Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mziki wa Chama wamdatisha kocha

Chama Vs Jwaneng.jpeg Mziki wa Chama wamdatisha kocha

Mon, 4 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kama unadhani hiki ndicho kilele cha kiwango cha Mwamba wa Lusaka, Clatous Chama, basi unajidanganya. Hilo ameeleza kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha baada ya fundi huyo kuonyesha kiwango cha juu katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao Wekundu wa Msimbazi waliinyuka Jwaneng Galaxy kwa mabao 6-0.

Katika mchezo huo ambao ulichezwa jana Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, Chama aliupiga mwingi na kuwavuruga wageni akiifanya Simba iwe hatari kwenye eneo la mwisho la ushambuliaji akiwa ndiye aliyeingia mara nyingi zaidi katika eneo la penalti la Jwaneng Galaxy, akifanya hivyo mara mane kuliko mchezaji yeyote ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza.

“Chama ni mchezaji hatari zaidi katika kukabiliana na mtu kwa mtu (one against one), na alichofanya leo (juzi) ni maajabu na kile ambacho mnakiona kutoka kwake ni kidogo katika uwezo mkubwa alionao. Ninyi bado hamjamuona Chama mwenyewe...," amesema Benchikha aliyeiwezesha USM Alger ya Algeria kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika na CAF Super CAF akizizidi ujanja Yanga na Al Ahly mtawalia.

Takwimu zinaonyesha kwamba katika dakika 90 za mchezo huo wa jana, Chama alipiga mashuti sita, akifunga na kutoa astisti moja na ndiye mchezaji wa Simba aliyepewa alama kubwa zaidi katika mitandao mbalimbali inayopima ufasini wa mchezaji mmoja mmoja uwanjani katika mchezo husika.

Kwa upande wake, Chama amewapongeza wachezaji wenzake kwa kazi kubwa ambayo walifanya katika mchezo huo ambao walihitaji ushindi ili kutinga robo fainali ya nne kwenye michuano ya klabu ya Afrika.

"Ilikuwa siku ya kipekee. Kila mmoja alijitoa kwa ajili ya timu. Hii ni hatua moja bado nyingine ambayo ni robo fainali. Mashabiki wetu walifanya kazi nzuri na kubwa ya kuwa nyuma yetu. Tulijisikia kupambana muda wote," amesema Mwamba wa Lusaka.

Katika mchezo huo, Chama alishinda mara nyingi vita dhidi ya mabeki tofauti (1 vs 1) ambao alikuwa akikabiliana nao na aliifanya Simba kuwa na nguvu upande wa kushoto ambako alikuwa akitokea.

Nyota huyo hakuibuka tu kuonyesha kiwango bora kwenye mchezo huo, amekuwa kwenye mwendelezo wa kufanya vizuri tangu arejee kikosini baada ya kumalizika kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.

Miongoni mwa michezo ambayo aliibeba Simba ni pamoja na ule wa Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania ambapo bao lake liliifanya timu hiyo kuvuna pointi tatu kabla ya kwenda Ivory Coast kukabiliana na Asec Memosas.

Siyo Benchikha pekee, bali pia kocha wa Jwaneng Galaxy, Morena Ramoreboli naye amemmwagia sifa Chama akisema alikuwa mwiba kwao na kuitakia Simba kila la heri katika hatua ya robo fainali ambako inaweza kukutana na wababe wenzake Afrika kama Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Petro de Luanda ya Angola au Al Ahly ya Misri.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: