Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngoma aanika kila kitu, Cadena atemacheche

Ngoma Pics Kiungo wa Simba SC, Fabrice Ngoma

Mon, 13 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mastaa wa Simba wanaingia kambini leo kujiandaa na mechi ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast itakayopigwa Novemba 25, jijini Dar es Salaam, huku baadhi yao wakikiri wamesikia manung’uniko ya wanachama na mashabiki wa timu hiyo wakiahidi kuwapa raha.

Tangu kipigo cha mabao 5-1 ilichopewa na Yanga katika mechi ya watani ya Kariakoo Derby, Simba hali ni kama haijatulia kwa mabosi wa klabu hiyo kujifungia kwa siku zaidi ya mbili wakipanga mikakati baada ya awali kuwafuta kazi makocha watatu kwa mpigo akiwamo kocha mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’.

Pia mitaani hadi kwenye mitandao ya kijamii kumekuwa na kelele nyingi kutoka kwa Wanasimba wakiushutumu uongozi na hata wachezaji, lakini sasa mastaa wa timu hiyo wameamua kuvunja ukimya na kuwatuliza kwa kuwaambia; ‘Tulieni, tumewasikia na tunajipanga kuwapa raha zaidi.’

Kauli hiyo imetolewa na kiungo Fabrice Ngoma na nahodha msaidizi, Mohamme Hussein ‘Tshabalala’, waliosema kwa nyakati tofauti kuwa, hata wao wanaumia kwa kilichotokea Novemba 5, na sasa wanajipanga upya ili kuwapa raha mashabiki wa klabu hiyo kwa mechi za CAF na zile za ligi ya ndani.

Ngoma, aliyesajiliwa msimu huu akiwa mmoja ya wachezaji 11 wapya, alisema kwa uzoefu wake wa soka la Afrika, presha za namna hiyo huwa zipo sana na alipitia hivyo akiwa Raja Casablanca lakini anajua namna ya kukabiliana nazo na kuzishinda.

“Mara nyingi mashabiki wanataka matokeo mazuri tu, na ni haki yao lakini wanatakiwa kutambua soka lina matokeo matatu, kushinda, kutoa sare na kupoteza. Tunajua namna mashabiki wetu wameumia lakini haina budi kutoa lawama kwa yeyote yule, tunatakiwa kuungana kuwa kitu kimoja na naamini tutarejea kufanya vizuri kwani bado tupo kwenye msitari na kila kitu kinawezekana,” alisema Ngoma ambaye alitajwa na Robertinho, kama usajili bora wa msimu huu sambamba na beki Che Malone Fondoh.

Kwa upande wa Zimbwe Jr, alisema muda wa mapumziko kupisha ratiba za mechi za timu za taifa, watautumia kujitathimini na kujiandaa kwa ajili ya kurejea kwenye ushindani.

“Matokeo yaliyotokea hatukuyatarajia ila tayari yamepita, kipindi hiki cha mapumziko tutakitumia vyema kuangalia wapi tulikosea ili kurekebisha lakini kitatusaidia pia kurejesha morali yetu. Hatupaswi kuhuzunika sana bali kuinua vichwa vyetu na kusonga mbele,” alisema Zimbwe Jr ambaye ni mchezaji mwandamizi kwa sasa kwenye kikosi hicho alichojiunga nachi tangu mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar.

CADENA ATEMA CHECHE

Kwa upande wa kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Dani Cadena aliwatoa hofu mashabiki na wadau wa Simba akiwataka kujivunia timu yao kwani bado ina nafasi ya kufanya vizuri.

Kocha huyo aliyetua Simba kama kocha wa makipa mwanzoni mwa msimu huu licha ya kuwa anasifa zote za kuwa kocha mkuu, alisema Simba haijapoteza ramani kwani bado ina uwezo wa kufikia malengo yake kinachotakiwa ni kuwa na subra tu. “Ligi bado ina mechi nyingi, timu ipo makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, kwanini watu wawe na wasiwasi?” Alihoji Cadena aliyetua Msimbazi akitokea Azam FC na kuongeza;

“Duniani kote kupoteza mechi ya dabi huwa inauma na kuvuruga lakini sio mwisho wa mashindano, Simba ni timu kubwa na ina nafasi nzuri tu ya kufikia malengo yake hivyo watu wasiwe na shida sana, tusubiri muda utaongea.”

Wakati mabosi wa Simba wakitarajia kumalizia vikao vyao vilivyoanza tangu wikiendi iliyopita, leo Jumatatu cha kupanga mikakati ya kumleta kocha mpya, msaidizi na kocha wa viungo baada ya Robertinho, Ounane Sellami na Corneille Hategekimana kufungashiwa virago, Mwanaspoti linajua Simba inataka kushusha wataalamu hao watatu kabla ya mechi ya Asec Mimosas.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: