Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ni kweli Simba inampa hasara Mo Dewji?

Mohammed Dewji Mo Rais wa Heshima wa Simba SC, Mohamed Dewji

Sat, 2 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kuna mjadala mkubwa unaendelea huko mitandaoni kuhusu Mwekezaji wa Simba, Mohamed Dewji. Ni mjadala mkubwa.

Mjadala huu umechagizwa na kauli ya Mo Dewji kuwa ameinunua Simba miaka mitano iliyopita. Ni ngumu kuamini taarifa hiyo, kwani haijulikani aliinunua lini? Kwa kiasi gani cha fedha na tenda ilitangazwa lini na washindani wake walikuwa ni kina nani?

Pia alikabidhiwa na nani mauzo hayo ya klabu hiyo ya umma inapambana kuendeshwa kwa mfumo wa Hisa? Pia Mo Dewji akaenda mbali zaidi na kusema timu hiyo imempa hasara ya Sh51 Bilioni.

Ni kauli ya kushtua kwa Wanasoka. Kwa nini? Kwa sababu kwanza haiko wazi kama Mo Dewji tayari amekamilisha ununuzi wake wa hisa za Simba au la.

Pili kiasi cha fedha ambacho Dewji anasema amepata hasara ni kikubwa sana. Inafikirisha.

Ni kweli Mo Dewji anatoa pesa ndani ya Simba. Lakini swali linabaki, anatoa kiasi gani kila msimu?

Tangu amekubali kuwekeza Simba ni miaka saba imekwisha. Ni kweli katika kipindi cha miaka saba Simba imeingiza hasara ya Sh51 Bilioni? Ni ngumu.

Ni kweli Simba inatumia fedha nyingi kujiendesha. Inasajili wachezaji kwa gharama kubwa. Inalipa mishahara na posho kubwa kwa wachezaji wake na benchi la ufundi.

Inatumia gharama kubwa kwenye mechi za kimataifa. Hata hivyo, bado kiasi alichotaja Mo Dewji kinaonekana hakina uhalisia.

Simba ina wadhamini wengi. Inavuta pesa ndefu kutoka Azam TV katika haki za matangazo ya televisheni. Ni zaidi ya Sh3 bilioni kwa msimu.

Inapata Sh2 Bilioni kutoka kwa mzabuni wao wa jezi Sandaland. Inapata pesa kutoka CAF. Ni kweli fedha hizo hazifiki hata nusu ya bajeti yake? Hapana.

Kwenye bajeti ya Simba kwa msimu uliopita inaonyesha Dewji alichangia Sh2 bilioni na nyongeza kidogo. Fedha nyingine alilipa kama sehemu ya udhamini wa bidhaa zake zinazokaa kwenye jezi ya Simba. Ni kweli anafanya kwa hasara? Inafikirisha sana.

Ninachofahamu ni bado Simba haijaweza kujiendesha kwa faida, lakini bado siamini kama inaingiza hasara kubwa kiasi hicho.

Kama hasara ni kubwa kuna haja ya kupunguza matumizi yasiyo na lazima. Mfano kwenda kuweka kambi ya maandalizi ya msimu huko Ulaya. Haina ulazima.

Hakuna sababu ya kuweka posho kubwa kwa wachezaji ambao tayari wana mishahara mikubwa.

Katika eneo la usajili inabidi kufanyike mabadiliko makubwa. Kwenye miaka hii ya karibuni, Simba imesajili wachezaji wengi ambao wamefeli na kuondoka.

Kuvunja mikataba ya wachezaji hawa ni gharama. Mfano kina Victor Akpan, Augustine Okrah, Aubin Kramo, Nelson Okwa, Ismael Sawadogo na wengineo ni sehemu ya usajili wa Simba uliofeli.

Ikitokea kila msimu wanasajiliwa wachezaji wengi na kufeli ni hasara kwa klabu. Kwanza inawalipa ili kuvunja mikataba yao, halafu inaingia gharama kubwa kusajili wachezaji wengine.

Kwa mantiki hiyo lazima Mo Dewji aone hasara ni kubwa. Matumizi yanakuwa makubwa kila msimu.

Bahati mbaya ni kwamba wakati huu Mo Dewji analalamikia hasara hiyo, ni wakati ambao kikosi cha Simba kinahitaji mabadiliko makubwa.

Wachezaji wengi wamechoka. Wachezaji wengine umri umesogea hivyo timu inapaswa kuanza kufikiria mbadala wao.

Ni kama kwenye eneo la ushambuliaji. John Bocco anaondoka mwishoni mwa msimu, anatakiwa mbadala wake. Bado hawa kina Freddy Michael na Pa Omary Jobe hawajaonyesha kiwango cha kuridhisha.

Kule kwa Shomari Kapombe kunahitajika mbadala wake. Kwa Mohamed Hussein kunahitajika mtu mwingine wa kuvaa viatu vyake.

Kwenye nafasi ya kiungo Mzamiru Yassin ameanza kuchoka. Saido Ntibazonkiza umri umeanza kumtupa mkono wakati Luis Miquissone gari limegoma kuchanganya.

Ni wazi Simba inahitaji kufanya usajili huo mkubwa mwishoni mwa msimu. Hivyo ni lazima Mo Dewji aendelee kutoa fedha.

Katika upande mwingine ili kupunguza hizi lawama ni lazima Simba ikamilishe huo mchakato wa mabadiliko. Dewji anatakiwa kuwepo kisheria na sio kuonekana kama anafanya hisani.

Endapo mchakato huo utakamilika, Simba inaweza kujiendesha kibiashara zaidi. Inaweza kupata wadhamini zaidi.

Ni nyakati hizi ambazo Simba inahitaji kuwa na uwanja wake. Tayari ina eneo pale Bunju. Imejenga uwanja wa mazoezi lakini inaweza kuendeleza mradi huo. Inawezekana kama mchakato wa uwekezaji utakamilika mapema.

Sehemu nyingine ni kuongeza nguvu ya Wanachama kuchangia timu yao. Usajili wa Wanachama unapaswa kufanyika kwa nguvu. Yanga wamefanikiwa katika hilo.

Kila siku wanaongeza mamia ya wanachama. Wanapata fedha ndefu kupitia wanachama wao. Mwaka jana walitangaza kupata zaidi ya Sh1 Bilioni. Ni fedha nyingi. Simba ni kama vile wanachama wanaamini Dewji atafanya kila kitu. Haiwezekani.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: