Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mitazamo tofauti Manula vs Al Ahly

Aishi Manula Back.jpeg Mitazamo tofauti Manula vs Al Ahly

Mon, 16 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baada ya kukaa nje ya uwanja kwa takribani miezi sita akiuguza majeraha ya nyonga, kipa Aishi Manula juzi Jumamosi kwa mara ya kwanza alirejea uwanjani huku kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akisema atakuwa tayari kuwakabili Al Ahly, kauli ambayo imezaa mitazamo tofauti.

Manula alianzishwa katika kikosi cha Simba kilichoshinda 5-1 dhidi ya Dar City katika mechi yao ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mo Arena na alitumika kwa dakika 40 kabla ya kumpisha Hussein Abel.

Kocha Mbrazili, Robertinho, alisema benchi lake la ufundi limeridhishwa na kiwango cha Manula na moja kwa moja anaingia kwenye mipango ya mechi yao ya michuano mipya ya African Football League (AFL) dhidi ya Al Ahly itakayopigwa Ijumaa hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

“Kila kocha anatamani kuwa na wachezaji wake wote kikosini, tumefurahi kumuona Manula akirejea pia ameonyesha kiwango bora,” alisema Robertinho na kuongeza;

“Amerejea wakati tukijiandaa na mechi ya Al Ahly, ni mchezaji mzoefu na tayari tumemjumuisha kwenye mipango ya mechi hiyo kama ilivyo kwa wengine. Ni wakati wake kuitumikia klabu.”

Kurejea kwa Manula ambaye alipata majeraha ya nyonga Julai 7 mwaka huu, kumeibua mitazamo tofauti kutoka kwa wadau wa soka wengine wakiamini ataisaidia safu ya ulinzi hali ya kujiamini, wengine wakiona bado atakosa utimamu wa kucheza mechi.

Kipa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Ivo Mapunda alisema kurejea kwa Manula kutaongeza kitu kwenye eneo la ulinzi la Simba.

“Manula ni mzoefu kwenye mechi za kimataifa, kama atakuwa fiti ataisaidia sana Simba kwani ana ubora mkubwa katika eneo hilo na amethibitisha kwa muda mrefu,” alisema Mapunda ambaye kwa sasa ni kocha wa makipa wa Biashara United inayoshiriki Championship.

Kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema hana hakika kama Manula atakuwa tayari kwa mechi kubwa kiasi hicho.

“Manula ni mkongwe pale Simba, pia ni mzoefu na mechi ngumu, sidhani kama atakuwa na game fitness (utimamu wa mechi) kwa kiwango kikubwa, lakini bechi la ufundi ndilo litaamua kumpanga,” alisema Julio na kuongeza;

“Hata asipodaka Manula, wale makipa wengine waliopo Simba wanaweza kudaka na kufanya vizuri, hakuna kipa asiyefungwa duniani hivyo Simba inachotakiwa kufanya ni kucheza kwa tahadhari na kupunguza makosa kwenye kila eneo.”

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: