Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Robertinho ataka mshambuliaji mwingine na mbadala wa Chama

Robertinho X Bocco Robertinho ataka mshambuliaji mwingine na mbadala wa Chama

Fri, 5 May 2023 Chanzo: Nipashe

Wakati timu yake ikilazimishwa sare ya bao 1-1 na Namungo FC katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyochezwa juzi, Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira 'Robertinho' amesema anahitaji nyota wapya kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Super League inayotarajiwa kufanyika Agosti, mwaka huu.

Robertinho amesema hayo muda mchache baada ya kumalizika kwa mechi hiyo ya ligi alipokutana na mabosi wa Simba katika kikao cha tathmini.

Akizungumza nasi jana, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema katika kikao hicho kilichohusisha wajumbe wa bodi waliokuwa mkoani Lindi, Robertinho aliweka wazi anahitaji beki, viungo wawili (mshambuliaji na kiungo mkabaji) pamoja na mshambuliaji ambaye ana ubora zaidi ya Jean Baleke.

Ahmed alisema tayari kocha huyo  ameshafanya maboresho ndani ya kikosi cha Simba ambacho kimekuwa na mwendelezo mzuri na anataka kuitengeneza timu hiyo ili iwe tishio kwa ndani na nje ya nchi.

"Baada ya mchezo wa marudiano dhidi ya Wydad Casablanca, Kocha Robertinho alifanya kikao na viongozi wa bodi tukiwa hotelini Morocco, kikubwa ni kutoa tathmini ya timu kufuatia ushiriki wa Ligi ya Mabingwa Afrika, na katika kikao hicho ametoa mapendekezo ya usajili wa wachezaji wapya,” alisema Ahmed.

Meneja huyo alisema anaamini wachezaji walioko wana ubora na kinachohitajika ni maboresho ambayo kazi yake imeshaanza kufanyika.

“Kocha amesema anapata changamoto kwa sasa kwa sababu ya mshambuliaji mmoja (Jean Beleke), aliyekuwa naye, lakini pia anataka mbadala wa Chama (Clatous), lengo ni kutengeneza kikosi bora na tishio katika ukanda huu wa Afrika na zaidi kufika hatua ya nusu fainali hadi fainali katika michuano ya kimataifa,” Ahmed alisema.

Robertinho aliliambia gazeti hili matokeo hayo yamewapunguzia presha wapinzani wao wakubwa, Yanga ambao wako katika mbio za kuwania ubingwa.

"Wachezaji walijitahidi kupambana, makosa madogo yalitugharimu lakini sasa tunaangalia mbele kwenye michezo ya ligi iliyobakia na Kombe la FA," alisema Robertinho.

Aliongeza alilazimika kupumzisha baadhi ya nyota wake wa kikosi cha kwanza kutokana na kukabiliwa na mchezo muhimu wa hatua ya nusu fainali ya FA dhidi ya Azam itakayochezwa Jumapili.

Naye Kocha Msaidizi wa Simba, Juma Mgunda, aliliambia gazeti hili baada ya kushindwa kuvuna pointi zote tatu katika mechi hiyo iliyopita, bado malengo yao ni kupambana na kushinda michezo iliyosalia.

Mgunda alisema bila kujali matokeo ya timu nyingine, wao watahakikisha wanapambana kusaka alama tatu ili kumaliza vizuri msimu huu wa ligi.

"Mchezo dhidi ya Namungo umemalizika, tumepata sare, tunarudi kwenye uwanja wa mazoezi kujiandaa na mechi zilizosalia,  hatuangalii nani kafanya nini, tunahitaji kushinda mechi zetu zote.

Tulijua isingekuwa mechi rahisi, Namungo ni timu nzuri hasa inapokuwa nyumbani, lakini mpira una matokeo matatu, tunarudi kujipanga kwa mechi zilizopo mbele yetu,"  Mgunda alisema.

Katika mchezo huo Simba iliwakosa Chama, Enock Inonga, Mzamiru Yassin, Saido Kanoute, Shomari Kapombe na Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr'.

Chanzo: Nipashe
Related Articles: