapa Horoya mabao 7-0 na ushindi kwenye michezo miwili dhidi ya Vipers.

Simba ambao thamani ya kikosi chao ni ya chini kuliko timu zote kwenye hatua hii ya bilioni 5.5 inamtegemea zaidi kiungo wake Clatous Chama ambaye ameshafunga mabao manne kwenye hatua ya makundi na ndiye anayetupiwa jicho kali na Wydad ambao wameshatwaa ubingwa huu mara tatu na ndiyo mabingwa watetezi, thamani ya kikosi chao ikiwa ni bilioni 48.9.

Timu hii pamoja na mambo mengine inamtegemea zaidi Junior Sambou ambaye ameonyesha uwezo mkubwa kwenye hatua ya makundi jambo la msingi tusubiri tuone itakavyokuwa.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: