Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nani kasema Kapombe, Tshabalala wamezeeka?

Kapombe Na Tshabalala Mohamed Hussein Nani kasema Kapombe, Tshabalala wamezeeka?

Mon, 9 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hii nchi imejaa mambo ya ajabu mengi. Kila mtu ni mjuaji sana. Kuna watu wanajua siasa, burudani, soka, mambo ya kijamii na kila kitu. Watu wa ajabu sana. Ndio Tanzania.

Miaka ya nyuma kuna watu walianza kusema Wema Sepetu amezeeka. Mtu anazeekaje akiwa na umri wa miaka 30? Inashangaza sana.

Kisa Wema alikuwa Miss Tanzania 2006 watu wanakwambia leo amezeeka. Kwanini? Kwa sababu wamekuwa wakimuona kwenye ubora wake kwa miaka mingi.

Kwanini Wema azeeke halafu Kajala Masanja awe kijana? Wakati Wema anakuwa Miss Tanzania, Kajala tayari alikua na Paula. Leo Wema ni mzee halafu Kajala ni kijana.

Kwanini Jokate, Aunt Ezekiel, Irene Uwoya na wengineo walikuwa na Wema mwaka 2006 hawaonekani wazee? Hapa unagundua kuwa ni wivu tu. Watu wana mambo ya ajabu.

Ndivyo ambavyo ilivyo kwenye soka sasa. Walianza na Juma Kaseja. Wakati anaendelea kupambana na maisha yake ya soka, watu wakasema amezeeka. Wakaanza kumnyooshea vidole.

Bahati nzuri ni kwamba aliyekuwa Kocha wa Taifa Stars kwa wakati ule, Etienne Ndayiragije akamjumuisha katika kikosi. Kaseja akatubeba pale Kenya mwaka 2019 kwenye mechi za kufuzu Chan. Akadaka mikwaju kadhaa ya penalti na timu ikasonga mbele.

Akaja kwa Mkapa akatubeba mbele ya Burundi. Akapangua mikwaju kadhaa ya penalti. Watu wakasahau kama walisema ni mzee sasa atundike darunga. Ndio Watanzania.

Hapa katikati wameanza kumnyooshea vidole Mbwana Samatta. Baadhi ya mashabiki wanasema amezeeka na astaafu kuchezea timu ya Taifa. Inashangaza sana.

Wakati Watanzania wakiona Samatta amezeeka, akatua kwenye timu ya PAOK ya pale Ugiriki. Wagiriki wamemuona Samatta bado anadai na anaweza kuwasaidia katika timu yao, wakati huku mashabiki wanadai ni mzee atundike daruga.

Ndio changamoto ya Watanzania. Ujuaji ni mwingi sana. Watu wanamuona Cristiano Ronaldo na Lionel Messi ni vijana halafu Samatta amezeeka. Basi kwa sababu hao wengine siyo Watanzania.

Tumeumbwa kuamini vitu vya ajabu. Anayepambana kuendelea kuwa katika ubora wake kwa miaka mingi tunamuona mzee, halafu wale wengine tunawaona vijana.

Ombwe hili sasa limewafikia Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’. Watu wameanza kuwanyooshea vidole kuwa wamechoka na wapewe mapumziko. Inashangaza sana.

Yaani leo Tshabalala na Kapombe wamechoka? Nani kasema? Hawa ni mabeki bora wa pembeni ambao tunao katika ligi yetu. Unawezaje kusimama na kusema kuwa wamechoka? Ni ushamba na ujinga.

Kapombe ameanza kucheza soka miaka 13 iliyopita. Alianza akiwa kijana mdogo tu pale Simba. Akapambana kupata nafasi yake. Akafanikiwa. Baada ya misimu miwili tu Simba ikapata ofa kutoka klabu ya AC Cannes ya pale Ufaransa. Ikamuuza huko.

Baada ya mwaka mmoja, Kapombe akashindwana na Wafaransa hao. Akarejea nyumbani. Akajiunga na Polisi Morogoro. Akafanya nao mazoezi kwa msimu mmoja kisha akatua Azam FC.

Akiwa chini ya kocha Stewart Hall, akarejesha makali yake. Nchi nzima ikawa inamuimba Kapombe. Beki wa kisasa. Anapanda na kushuka. Anatoa pasi za mabao. Akawa anafunga. Inafurahisha sana.

Baada ya Azam FC kufanya uzembe na kushindwa kumuongeza mkataba, Kapombe akahamia Simba tena ambako amekuwa kikosi cha kwanza mpaka leo. Ndiyo mabeki wapambanaji walivyo.

Hadi kufikia msimu huu hakuna beki bora mwingine wa pembeni ambaye amekuja katika zama hizi za Kapombe. Angalau msimu huu tunamfananisha na Yao Kouassi wa Yanga. Kwanini? Kwa sababu Kapombe ni bora.

Vipi kuhusu Tshabalala? Huyu ni miongoni mwa mabeki bora wa kushoto kuwahi kutokea nchini. Yupo Simba kwa miaka tisa sasa tangu alipojiunga nao mwaka 2014. Kabla ya hapo, Tshabalala alitumika muda mwingi kwenye timu za vijana za Azam FC. Kisha akatua Kagera Sugar.

Tangu Tshabalala ameanza kucheza soka wala haijatimia miaka 15, tunawezaje kusema amezeeka sasa? Ni ushamba tu.

Tangu Tshabalala ametua Simba amekuwa beki tegemeo wa kushoto. Wakati fulani aliumia akaletwa Asante Kwasi pale Simba kumpa changamoto. Nini kilitokea? Kwasi alicheza kwa ubora msimu mmoja tu, baada ya hapo Tshabalala akarudi katika nafasi yake. Baada ya hapo Simba imesajili mabeki wengi wa pembeni na hakuna aliyewahi kufikia ubora wa Tshabalala.

Anacheza katika ubora uleule kwa miaka tisa sasa. Kwanini leo tunaanza kusema amezeeka? Ni kwa sababu ya mechi moja tu ya Power Dynamos? Ni ujinga. Hata wachezaji bora hushindwa kufanya vizuri kwenye mechi fulani. Ni kama ilivyowakuta Tshabalala na Kapombe dhidi ya Power Dynamos. Inatokea. Lakini siyo sababu ya kusema wamezeeka.

Kama Kapombe na Tshabalala wamezeeka nani ni kijana? Tuache kukatisha tamaa wachezaji wazuri. Tunajiangusha kama nchi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: