Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Saido na mabao 24 Simba

Saido 38834065 Saido Ntibanzokiza

Wed, 19 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Simba imeachana na kiungo mshambuliaji wake tegemeo, Saido Ntibazonkiza, baada ya kuhudumu kwa msimu mmoja na nusu, akipachika jumla ya mabao 24 katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Taarifa iliyotolewa jana na uongozi wa kabu hiyo, imeeleza haitaendelea tena na raia huyo wa Burundi, aliyesajiliwa kipindi cha dirisha dogo la uhamisho msimu wa 2022/23, akitokea Geita Gold.

"Uongozi wa klabu unawatangazia kuwa hatutaendelea kuwa na mchezaji Saido, baada ya mkataba wake kumalizika," ilisema taarifa hiyo.

Mchezaji huyo anaondoka Simba akiwa amefunga jumla ya mabao 24 katika misimu miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara, mabao 13 msimu wa 2022/23, na msimu uliomalizika akifunga 11.

Alimaliza akiwa kinara wa ufungaji msimu wa 2022/23, akiwa na mabao 17, sawa na straika Fiston Mayele wa Yanga, manne akitoka nayo Geita Gold na kuwa mchezaji aliyeongoza kuwa na mabao mengi katika kikosi hicho.

Msimu uliomalizika pia aliweka rekodi hiyo, kwani mabao 11 aliyopachika yalikuwa ni mengi zaidi ya mchezaji yeyote wa timu hiyo, akifuatiwa na Jean Baleke ambaye aliachwa kipindi cha dirisha dogo akiwa ameshapachika mabao manane.

Kabla ya kwenda Geita Gold, Saido, ambaye pia ni mchezaji wa Timu ya Taifa ya Burundi, aliichezea Yanga kuanzia 2020 hadi 2022.

Wakati Simba ikiachana na Saido, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amewatoa wasiwasi wanachama na mashabiki wa Simba kuhusu suala ya kocha.

Alisema suala hilo lipo chini ya kamati maalum kwa ajili ya kufanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kuchujwa kwa majina, ili kumpata mwenye kiwango kizuri anayeendana na falsafa ya Simba na mazingira pia.

"Niwaambie tu wanachama na mashabiki wa Simba kila kitu kiko vizuri, kuanzia usajili hadi eneo la benchi la ufundi, nadhani hata mwekezaji wetu, Mohamed Dewji alilieleza hilo, msimu uliopita tulibezwa sana na kupewa kila aina ya manyanyaso na masimango hali iliyomtoa Ughaibuni mwekezaji wetu kuja kushika kijiti cha usajili kwa kuhakikisha hatufanyi makosa tena," alisema Ahmed.

Taarifa zinaeleza kuwa mkononi yalibaki majina ya makocha wanne ambayo ni Florent Ibenge raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo anayeifundisha Al Hilal ya Sudan, Mreno, Alexandre Santos anayemaliza mkataba wake na Klabu ya Petro de Luanda ya Angola, Omar Najhi, raia wa Uingereza mwenye asili ya Morocco, pamoja na anayetajwa kuwa na asilimia kubwa ya kupewa mikoba ya kukinoa kikosi hicho, Steve Komphela raia wa Afrika Kusini, anayeifundisha Klabu ya Lamontville Golden Arrows ya Sauzi.

Wakati akitangaza wajumbe wapya wa Bodi ya Wakurugenzi upande wake, Mo, alitaja sababu mbalimbali zilizoikwamisha Simba kufanya vema, ikiwamo kutokuwa na benchi zuri la ufundi akiahidi kulifanyia kazi.

"Tumeshindwa kutegeneza timu bora ya ushindani, eneo la benchi la ufundi halikuwa zuri, hii imesababisha hata kupoteza falsafa yetu ya pira-biriani, hili ni eneo muhimu la kufanyia kazi, naahidi tutashirikiana na wenzangu kusuka upya eneo hilo," alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: