Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Robertinho tutaivaa Wydad kivingine kwao

Robertinho Mipango Robertinho tutaivaa Wydad kivingine kwao

Mon, 24 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya ushindi hafifu wa bao 1-0 dhidi ya Wydad Casablanca kwenye mechi ya robo fainali ya mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha Mkuu wa Simba, Robertinho Oliveira, amesema kazi bado haijamalizika na wataenda na sura mpya katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Jumamosi nchini Morocco.

Simba inatarajia kucheza mchezo wa marudiano Aprili 28, mwaka huu, nchini Morocco katika Uwanja wa Mohammed V, kusaka ushindi ama sare yoyote ili kutinga nusu fainali.

Akizungumza nasi hili baada ya kukamilika kwa dakika 90 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa juzi, Robertinho alisema anashukuru na kuwapongeza wachezaji wake kwa kupata matokeo mazuri japo ni ushindi mwembamba.

Alisema hii ni Ligi ya Mabingwa na walikuwa wanacheza na bingwa wa Morocco na mtetezi wa michuano hiyo ya Afrika, hivyo haikuwa kazi nyepesi kuwafunga Wydad.

"Watu wanatakiwa kuipongeza Simba kwa ushindi huu, imeonesha dunia nzima kila mpinzani anatakiwa atuheshimu, tumeonesha tuna ubora mzuri ndani ya uwanja," alisema Robertinho.

Aliongeza kuwa sasa wanarejea katika uwanja wa mazoezi kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mechi hiyo kwa ajili ya kujiandaa na kibarua kingine cha mchezo wa marudiano.

Robertinho alisema anatambua itakuwa mechi ngumu na ushindani mkubwa kwa kuwa Wydad watahitaji kutumia vizuri uwanja wao kama ilivyo kwa Simba ikiwa Benjamin Mkapa.

"Haitakuwa mechi rahisi na tutalazimika kucheza kwa mbinu tofauti na mechi ya leo [juzi], na wachezaji kuingia kivingine katika mchezo wa marudiano tofauti na tulivyocheza ili kufikia malengo yetu ya kusonga mbele kucheza nusu fainali," alisema Robertinho.

Alisema kuwa anaimani kubwa na wachezaji aliokuwa nao ndani ya kikosi kwa kufanikisha malengo yao akiwamo Mohammed Hussein [Tshabalala] Saido [Ntibazonkiza], Kapombe [Shomari], Baleke [Jean] na Mzamiru [Yassin] na wengineo.

Nahodha Msaidizi wa Simba, Tshabalala, alisema licha ya kupata ushindi bado wanahitaji kwenda nchini Morocco kwa silaha nyingine ili kumaliza dakika 90 za kumalizia mchezo.

Alisema dakika 90 za kwanza zilikuwa ngumu sana kucheza na Mabingwa wa Afrika pia bingwa wa Ligi ya Morocco, lakini wamepambana na kupata matokeo mazuri.

"Tunaenda na mipango mingine tofauti na tulivyocheza hapa nyumbani ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri, lazima tutapambana, tunatambua mechi itakuwa ya ushindani mkubwa," alisema Tshabalala.

Rais wa Heshima na Mwekezaji wa Simba, Mohammed 'Mo' Dewji, amewataka wachezaji kwenda kupambana katika mchezo wa marudiano dhidi ya Wydad Casablanca.

“Tunafurahi kwa ushindi huu, lakini bado, tuna kazi kubwa na mlima mrefu wa kuupanda Aprili 28, mwaka huu, nchini Morocco ili tumfunge Wydad nyumbani kwake na kusonga mbele lazima tukapambane kiume ugenini,” alisema Mo Dewji.

Alisema anaimani kubwa na Simba kufikia rekodi hiyo ya mwaka 2003 kwa sababu ya kuwa na kikosi imara na wachezaji kumhakikishia kupata matokeo mazuri katika dakika 90 zijazo.

Kocha wa Wydad Casablanca, Juan Carlos, alisema hawakuwa na mchezo mzuri kwa sababu hali ya hewa haikuwa rafiki na Simba kutumia madhaifu kwa nafasi waliyotengeneza.

Alisema mechi ilikuwa na ushindani mkubwa na Simba wametumia vizuri uwanja wa nyumbani kupata matokeo mazuri na wao wameshindwa kutumia nafasi walizotengeneza.

"Kusema ukweli hatukuwa na mchezo mzuri leo [juzi] sababu kubwa ni mvua, uwanja haukuwa rafiki na mliona jinsi gani wachezaji walikuwa wakiteleza sana uwanjani.

"Tumemaliza dakika 90 za Dar es Salaam, tunawakaribisha Simba katika mchezo mwingine nyumbani kwetu Morocco, lazima tupambane tushinde mchezo huo kwa sababu malengo yetu ni kucheza nusu na fainali, ninawapongeza Simba kwa ushindi walioupata," alisema Carlos.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: