Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkizubaa tu mnapigwa leo

Simba Singida6401441 Mkizubaa tu mnapigwa leo

Sun, 8 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Utamu wa Ligi Kuu Bara unaendelea tena leo kwa mechi mbili zitakazopigwa kwenye viwanja viwili tofauti, lakini macho na masikio ya mashabiki yataelekezwa mjini Singida, wakati Simba itakapokuwa ugenini kuvaana na Singida Big Stars, huku kila timu ikitoka kupata ushindi mechi zilizopita za ugenini.

Simba iliishinda Tanzania Prisons kwa mabao 3-1 Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, wakati Singida iliinyoa na kuonja ushindi wa kwanza wa Ligi msimu huu kwa kuilaza Mtibwa Sugar  1-0 kwenye pambano kali lililopigwa Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.

Mechi nyingine ya leo ni ile itakayozikutanisha Tanzania Prisons itakayosalia nyumbani kuikaribisha Mtibwa wakati zote zikiwa zinauguza maumivu ya vipigo zilivyopata mechi zilizopita, na zikisaka ushindi wa kwanza msimu huu ili kujiondoa kwenye eneo la chini la msimamo wa ligi hiyo inayoongozwa na Azam FC.

Mechi zote za leo zinachezwa kuanzia saa 10 jioni, huku pambano la mjini Singida litakuwa la tatu kwa Simba na Singida kukutana mwaka huu na wenyeji wakiwa na hasira za kutaka kulipa kisasi kwa wageni.

Simba iliifumua Singida Februari kwa mabao 3-1 katika mechi ya mwisho ya ligi msimu uliopita, kisha kuishinda kwa penalti katika nusu fainali ya Ngao ya Jamii iliyopigwa Mkwakwani, Tanga, Agosti 10, mwaka huu baada ya dakika 90 kuisha kwa suluhu na hivyo mchezo wa leo utakuwa nafasi ya kufuta unyonge huo.

Katika mechi ya ligi msimu uliopita iliyopigwa Uwanja wa Liti, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, Simba ikichomoa bao la Deus Kaseke kupitia kwa Peter Banda ambaye kwa sasa hayupo kwa Wekundu hao, lakini kiu kubwa ni ya mashabiki wa timu zote kutaka kuona wimbi la ushindi na mpira mwingi unapigwa jioni.

Singida iliyokosa utulivu kwenye benchi baada ya kumtimua Hans Pluijm aliyeiongoza kutoka suluhu mechi mbili za awali za ligi, kisha kukimbiwa na kocha wake Ernst Middendorp, kwa sasa ipo chini ya mkurugenzi wa Ufundi, Ramadhan Nsanzurimo akisaidiwa na Thabo Senong huku ikielezwa Mathias Lule naye akiwa kwa mbali anasaidiana na makocha hao.

Bila shaka benchi hilo litataka kupata ushindi wa kwanza wa timu hiyo mbele ya Simba na pia kukusanya pointi tatu ili kujiweka pazuri kwenye msimamo, ilhali Simba itataka kuendelea soka tamu la mabao mengi kama ilivyofanywa jijini Mbeya na ushindi wa leo utawarejesha tena kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.

Singida inajua Simba haina shoo nyepesi, hivyo ni lazima ijipange kama ambavyo wageni wao watakavyojipanga wakiwa na nia ya kuendeleza vaibu lao la ushindi ikiwa ndio timu pekee hadi sasa kwa msimu huu katika ligi ambayo haijadondosha pointi hata moja.

Kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alisema, japo hawajapata muda wa kutosha kujiandaa na mchezo huo, lakini wanaingia kwenye mchezo huo wakitaka kuendeleza ubora wao kwa kucheza bila presha lakini wakiwa na mipango ya kutengenza matokeo.

“Hii ni mechi ya pili msimu huu tunakutana na Singida, ni timu kubwa ina wachezaji bora, itakuwa ni mechi ngumu lakini tunahitaji ushindi, hatujapata muda wa kutosha kujindaa na hii mechi tutamia falsafa yetu kutengeneza ushindi mwingine muhimu, “alisema Robertinho, wakati wenyeji kupitia Senong walikiri kwamba mechi ni ngumu, lakini wanataka ushindi wa kwanza nyumbani.

”Tunakwenda kukutana na Simba, hizi ni aina ya mechi zinazoamuliwa na wachezaji pengine kuliko hata makocha,” alisema Senong.

“Kwa kuwa wachezaji wanajuana vizuri, na kwa bahati timu zote wachezaji wameandaliwa vizuri, hivyo tunatarajia mchezo mzuri wenye kuburudisha na kiwango bora, lakini kubwa ni kupata matokeo tukiwa nyumbani.”

Kwenye Uwanja wa Sokoine, wakongwe wa Ligi Kuu Bara, Mtibwa Sugar na Tanzania Prisons zitakuwa na kazi ya kutunishiana vifua ili kupata ushindi wa kwanza huku zikitenganishwa kwa tofauti na pointi moja katika msimamo wa michuano hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: