Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Robertinho ashtukia ishu Simba

Robertinho 5.jpeg Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’

Thu, 12 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Leo ni siku ya pili kwa Simba kupiga tizi la kimkakati kambini Bunju, Dar es Salaam ikijiandaa na mechi dhidi ya Al Ahly ya Misri kwenye michuano mipya ya African Football League itakayozinduliwa Oktoba 20, mwaka huu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na fasta benchi la ufundi la wana Msimbazi limeshtukia kitu.

Simba ni miongoni mwa timu nane zitakazoshiriki michuano hiyo mipya kwa Afrika wakati nyingine zikiwa ni Alhy, TP Mazembe, Esperance, Enyimba, Wydad AC, Petro Atletico na Mamelodi Sundowns.

Wakati kila moja ikijiandaa kuonyesha ushindani kwenye michuano hiyo, Simba haitacheza mchezo wowote wa mashindano kwa siku tisa zijazo, jambo ambalo benchi la ufundi chini ya kocha mkuu Roberto Oliveira ‘Robertinho’ limeshtuka kuwa kama mtego kwao na tayari wamepata mpango mwingine.

Robertinho aliliambia Mwanaspoti kwamba, licha ya kwamba kwa kuhesabu siku tisa zinaonekana ni nyingi, lakini kwenye soka ni chache zinazopaswa kutumika ipasavyo hivyo ameomba mechi mbili za kirafiki.

Kocha huyo ambaye chama lake linaongoza Ligi Kuu na alama 15 baada ya mechi tano, alisema kukaa siku tisa bila kujipima ni changamoto kwa wachezaji na ndiyo sababu ameomba mechi za kirafiki.

“Ni muda mwingi lakini pia ni mfupi. Kwa bahati nzuri Simba tuna timu bora yenye mwendelezo, tunataka kujiimarisha zaidi katika kipindi hiki ili tupate matokeo chanya dhidi ya Al Ahly ambao ni bora pia.

“Tunapanga kucheza mechi mbili au moja za kirafiki kabla ya Ahly, lengo ni kufanya uchambuzi wa kikosi na kujua tunachotarajia kufanya kimekamilika kwa kiasi gani na baada ya hapo tutajua tunaingiaje dhidi ya Ahly mchezo ambao utakuwa na ushindani mkubwa lakini lengo ni kushinda,” alisema Robertinho.

Ikumbukwe michuano hiyo itachezeka kwa mtoano - nyumbani na ugenini ambapo baada ya mechi ya Oktoba 20, pale kwa Mkapa, Simba itakutana na Ahly tena Oktoba 24, Cairo, Misri na mshindi wa jumla ataingia robo fainali.

Nusu fainali mbili za michuano hiyo zitapigwa kati ya Oktoba 29 na Novemba 1, kisha fainali nayo itapigwa mara mbili (nyumbani na ugenini), Novemba 5 na 11. Simba tangu kuanza kwa msimu huu imecheza mechi tisa za mashindano ikiwa haijapoteza mechi yoyote ikishinda saba na kutoka sare mbili.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: