Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mshtuko ghafla tu wamegoma wakasepa kwengine

Pape Sakho TT.jpeg Mshtuko ghafla tu wamegoma wakasepa kwengine

Fri, 8 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Dirisha kubwa la usajili nchini lilifungwa Agosti 31, mwaka huu na msimu wa ligi tayari ulikuwa umeanza.

Zipo timu ambazo zilikuwa zimemaliza usajili wao na kutangaza wachezaji kabla ya msimu kuanza na nyingine zilisubiri hadi dakika za mwisho kukamilisha usajili wao.

Katika dirisha hili, mengi yametokea likiwamo la mastaa wakubwa ambao walitarajiwa kuwepo kwenye timu zao msimu huu, kuondoka kwa ajili ya kusaka changamoto mpya kwengine.

Wapo walioondoka kwa kuomba au kuachwa na wengine walilazimisha tu kwa sababu maalumu, nyingine zikiwa ni kupata nafasi ya kucheza, kutakiwa na timu nyingine yenye dau kubwa na wengine kushindwana na waajiri wake.

Wababe wa Ligi Kuu Bara, Yanga na Simba ni kati ya wahanga wa sakata la kukimbiwa na nyota wao kwa kulazimisha kuondoka huku mabingwa watetezi Wanajangawani ikiwa ndio mhanga zaidi.

Mwanaspoti linakuletea mastaa sita waliolazimisha kuondoka kwenye timu zao wakiwa bado wanahitajika.

FISTON MAYELE

Alikuwa mmoja wa nyota tegemeo Yanga na aliisaidia kushinda mataji kwa misimu miwili na kuifikisha kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Alijitengenezea Ufalme Jangwani akifunga mabao 33 katika misimu miwili aliyocheza Ligi Kuu Bara na kuwa mshambuliaji tishio, huku kimataifa akiibuka mfungaji bora baada ya kutupia mabao saba.

Kutokana na ubora wake, timu kubwa Afrika zilianza kummezea mate na Pyramid FC ya Misri ilimwekea mkwanja mrefu mezani.

Hata hivyo, akiwa bado na mkataba wa mwaka mmoja, viongozi wa Yanga walijaribu kutaka kumbakiza, lakini dau nono la Pyramid lilitosha kumaliza ufalme wake Jangani na kuuhamishia Misri na Yanga kumruhusu kwenda kuanza maisha mapya huko.

FEISAL SALUM ‘FEI TOTO’

Kiungo huyu wa boli, alitikisa kabla na wakati wa usajili.

Alianza kwa kujiweka pembeni kwenye kikosi cha Yanga katikati ya msimu kwa madai ya kuboreshewa mkataba wake.

Tangu desemba 23 mwaka jana, alihusishwa na kutua Azam FC na aliaga mashabiki wa Jangwani kwenye kurasa za mitandao yake ya kijamii.

Hata hivyo, baada ya mabosi wa Yanga kushtukia hilo, waliweka ngumu wakisisitiza bado ni mchezaji wao halali na anayemtaka ni lazima wakae mezani wazungumze.

Baada ya mvutano wa muda mrefu, hatimaye pande hizo mbili zilikaa na kukubaliana na Feisal kutua Azam FC na tayari ameifungia mabao matatu kwenye mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Mashujaa kwenye ushindi wa mabao 4-0.

Kiungo huyo alisajiliwa na Yanga akitokea JKU ya Zanzibar

YANICK BANGALA

Alisajiliwa kama kiungo mkabaji lakini baada ya kutua Yanga alitumika nafasi mbili tofauti beki wa kati na kiungo mkabaji na kote alifanya kazi kwa ubora.

Msimu wake wa kwanza Yanga alitumika zaidi nafasi ya kiungo na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa msimu aliiongoza timu yake kutwaa ubingwa msimu uliofuata alichanganywa nafasi akicheza beki na kiungo.

Ameitumikia Yanga kwa mafanikio akitwaa mataji sita Ngao, Ligi na Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) misimu miwili mfululizo huku akicheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga ikiwa bado inamhitaji kutokana na kuwa na mkataba na timu hiyo wa mwaka mmoja alioibuka kwenye vyombo vya habari na kubainisha ana asilimia 20 za kubaki huku 80 ikiwa ni kuondoka.

Lengo lake limetimia baada ya uongozi wa Yanga kufanya biashara na Azam FC kwa kumuuza mchezaji huyo.

DJUMA SHABAN

Kuondoka kwake Yanga sio kwa wema kwani hata jina lake ni miongoni mwa waliopewa mkono wa kwa heri na bado alikuwa na mkataba na timu hiyo wa mwaka mmoja.

Djuma sambamba na Bangala waliongezwa mkataba wa mwaka mmoja katikati ya msimu ambao ulikuwa ni wa mwisho kwao kuitumikia Yanga baada ya kujiunga nayo kwa miaka miwili ambayo wameitumikia kwa mafanikio wakitwaa mataji sita.

Djuma hadi sasa haijajulikana atacheza timu gani msimu huu baada ya kuachwa na Yanga baada ya makubaliano ya pande zote mbili na wanasubiri ofa ya timu yoyote ili wafanye biashara.

Hata hivyo, siku moja kabla dirisha halijafungwa alitajwa kutua Azam FC lakini dili lake lilishindikana baada ya Azam kushindwa kuachana na kipa Ali Ahmada.

JOASH ONYANGO

Beki mwenye mafanikio ndani ya Simba alilazimika kuomba kuondoka ndani ya kikosi hicho kutokana na lawama dhidi yake ikiwa ni pamoja na ujio wa beki mwingine wa kigeni ndani ya kikosi cha Simba, Che Malone.

Onyango tayari ametimkia Singida Fountain Gate akipishana na Pascal Wawa ambaye ameachwa baada ya mkataba wake na timu hiyo kumalizika.

Onyango alitua Simba, Agosti, 2020 kwa mkataba wa miaka miwili na kuongeza mwingine msimu uliopita unaomalizika katikati ya msimu ujao na sasa anakipiga Singida Fountain Gate kwa mkopo wa mwaka mmoja.

PAPE SAKHO

Ujio wa Luis Miquissone ndio uliomwondoa kikosini na uongozi ulifanya uamuzi wa kumrudisha aliyekuwa staa wao huyo wa zamani kutokana na kutopata kitu kikubwa walichokuwa wanatarajia kutoka kwa Sakho.

Winga huyo ambaye ameondoka Simba na rekodi ya kupata kiatu cha dhahabu kutoka CAF kutokana na kufunga bao moja la mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ameuzwa na kuinufaisha Simba.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: