Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Robertinho, Minziro wachimbana mikwara Mbeya

Robertinho  Instagram Robertinho, Minziro wachimbana mikwara Mbeya

Thu, 5 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Simba SC na Tanzania Prisons kesho zinatarajiwa kuvaana kwenye pambano la kwanza msimu huu la Ligi Kuu Bara, huku makocha wa timu hizo, Roberto Oliveira 'Robertinho' na Fred Felix 'Minziro' wakipigana mikwara kila mmoja akitamba ni lazima waibuke na ushindi kwenye pambano hilo litakalopigwa Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa litapigwa kuanzia saa 10:00 jioni, huku Robertinho akisisitiza anaamini timu yake inao uwezo na kiwango bora kuendelea kufanya vizuri, akiwataka mashabiki wasubiri kesho kuona watakapowakabili maafande hao wa Tanzania Prisons.

Hata hivyo, Minziro amesema licha ya ukubwa wa jina la Simba, kesho Alhamisi watakutana na sapraizi ya aina yake kwa vile wamejiandaa kutoka na ushindi ili kunyakua pointi tatu za kwanza msimu huu, lakini pia kulipa kisasi cha mechi za msimu uliopita ilipopoteza nyumbani 1-0 na kulala ugenini mabao 7-1.

Mechi hizo zote Simba ilipata ushindi ikiwa chini ya kocha Juma Mgunda ambaye baadaye alikuja kumuachia kiti Robertinho. Huu ni mchezo wa kwanza kwa Mbrazili huyo kuikabili Prisons kwenye mechi za Ligi Kuu Bara, akibebwa na rekodi ya kutopoteza mechi yoyote kati ya 14 alizoziongoza tangu ajiunge na Simba.

Akizungumza pambano hilo, Robertinho amesema licha ya mashabiki kulalamika, kikosi chake kina uwezo wa kupata matokeo uwanja wowote na hilo litathibitishwa kesho Sokoine.

Kocha huyo amesema Simba inacheza kwa mbinu kutokana na aina ya mchezo wanaokutana nao. Akizungumzia wanaotilia shaka kiwango kufuatia mchezo uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos, Robertinho anasisitiza wao walihitaji kufuzu makundi, jambo ambalo walifanikiwa.

Kauli ya kocha huyo Mbrazil inakuja wakati baadhi ya mashabiki wa Simba wakieleza kutofurahishwa na kiwango cha timu hiyo ambayo ilifuzu hatua ya makundi 'ikibebwa' na kanuni kwa matokeo ya jumla ya mabao 3-3, ikinufaika kwa wastani wa mabao mawili ya ugenini.

Wekundu hao katika mechi ya kwanza dhidi ya Dynamos waliyocheza ugenini walimaliza kwa sare ya 2-2 huku mchezo wa marudio katika uwanja wa Chamazi Dar es Salaam ukiisha kwa 1-1 na kuwaondoa wapinzani wao kutoka Zambia.

Robertinho amesema timu hiyo ina uwezo na kiwango na kwamba malengo yao ilikuwa ni kutinga makundi klabu bingwa, hivyo anaamini kesho atawapa raha mashabiki.

Amesema anafahamu mechi dhidi ya Prisons itakuwa ngumu, lakini kwa maandalizi waliyofanya watashinda, akibainisha kuwa kesho mashabiki watafurahi kwa soka litakalopigwa.

"Naamini watafurahi kesho kutokana na maandalizi tuliyofanya, tunafahamu mechi itakuwa ngumu dhidi ya wapinzani lakini tumejipanga, mechi iliyopita ilikuwa ya mbinu kufuzu makundi klabu bingwa na tulifanikiwa" amesema kocha huyo.

Kipa wa timu hiyo, Hussein Abel aliyewahi kuidakia Prisons kabla ya kutua KMC na baaade Simba kupitia dirisha la usajili lililofungwa Agosti 31, amesema wachezaji wamejipanga kuwapa raha mashabiki, akikiri timu hizo huwa na upinzani mkali zinapokutana.

"Sisi tunaahidi furaha kwa mashabiki. Matarajio yangu nikipata nafasi nitafanya vizuri, tunajua mechi siyo rahisi lakini muhimu ni pointi tatu," amesema kipa huyo aliyewahi kuichezea pia Coastal Union.

Minziro, nyota wa zamani wa Polisi Zanzibar na Yanga, amesema pamoja na ukubwa wa Simba, lakini iwapo nyota wake watafuata maelekezo, Prisons inaenda kumaliza kazi mapema kwa kubaki na pointi tatu, huku akisisitiza nidhamu uwanjani.

Amesema kwa mechi tatu walizocheza, Prisons haijaonja ushindi, hivyo kesho wakiwa nyumbani kwa mara ya kwanza wanataka kuwapa burudani mashabiki wao.

"Simba haina ugeni hapa kutokana na mashabiki wake kuwa kila kona, kimsingi tumejiandaa vyema na vijana wanapaswa kuzingatia nidhamu, matarajio yetu ni ushindi tukiwa nyumbani" amesema Minziro.

Nahodha msaidizi wa timu hiyo, Benjamin Asukile amesema maelekezo waliyopewa na benchi la ufundi watayatumia vyema akieleza kuwa wamejipanga kisaikolojia kuhakikisha wanashinda mechi hiyo.

"Yeye kocha kazi yake imeisha, yaliyobaki ni ya kwetu wachezaji kuhakikisha tunacheza kwa umakini bila kurudia makosa kama mchezo uliopita dhidi ya Tabora United " amesema Asukile.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: