Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miquissone ahamishwa nyumba, apewa kocha spesho kuiua Al Ahly

Luis Miquissone Miquissone ahamishwa nyumba, apewa kocha spesho kuiua Al Ahly

Thu, 28 Sep 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba inajiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Power Dynamos, Jumapili, lakini Mwanaspoti linajua timu hiyo imemfanyia kufuru kiungo wake Luis Miquissone na kama mambo yakienda vizuri atawafurahisha.

Mwanaspoti linajua staa huyo ambaye ameanza kunoga kikosini amepewa ndinga kali ya kisasa yenye hadhi yake, amehamishwa nyumba aliyokuwa amefikia pamoja na kukabidhiwa kwa mtaalamu spesho wa viungo kumnoa.

Ikumbukwe kiungo huyo alijiunga na Simba akitokea Al Ahly ambako hakupata nafasi ya kucheza kwa muda na kutua Simba ikiwa tayari imemaliza maandalizi ya msimu, hivyo anapambana kujitafuta ili awe fiti kabla ya kuvaana na Waarabu hao kwenye michuano mipya ya Super Cup, Oktoba 20 na kurudiana wiki mbili baadaye.

Luis aliondoka nchini msimu wa 2020/21, lakini baada ya kurejea Msimbazi kocha Oliveira Roberto ‘Robertinho’ alibaini huyo hayupo fiti akampa muda wa kujitafuta huku akimpa dakika chache za kucheza ili kumuingiza kwenye kikosi chake.

Hata hivyo, akiwa na programu maalumu ya kupunguza uzito ambapo amefanikiwa kupungua kilo nne, alikuwa anafanya mazoezi pamoja na timu na katika mechi iliyopita ya ligi ambayo Simba ilishinda mabao 3-0 mbele ya Coastal Union alicheza dakika 90 na kuonyesha kiwango bora ambapo kocha wake alisema kuwa ameanza kuwa fiti.

Mwanaspoti limezipata za ndani kutoka Simba kuwa uongozi umeamua kumsuka Luis wa misimu miwili nyuma baada ya kumtafutia mtaalamu wa viungo ili aendelee kumuweka fiti zaidi ya alipofikia sasa.

Habari zinasema kwamba pamoja na mechi zingine za mashindano, lakini Simba wanataka mpaka ikifika mechi na Ahly jijini Dar es Salaam, Luis awe kwenye fomu kuongeza nguvu kikosini kwani michuano hiyo ina pesa nyingi na inaweza kuwapa heshima kubwa zaidi Afrika.

Kwa mujibu wa Rais wa TFF, Wallace Karia, CAF imeamua mechi ya Simba iwe kama ya kukata utepe wa mashindano hayo kutokana na mwamko wa soka na mashabiki wa Tanzania.

Habari zinasema kwamba Simba wamepania kuonyesha ukubwa na utofauti na mtani wao, Yanga, kupitia mashindano hayo kwani tayari watani hao wote wako kwenye uwezekano mkubwa wa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Habari za uhakika zinasema kwamba tayari Luis yuko na mtaalamu huyo mwenye uzoefu mkubwa jijini Dar es Salaam na mbali na kufanya naye programu za kawaida kwenye timu huenda mbali zaidi baada ya muda wa kawaida na atakuwa naye mpaka wiki ya tatu ya Oktoba.

Za ndani ambazo Mwanaspoti limezipata ndani ya uongozi ni kwamba mbali na malengo ya timu na viongozi, Luis binafsi amepania kufanya makubwa katika mchezo huo kama ilivyokuwa awali walivyomuona wakamnunua kwa fedha nyingi na kwenda kumuweka benchi.

Kuhusu gari, Mwanaspoti limejiridhisha kwamba Luis amekabidhiwa ndinga ya kisasa aina ya Crown New Model ya mwaka 2023 ambayo inakadiriwa thamani yake ni zaidi ya Sh100 milioni na tayari juzi na jana ameonekana nayo kwenye matizi kule Bunju.

Mbali na ndinga amehamishiwa kwenye nyumba ya kifahari maeneo ya Mbezi Beach Africana jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya mkataba wa pande zote na vilevile kuhakikisha anatuliza akili uwanjani na kurejesha makali yake kwa klabu msimu huu.

Luis ambaye ni raia wa Msumbiji, mwenyewe alikiri hivi karibuni ni kuwa amepungua kilo nne na imekuwa hivyo baada ya kufanya mazoezi kwa nguvu ili aweze kurudi kwenye ubora wa kuipa matokeo timu.

“Kila kitu kinakwenda na muda sasa mambo yanaenda taratibu kutoka dakika 45, nimecheza dakika 90 mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya Coastal Union.

“Naona kuna mabadiliko makubwa kwangu japo bado naendelea kupambana ili kujiweka fiti zaidi. Nafikiri mashabiki wawe na subiri tu mambo yatakuwa safi,” alisema staa huyo ambaye timu yake inakabiliwa na mechi dhidi ya Tanzania Prisons Oktoba 3.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: