Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Panga la Simba kupita na hawa

Chama X Miquissone Mtibwa Panga la Simba kupita na hawa

Sat, 18 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Simba kinaendelea kujifua kambini kujiandaa na mchezo wa kwanza wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast, lakini akili za makosi wa klabu hiyo zipo kwenye dirisha dogo la usajili wakisubiri lifunguliwe hiyo Desemba 16 na kufungwa Januari 15 mwakani.

Mabosi wa Simba wapo kwenye presha kubwa kutoka kwa wanachama, mashabiki na wapenzi hasa baada ya kikosi hicho kufungwa mabao 5-1 na Yanga, huku kelele zikiwaangukia wao kwa kushindwa kusajili majembe ya maana na badala yake kusajili bora liende na kuifanya timu ipungue makali yake.

Ipo wazi kuwa, uongozi, mashabiki wa wadau wa timu hiyo kwa sasa hawaridhishwi na muenendo wa kikosi hicho na wapo tayari kwa mabadiliko.

Ndio maana haikuwa ajabu Jumanne iliyopita (Novemba 14), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alikaririwa akisema yeye na bodi kwa ujumla hawatakuwa tayari kuwavumilia wachezaji wasioonyesha kiwango bora uwanjani ilihali wanalipwa pesa nyingi.

Try Again aliyasema hayo katika mahojiano aliyoyafanya na kituo cha runinga cha Azam TV akiwapa muda wa takriban mwezi mmoja na nusu mastaa wa Simba wajitafakari kabla ya panga kupita.

“Nadhani kuna wachezaji ambao watapoteza nafasi zao, Simba haiwezi kukaa na kusubiri, Simba inahitaji mafanikio hivyo watakaoshindwa kuonyesha walichonacho kwa kipindi hiki ‘Thank You’ itawahusu, wale wote ambao hawako tayari, hatuko tayari kukaa nao,” alisema Try Again na kuongeza;

Hatutaki mchezaji anayekuja na kukaa benchi, tumewasajili kwa pesa nyingi na tunawalipa mishahara mikubwa hivyo tunataka kuona thamani ya pesa hizo uwanjani.”

Maneno hayo ya kiongozi huyo wa juu wa Simba, yanakuwa machungu kwa mastaa wengi wa Simba ambao msimu huu hawajafanya vizuri kutokana na namba zao na moja kwa moja wanaingia kikaangoni kujirekebisha kabla dirisha dogo la usajili halijafunguliwa la sivyo wanaweza kwenda na maji.

Mwanaspoti kupitia makala haya linakuletea baadhi ya mastaa wa Simba ambao wameingia moja kwa moja kwenye mtego wa kauli hiyo ya Try Again.

AYOUB LAKRED

Huyu ni kipa Mmorocco aliyesajiliwa na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea FAR Rabat ya kwao. Inaelezwa kipa huyo alisajiliwa kwa pesa ndefu na mshahara wake umechangamka lakini Wanasimba bado hawajamuona akitimiza majukumu yake yote.

Ayoub alisajiliwa kwa lengo la kusimama langoni kwa Simba kwa sababu aliyekuwa namba moja wa chama hilo Aishi Manula alikuwa majeruhi, lakini hadi sasa kipa huyo huyo hajaonyesha thamani yake kwani amedaka mechi mbili tu za ligi na mara nyingi amekuwa akikaa benchi mambo ambayo Try Again hataki hivyo kama asipobadilika huenda akapewa ‘Thank You’ mwezi ujao.

LUIS MIQUISSONE

Huyu ni kipenzi cha mashabiki wa Simba, lakini tangu amerejea kikosini hapo msimu huu akitokea Al Ahly ya Misri, amedoda. Miquissone alisajiliwa ili kuongeza nguvu zaidi kwenye kikosi cha Simba kutokana na rekodi zake alizoziweka unyamani hapo kati ya mwaka 2020 na 2021.

Miquissone ni miongoni mwa wale wachezaji Try Again anawataja kusajiliwa kwa pesa nyingi na kukaa benchi kwani tangu ametua msimbazi hapo amekuwa akianzia benchi tu na kuingia mara chache na katika mechi tisa za ligi hadi sasa ametoa asisti tatu tu.

SAIDI NTIBAZONKIZA

Huyu ni staa wa Simba na timu ya taifa ya Burundi akijulikana zaidi kwa jina la ‘Saido’. Licha ya kuwa mfungaji bora wa msimu uliopita akifunga mabao 17, msimu huu ameanza kinyonge kwani hadi sasa amefunga mabao mawili tu.

Kama Simba itaamua kutumia kigezo hicho cha namba, Saido naye atakuwa matatani kutemwa, kama hatabadilika haraka kwani ni miongoni mwa wachezaji wa Simba wanaolipwa pesa nyingi.

KRAMO AUBIN

Huyu jamaa bwana aliandamwa na majeraha tangu ametua Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast.

Hadi sasa, Kramo hajacheza mechi hata moja ya mashindano kwa Simba na yupo nchini kwao akiunguza jeraha la goti alilopata.

Jina la mshambuliaji huyu huenda likawa la kwanza kukatwa katika dilisha dogo kwani hajafanya kile ambacho Simba ilimnunua kufanya, ingawa kuna uwezekano wa kusubiriwa kuangaliwa kwanza arudi kutoka majeruhi ili kuona atawapa kitu gani, vinginevyo itakula kwake mazima.

JOHN BOCCO

Huyu ndiye nahodha wa Simba, Bocco ni miongoni mwa wachezaji watatu wazawa wa Simba wanaolipwa pesa nyingi lakini muenendo wake uwanjani umekuwa wa kusua sua.

Licha ya kuwa kiongozi wa wenzake lakini ameshindwa kufanya vizuri na kupata namba ya uhakika kikosini hapo jambo linalowafikirisha mashabiki wengi wa timu hiyo kwanini anabaki.

Kama Simba itatumia kigezo cha wachezaji wanaolipwa pesa nyingi lakini wanakaa sana benchi kupunguza watu, basi nahodha Bocco naye panga huenda likampitia, baada ya kunusurika kwenye dirisha kubwa lililopita ambalo lilimhusisha kutemwa kabla ya kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ kumbakiza. Robertinho ameshatimuliwa sambamba na wasaidizi wake wawili baada ya kipigo cha Yanga.

WILLY ONANA

Huyu ni mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Rwanda kwa msimu uliopita akicheka na nyavu mara 16, jambo lililowashawishi Simba na kuamua kumsajili lakini hadi sasa hajaonyesha thamani yake uwanjani.

Onana ameonekana kuwa mchezaji asiye na madhara kwa wapinzani kutoka kikosi cha Simba na mara nyingi ameishia kukaa benchi na hata pale anapopata nafasi amekuwa akionyesha kiwango cha kawaida. Kama asipobadilika na kuendana na matakwa ya Simba, basi naye ‘Thank You’ itamuhusu katika dilisha dogo.

WENGINEO

Nassoro Kapama, Mohamed Mussa, Jimmyson Mwanuke na Israel Mwenda ni wachezaji waliokuwepo Simba tangu msimu uliopita lakini wameshindwa kuonyesha changamoto kikosini hapo na kupata nafasi ya kucheza hivyo huenda ‘Thank You’ ya mwezi ujao ikawahusu.

Wengine ni wale waliosajiliwa msimu huu, Hussein Abel, David Kameta ‘Duchu’, Hussein Kazi, Abdallah Khamis na Shaaban Idd Chilunda ambao nao hawajaonyesha makeke kikosini Simba, hivyo kama kauli ya ‘Hatujasajili wachezaji wa kukaa benchi,’ aliyoitoa Try Again itatafsiriwa vyema basi nao wapo kikaangoni.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: