Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Patamu, huku Baleke kule Fei Toto

Baleke X Fei Patamu, huku Baleke kule Fei Toto

Thu, 12 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

LIGI Kuu Bara imesimama kwa wiki mbili, huku mechi 40 hadi sasa zikipigwa.

Mechi hizo zimepigwa kuanzia Agosti 15 hadi Oktoba 8, zimezalisha mabao 89, huku wazawa 39 wakifunga mabao 50, wakiongozwa na kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga mabao manne, ikiwamo hat trick dhidi ya Tabora United.

Katika mabao hayo 50 yaliyofungwa na wazawa, mawili tu ndiyo yaliyofungwa kwa mikwaju ya penalti, ikiwa na maana 48 yametupiwa kawaida. Mabao hayo ya penalti kwa wazawa yamefungwa na Elias Maguri wa Geita na Danny Lyanga wa JKT Tanzania.

Kwa upande wa nyota wa kigeni ambao wapo zaidi ya 75 waliosajiliwa msimu huu miongoni mwa timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu ni 23 tu ndio waliofunga mabao wakichangia 39, huku kinara akiwa ni straika wa Simba, Jean Baleke aliyechangia matano ikiwamo hat trick dhidi ya Dodoma Jiji.

Katika mabao 39 ya nyota wa kigeni, manne yamekana na penalti likiwamo moja la Baleke. Penalti nyingine za wageni ni za Saido Ntibazonkiza (Simba), Eric Okutu (Tabora United) na Fabrice Ngoy wa Ngoy wa Namungo aliyekuwa wa kwanza msimu huu kufunga bao la penalti.

DR CONGO YAFUNIKA

Katika mabao 39, yaliyofungwa na mapro wa kigeni, DR Congo ndio iliyochangia mengi zaidi, ikifuatiwa na Zambia kisha Ivory Coast, Burkina Faso, Uganda na Ghana.

Kwa mujibu wa rekodi za mechi hizo 40 za Ligi Kuu, DR Congo pekee zimezalisha jumla ya mabao 10, yakiwamo matano ya Baleke, matatu ya kiungo wa Yanga, Maxi Nzengeli na moja moja ya Fabrice Ngoy na Fabrice Ngoma wa Simba.

Zambia imezalisha mabao matano, nyota wawili wa Simba, Clatous Chama na Moses Phiri kila mmoja akifunga mabao mawili na lingine kutoka kwa straika wa Mzambia, Kennedy Musonda aliyefunga moja.

PACOME, YAO NA AZIZ KI

Nyota wawili wa Yanga, Pacome Zouzoua na Yao Kouassi wameibeba Ivory Coast kwa kufunga jumla ya mabao manne ikiwa ni nchi ya tatu iliyozalisha mabao mengi kwenye Ligi Kuu hadi sasa.

Pacome ndiye kinara akifunga matatu, huku beki la kazi, Yao akiwa na bao moja na kuifanya nchi ya Ivory Coast kuandika historia kwa sasa kwenye ligi ikichangia mabao mengi.

Mataifa mengine yanayoifuata Ivory Coast kwenye kutupia mipira nyavuni kwenye Ligi Kuu hadi sasa ni Ghana na Uganda ambayo kila moja imezalisha matatu matatu.

Ben John anayekipiga Tabora United ndiye aliyeibeba Uganda kwa kufunga mabao mawili akifuatiwa na beki wa Kagera Sugar, Disan Galiwango aliyefunga moja sawa na straika wa Yanga, Hafiz Konkoni anayemfuata Eric Okutu wa Tabora United kuibeba Ghana hadi sasa katika ligi hiyo.

Kiungo wa Yanga, Stephane Aziz KI kwa upande wake ameibeba Burkina Faso kwa kufunga mabao matatu na kuifanya nchi hiyo kuingia kwenye orodha ya zilizozalisha mabao mengi.

SAIDO NA DUBE WAMO

Jumla ya mataifa manne yanafuata kwenye orodha ya nchi zilizozalisha mabao mengi kwenye ligi hiyo, huku Prince Dube wa Azam FC na kiungo mshambiuliaji wa Simba na mmoja ya wafungaji bora wa msimu uliopita, Saido Ntibazonkiza wakizibeba nchi za Zimbabwe na Burundi kila mmoja akifunga mabao mawili, sawa na yaliyofungwa na nchi za Cameroon na Kenya. Cameroon imechangia mabao hayo kupitia winga wa Simba, Willy Onana na Moubakarak Amza wa Ihefu ambao kila mmoja amefunga bao moja kama ilivyo kwa Wakenya Elvis Rupia wa Singida Big Stars na Joshua Nyatini wa Tanzania Prisons.

SOMALIA, TOGO ZIMO

Katika orodha ya nchi zilizochangia mabao 39 katika Ligi Kuu Bara msimu huu, Senegal, Somalia na Togo nazo zimo, baada ya nyota wa nchi hizo nazo kufunga wakati ligi ikienda kusimama kwa muda.

Marouf Tchakei, raia wa Togo anayekipiga Singida Big Stars, Ibrahim Elias wa KMC kutoka Somalia na beki wa Azam FC, Cheikh Sidibe wa Senegal ni kati ya waliochangia mabao hayo kila mmoja akifunga bao mojamoja na kufunga hesabu za mapro wa kigeni hadi sasa.

WAZAWA KAZI IPO

Japo ni mapema mno kwa sasa kuanza kutabiri upepo utakavyokuwa kwenye mwisho wa msimu wa Ligi Kuu, lakini ni wazi wazawa wanapaswa kukaza msuli kwani, nyota wa kigeni wapo moto kama msimu uliopita walipobeba Tuzo ya Mfungaji Bora.

Msimu uliopita Fiston Mayele aliyekuwa Yanga na Saido wa Simba ndio walibeba kila mmoja akifunga mabao 17 na kwa sasa, Baleke ndiye kinara akifuatiwa na Fei Toto mwenye mabao manne anawabeba wazawa, kisha wageni watatu Pacome, Aziz KI na Maxi wanaongoza orodha ya wenye mabao matatu kila mmoja sawa na mzawa, Matteo Antony wa Mtibwa Sugar.

Kulinganisha idadi ya mabao yote yaliyofungwa na wazawa yaani 50 kulinganisha na idadi yao (39) inatoa wastani mdogo wa kasi ya kutupia nyavuni ikiwa ni 1.28 kulinganisha na wageni ambao ni 23 kwa mabao 39 ikiwa ni wastani wa 1.7 ya mabao waliyofungwa hadi sasa, hata kama muda bado upo.

Hata hivyo, picha inaonyesha kasi ya ufungaji mabao kwa msimu huu katika mechi hizo 40 ni mdogo kulinganisha na mabao 89 ina maana ya wastani wake ni 1.43 tu ufungaji wa bao kwa kila mechi, kitu ambacho ni wazi ligi ikirejea tena, wazawa na wageni wanapaswa kukaza buti zaidi.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: