Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Robertinho ajifungia na Kramo dakika 30

Aubin Kramo Training Robertinho ajifungia na Kramo dakika 30

Sat, 2 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba SC inaendelea na mazoezi ya kujiandaa na mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu dhidi ya Power Dynamos, lakini kuna kikao ambacho kocha wa, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amekifanya na winga mmoja aliyesajiliwa kutoka ASEC Mimosas ya Ivory Coast.

Katika kikosi hicho, Robertinho alitumia muda wa zaidi ya nusu saa kumjaza upepo winga huyo Aubin Kramo aliyerejea kutoka katika majeraha na kushindwa kuanza kwa kasi ndani ya kikosi hicho, ili kumtaka kuliamsha kama alivyokuwa kabla ya kusajiliwa mwezi uliopita.

Robertinho amesema, amefanya kikao kifupi na Kramo akimuandaa kuhakikisha anarejea na akili mpya ya kuanza kazi ya kuitumikia Simba.

Kocha huyo alisema amemtaka Kramo kujipanga kuanzia kwenye mazoezi, kwani anamtaka haraka kupigania nafasi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

“Nina furaha sana ya kurejea kwa Aubin (Kramo), sikiliza huyu ni mchezaji mmoja kati ya wachezaji ambao tuliwaongeza hapa wakiwa na ufanisi bora huko walikotoka hasa mashindano haya ya CAF,” alisema Robertinho.

“Nimekutana naye nimemwambia kwamba bado hajachelewa, huu ni wakati wake kuanza kwa nguvu akijituma kwenye mazoezi haya tunayofanya tutampa nafasi hata kwenye hizi mechi za kirafiki ambazo tutacheza hivi karibuni,” alisema kocha huyo aliyeiongoza Simba katika mechi 13 za Ligi Kuu bila kupoteza tangu atue akitokea Vipers ya Uganda, ikiwamo kuitungua Yanga kwa mabao 2-0 na kuivua Ngao ya Jamii kwa penalti 3-1 kupitia fainali iliyopigwa Agosti 13, jijini Tanga.

“Nahitaji kumuona anakuwa tayari kabla ya mechi yetu ya kwanza, kumbuka huyu ni mchezaji ambaye alifanya vizuri mashindano ya Afrika msimu uliopita, ndio maana Simba ikamleta hapa, akiwa tayari kuanza kucheza timu itaongeza kitu kikubwa.

Msimu uliopita ambao Kramo aliitumikia ASEC Mimosas ya Ivory Coast Kramo alifanikiwa kufunga mabao manne timu yake ikiishia hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Robertinho aliongeza sio Kramo peke yake pia amewataka wachezaji wengine ambao wamesajiliwa msimu huu ambao hawajapata nafasi ya kucheza kwenye mechi mbili zilizopita kuamka haraka na kuanza kupigania nafasi ya kikosi cha kwanza.

“Hii sio kwa Aubin (Kramo) peke yake tuna wachezaji wengine ambao tumewasajili na bado hawajaweza kupata nafasi kwenye mechi za hivi karibuni Shaaban Idd  (Chilunda), Hamis (Abdallah), David (Kameta) na wengine wanatakiwa kujituma sasa wakati huu ili tuongeze ushindani, wako hapa kwa ajili ya kushindana aliye bora atapata nafasi,” alisema Robertinho na kuongeza;

“Nataka kuwa na mchezaji mshindani ambaye hatakiwi kukata tamaa, timu bora ni ile ambayo wachezaji wao watakuwa wanashindania nafasi hizi mechi tutakazocheza zitawasaidia sasa kupandisha ubora wao.”

Simba itacheza mchezo wa kwanza wa kirafiki Jumamosi Mo Simba Arena Bunju na timu kutoka Zanzibar kabla ya nyingine ili kuwaweka fiti nyota wa timu hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: