Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ngoma: Ukweli wa Simba ni huu

Fabrice Ngoma Mapinduzi.jpeg Kiungo wa Simba SC, Fabrice Ngoma

Sat, 13 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Simba, kipo mjini Singida kwa ajili ya pambano la Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji, Singida Black Stars (Ihefu) linalopigwa jioni ya leo kwenye Uwanja wa Liti, huku mashabiki wa timu hiyo wakiwa hawakielewi kikosi hicho, lakini kiungo Fabrice Ngoma amevunja ukimya akianika tatizo lilipo.

“Mashabiki wetu wana matarajio makubwa na kikosi chetu wameumia na haya matokeo na hata sisi wachezaji yametuumiza pia kilichotokea hatukukitarajia,tulishafanya makosa, lakini tatizo kubwa ni kushindwa kujituma vilivyo,” alisema Ngoma.

Mashabiki wa Simba kwa sasa kila mmoja amekuwa akitupa lawama eneo analoamini limechangia timu hiyo kutolewa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Ahly ya Misri na katika michuano ya Kombe la Shirikisho (FA) mbele ya Mashujaa, lakini Ngoma amefunguka na kuwajaza upepo wenzake.

Kiungo huyo raia wa DR Congo aliyetua Msimbazi akitoka Al Hilal ya Sudan, amesema kama wachezaji wameshagundua wapi walipojikwaa na kwa sasa ni wajibu wao kujitathmini na kuanza safari mpya ya mabadiliko kuanzia leo watakapobiliana na Ihefu (Singida BS) ugenini kabla ya kuivaa Yanga wiki ijayo.

Simba inavaana na Ihefu iliyohamia Singida ikitokea Mbarali, Mbeya mchezo ambao Ngoma anataka kuona mastaa wenzake kuamka na kusaka ushindi utakaokwenda kutuliza upepo mbaya. Akizungumza na Mwanaspoti, Ngoma alisema hata wao kama wachezaji wanaumizwa na hatua ya timu yao kutolewa kwenye mashindano mawili ndani ya wiki moja wakianzia Ligi ya Mabingwa Afrika kisha Kombe la Shirikisho (FA).

Ngoma alisema hakuna mwingine ambaye anaweza kubadilisha upepo huo mbaya isipokuwa wenyewe kama wachezaji wa Simba na kama kila mmoja wao atajituma kwa asilimia 80 hadi 100, Wekundu hao watayaondoa matokeo yaliyowatibulia.

Simba haijashinda mechi tatu zilizopita ikipoteza mechi mara mbili mbele ya Ahly kwa kulala nyumbani bao 1-0 na ugenini kupigwa 2-0 katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kisha ikatolewa kwa penalti 6-5 na Mashujaa Kombe la Shirikisho, baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1. “Huu sio wakati wa kuendelea kuinama chini, nadhani watu sahihi wanaotakiwa kubadilisha haya matokeo ni sisi wachezaji nafikiri kama kila mchezaji akijituma kuanzia asilimia 80-100 Simba haiwezi kutoka bila matokeo mazuri.

“Mashabiki wetu kazi yao kuja kutupa nguvu wasisite kuja uwanjani nasi kwe kuwa haya matokeo yametuumiza tutafanya juhudi kubwa kubadilisha upepo kuanzia mechi hii ya Ihefu.”

Aidha Ngoma alisema amefurahishwa na hatua ya kila mchezaji kuonyesha kuwa tayari kutamani kuona timu yao inapata ushindi kwenye mechi zao zinazokuja baada ya kuwa na vikao tofauti vya wenyewe kwa wenyewe.

Simba kwa sasa inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu ikikusanya pointi 45 kupitia mechi 19 na mara baada ya kumalizana na Ihefu leo, wikiendi ijayo itakuwa na Kariakoo Derby dhidi ya Yanga inayoongoza msimamo na alama 52 kwa mechi 20 ikiwa pia ni watetezi wa taji hilo.

Ushindi wa aina yoyote mbele ya Ihefu utaiwezesha Simba kufikisha pointi 48 na kuishusha Azam yenye 47 ikicheza michezo 21 na itakayoshuka uwanjani kesho ikiwa ugenini kuikabili Namungo kwenye Uwanja wa Majaliwa.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: