Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Rekodi zaibeba Simba kwa Mashujaa

Simba Kukipiga Na Mashujaa Tena Azam Sports Federation.jpeg Rekodi zaibeba Simba kwa Mashujaa

Tue, 9 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Baada ya Simba kuondoshwa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kwa sasa nguvu zao wamezielekeza kwenye mchezo wao wa kesho wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) hatua ya 16 bora wakati itakapocheza na Mashujaa Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma.

Simba iliondolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo baada ya kufungwa jijini Dar es Salaam bao 1-0 kisha kupoteza ugenini Cairo kwa kuchapwa 2-0 na kuondolewa kwa jumla ya 3-0 na kuaga mashindano hayo.

Wakati hilo likitokea kwa sasa hesabu za Simba za kunyakua ubingwa msimu huu ni kwenye michuano ya ndani ikiwemo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC ambayo haijalichukua kwa muda mrefu tangu mara ya mwisho ilipotwaa msimu wake wa 2020-2021.

SIMBA MBABE

Rekodi zinaibeba Simba katika mchezo wa leo ingawa kumbukumbu mbaya kwao ni kutolewa na Mashujaa kwenye hatua ya 64 bora ya michuano hii wakati huo ikishiriki Ligi Daraja la Kwanza (Championship) kwa kuchapwa mabao 3-2, Desemba 26, 2018.

Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, mabao ya Mashujaa yalifungwa na, Shabani Hamis, Jeremiah Josephat na Rajabu Athuman huku ya Simba yakifungwa yote na aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Paul Bukaba.

Kipigo hicho kilikuwa cha pili mfululizo kwa Simba kutolewa kwenye michuano hiyo baada ya msimu uliopita kupoteza mbele ya Green Warriors Desemba 22, 2017 katika hatua ya 64 kwa mikwaju ya penalti 4-3 kufuatia sare ya bao 1-1 dakika 90.

Mchezo wa mwisho kukutana wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Machi 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Simba ilishinda mabao 2-0 yaliyofungwa yote na Clatous Chama ikiwa ni ushindi wa pili wa timu hiyo kwa msimu huu zilipokutana.

Katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara baina ya timu hizo uliopigwa Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma, Simba ilishinda pia bao 1-0, Februari 3, mwaka huu lililofungwa na nyota wa kikosi hicho, Saidi Ntibazonkiza 'Saido' kwa penalti dakika ya 15.

Kwa mara ya kwanza timu hizi zilikutana katika mchezo wa kirafiki uliopigwa Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma Oktoba 14, 2019 ambapo Simba ilishinda bao 1-0, lililofungwa na aliyekuwa kiungo wa kikosi hicho Msudani, Shiboub Sharraf Eldin.

ZILIPOTOKA

Simba ilifika hatua hii kwa kishindo baada ya kuifunga TRA ya Kilimanjaro kwa mabao 6-0 huku kiungo wa timu hiyo, Sadio Kanoute akifunga matatu 'Hat-Trick' na mengine yakiwekwa kimiani na Ladack Chasambi, Freddy Michael na Pa Omar Jobe.

Kwa upande wa Mashujaa ilitinga hatua hiyo baada ya kuifunga Mkwajuni ya mkoani Songwe inayoshiriki Ligi ya Mabingwa wa Mkoa (RCL) mabao 2-1.

MABINGWA MARA NNE

Tangu michuano hii ilipoanzishwa rasmi mwaka 1967 ikifahamika FAT kabla ya kubadilishwa jina msimu wa 2015-2016, Simba imelitwaa taji hilo mara nne kuanzia 1995, 2016-2017, 2019-2020 na 2020-2021 ikipitwa na wapinzani wao Yanga iliyolitwaa mara saba.

Yanga ambao ndio mabingwa watetezi walianza kulitwaa taji hilo kuanzia 1967, 1974, 1998, 2001, 2015-2016, 2021-2022 na 2022-2023.

KAULI ZA MAKOCHA

Kocha Mkuu wa Mashujaa, Abdallah Mohamed 'Baresi' alisema licha ya kukaa kwa muda mrefu bila ya kucheza mechi yoyote ya kiushindani ila haiwezi kuwaathiri wachezaji wa timu hiyo kutokana na maandalizi bora waliyofanya ya utimamu wa kimwili.

"Tunaiheshimu sana Simba kwa sababu mechi zetu mbili tulizocheza nao walitufunga kutokana na makosa binafsi ya kiulizi tuliyokuwa tumeyafanya, kwa sasa tuko tayari kuonyesha dhahiri tumedhamiria kuepuka tulichokifanya mwanzoni," alisema.

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha alisema baada ya kuondolewa michuano ya kimataifa kwa sasa akili zao wamezielekeza katika mashindano ya ndani kwani wanatambua wana deni kubwa lililopo kwa mashabiki na viongozi wao.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: