Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Robertinho aendeleza makali Ligi Kuu

Robertinho Simba G Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’

Tue, 22 Aug 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, umemfanya kocha Roberto Oliveira 'Robertinho' kufikisha idadi ya michezo 13 mfululizo ya Ligi Kuu bila kupoteza huku akiweka rekodi ya timu yake kufunga bao katika mechi hizo zote ambazo yeye alikuwa kwenye benchi la ufundi.

Katika michezo hiyo 13 ambayo Robertinho ameiongoza Simba katika Ligi Kuu tangu alipojiunga nayo Januari mwaka huu, timu hiyo imepata ushindi mara 11 na imetoka sare mbili tu.

Safu ya ushambuliaji ya Simba imeonekana kutomuangusha Robertinho kwani haijawahi kutoka kapa tangu timu hiyo ilipoanza kunolewa na Mbrazil huyo.

Simba chini ya Robertinho, imefunga mabao 32 ikiwa ni wastani wa mabao 2.5 kwa kila mchezo na imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa tu ikiwa ni wastani wa bao 0.7 kwa mechi.

Robertinho alianza kwa ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mbeya City, akaja kuichapa Dodoma Jiji kwa bao 1-0, kisha akaibuka na ushindi wa mabao 3-1 mbele ya Singida Big Stars na mchezo uliofuata akalazimishwa sare ya bao 1-1 na Azam FC.

Baada ya hapo, Simba ikaibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, ikapata ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Ihefu na kuwafunga watani zao Yanga kwa mabao 2-0 na ikalazimishwa sare ya bao 1-1 na Namungo FC.

Timu iliyofuata kuonja makali ya Robertinho ilikuwa ni Ruvu Shooting iliyochapwa mabao 3-0, kisha Polisi Tanzania ikafungwa mabao 6-1 ikifuatiwa na Coastal Union iliyochapwa mabao 3-1 na msimu huu ikaanza kwa kuifunga Mtibwa Sugar mabao 4-2 na jana ikaifunga Dodoma Jiji kwa mabao 2-0.

Robertinho alisema kuwa siri ya mafanikio ya timu yake kwenye ligi ni staili yake ya kucheza soka la kushambulia.

"Siku zote natamani kuona tukishambulia na kucheza katika nusu ya mpinzani mara kwa mara ili kutengeneza nafasi na kufunga mabao," alisema Robertinho.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: