Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa Simba wapishana angani

Simba Vs Mashujaa.jpeg Mastaa Simba wapishana angani

Sat, 23 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha ameendelea kuwapa dozi za maana wachezaji wa timu hiyo ambao hawakuitwa katika timu za taifa ili kujiandaa kwa ajili ya mechi ijayo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, huku mastaa waliopo timu za taifa wameanza kupishana angani kuiwahi kambi hiyo iliyopo Zanzibar.

Simba imejichimbia visiwani humo kujiandaa na mechi ya kwanza ya hatua hiyo ya robo dhidi ya Al Ahly itakayopigwa Ijumaa ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kurudiana Aprili 5 jijini Cairo, Misri na mshindi wa jumla atatinga nusu fainali na kuvaana na kati ya Esperance ya Tunisia au Petro Atletico ya Angola.

Uamuzi wa timu hiyo kuweka kambi Zanzibar ni ombi la Benchikha aliyetaka kupata kambi yenye utulivu ili kuwapa mastaa wake madini yatayowawezesha kuizimisha Al Ahly.

Ipo hivi. Mastaa waliokuwa timu za taifa kuzitumikia kwenye mechi za kimataifa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), waliombewa ruhusa na kwamba baadhi yao wapo njiani ili kuwahi kambi hiyo ya Zanzibar kujipanga mapema kwa ajili ya mechi ya Ijumaa itakayopigwa Dar es Salaam.

Kabla ya Jumatatu asilimia kubwa ya wachezaji wa Simba waliokuwa katika timu za Tanzania, Zambia na Burundi na wamepata ruhusa ya kurejea nchini.

Kipa Aishi Manula, nahodha Msaidizi Mohamed wa Wekundu hao, Hussein ‘Tshabalala’, mshambuliaji Kibu Denis na beki Kennedy Juma waliokuwa na Stars iliyokuwa uwanjani jioni ya jana kucheza na Bulgaria huko Baku, Azerbaijan pamoja na viungo tegemeo Clatous Chama wa Zambia na Saidi Ntibanzokiza ‘Saido’ wa Burundi ndio waliokuwa wanakosekana kambini Zanzibar.

Hata hivyo, wachezaji hao leo wanaanza safari kuja nchini kuongeza nguvu katika kambi ya Simba, nyota wa nne wa Stars wanaanza safari kurejea, hivyo kuikosa mechi ya pili ya Taifa Stars na Mongolia itakayopigwa keshokutwa Jumatatu.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo alithibitisha: “Ni kweli klabu iliomba wachezaji wao kupewa ruhusa mapema na baadhi yao wataruhusiwa kujiunga na klabu haraka.”

Saido yupo Madagascar akiwa na timu ya taifa ya Burundi ambayo jana ilicheza mechi na wenyeji wao hao na Jumatatu pia ina mchezo mwingine nchini dhidi ya Botswana, lakini kiungo huyo ameliambia Mwanaspoti atawawahi Waarabu jijini Dar.

“Nimeombewa ruhusa na klabu. Nadhani nitarejea mapema na nitawahi maandalizi ya mwisho ya timu kabla ya mechi,” alisema Saido mwenye mabao saba na asisti mbili katika Ligi Kuu Bara hadi sasa.

Kwa upande wa Chama, yupo Malawi akiwa na kikosi cha Zambia kitakachocheza leo jioni dhidi ya majirani zao wa Zimbabwe na baada ya hapo anapanda ndege hadi nchini na kesho au keshokutwa atajiunga na timu kambini zikiwa zimesalia siku kama nne kabla ya mechi ya CAF.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema wanatarajia kuwa na kikosi kizima siku mbili hadi tatu kabla ya mechi.

“Timu inaendelea vizuri na mazoezi na tunatarajia kikosi kizima wakiwemo wachezaji waliokwenye majukumu ya timu za taifa, siku mbili hadi tatu kabla ya mechi,” alisema Ahmed na kuongeza:

“Tunahitaji ushindi katika mechi ya nyumbani ili kutanguliza mguu mmoja mbele kwenye nusu fainali. Tunajua ugumu wa Al Ahly, lakini wanatutambua kwani tumewafunga sana. Sasa tunataka kuthibitisha ubabe wetu kwa kuwaondosha tukianza kwa kuwafunga nyumbani. Tunaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi tuandike rekodi pale kwa Mkapa.”

Hii itakuwa ni mara ya nne kwa timu hizo kukutana katika mechi za CAF kwani zilishapangwa mara mbili katika makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kila mmoja alishinda mechi mbili za nyumbani na kupoteza ugenini kabla ya mwaka jana kuvaana tena kwenye michuano mipya ya African Football League.

Katika mechi hizo mbili za hatua hiyo ya robo faionali, zilishindwa kutambiana kwa kutoka sare ya 2-2 jijini Dar es Salaam kisha 1-1 Cairo, Misri na Al Ahly kubebwa na faida ya mabao ya ugenini ikiing’oa Simba hatua hiyo na kutinga nusu fainali ilipoenda kutolewa na walioibuka mabingwa, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini iliyowachapa Wydad CA ya Morocco katika michezo ya fainali.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: