Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mastaa Simba waapa kufa na Mwarabu

Simba Vs Mashujaa.jpeg Mastaa Simba waapa kufa na Mwarabu

Mon, 25 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kikosi cha Simba kinaendelea kujifua kambini Zanzibar huku, kikiendelea kuwapokea wachezaji waliokuwa timu za taifa, ilio kujiwinda na mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri, huku mastaa waliopo kambini wakipa lazima wapige tena mtu Kwa Mkapa.

Simba itakuwa wenyeji wa mchezo huo utakaopigwa Ijumaa hii kuanzia saa 3:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kabla ya kurudiana Aprili 5, jijini Cairo na mshindi atafuzu nusu fainali kusubiri mshindi wa mechi nyingine ya robo fainali kati ya TP Mazembe ya DR Congo na Petro Atletico ya Angola.

Wakiwa na mzuka mwingi wa kutaka kuvunja mwiko wa kushindwa kuvuka hatua ya robo fainali tangu mwaka 2018, Simba ikiwa imecheza hatua hiyo mara tano kati ya misimu sita iliporejea kwenye michuano ya kimataifa haijawahi kuvuka na mastaa wa timu hiyo wamekula kiapo cha kutaka kuivusha timu kibabe.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwanaspoti, mastaa hao wa Simba wamekiri watarajia mchezo mgumu mbeloe ya watetezi hao wa CAF, lakini kwa namna walivyojiandaa wanatarajia kufanya mambo makubwa wakitaka kufuta unyonge wa kushindwa kuvuka hatua hiyo kwenda nusu fainali.

Kipa Ally Salimu alisema matarajio kuelekea mchezo huo ni makubwa na maandalizi yao yanakwenda vizuri wanaahidi kupambana kuhakikisha wanapata matokeo huku akikiri kuwa hii wao kama timu wana utayari.

“Tumecheza robo fainali nne sasa ni ya tano tumezazoea na hii dhidi ya Al Ahly kwa kiasi kikubwa tuna utayari kulingana na maandalizi tuliyoyafanya sambamba na ubora wa kikosi til icho nacho,” alisema Ally aliyecheza mechi zote mbili za Simba na Al Ahly za AFL aliyeongeza;

“Kwenye hatua hizo zote nne kila msimu tulikuwa na uimara na mabadiliko kwenye kila mchezo lakini kwangu robo fainali ngumu kuwahi kucheza ni dhidi ya Kaizer Chiefs licha ya kuanzia ugenini tukijiamini tukakutana na ugumu na kuruhusu mabao mengi kitu ambacho kikatukwamisha kusonga mbele kwani nyumbani licha ya kushinda idadi ya mabao tuliyofungwa ilituangisha.”

Salim alisema msimu huu hawana cha kupoteza wanakutana na timu ambayo wanaifahamu ubora wao na mapungufu yao na hivi karibuni wamecheza nayo na ndio maana baada ya droo kupangwa walikuwa na furaha lakini hawatarajii mteremko.

Kiungo mshambuliaji, Willy Onana, alisema huu ndio wakati muhimu kwa timu yake kwenda kuandika historia mpya Afrika kwa kutinga nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu michuano hiyo ilipobadilishwa mfumo na jina kutoka Klabu Bingwa, ambapo Simba ilicheza hatua hiyo ikiwa ni rekodi mwaka 1974.

Onana mwenye mabao mawili, alisema anajua wanaenda kupambana na bingwa mtetezi hautakuwa mchezo rahisi kwao lakini ndio wakati wa kwenda kuonyesha ubora wao kwa kutimiza malengo yao ya muda mrefu.

“Binafsi najisikia vizuri kucheza robo fainali kwa mara ya kwanza Al Ahly ni kama Real Madrid kwa Afrika inaweza kuwa kwenye kipindi cha mpito lakini kwenye michuano ya ligi ya mabingwa wanakuja kivingine," alisema Onana na kuongeza;

“Tunatambua tunaenda kucheza na timu kubwa sana barani Afrika hii ni nyakati bora kwa wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi kuandika historia mpya.”

Alisema kama kuna aliyekuwa akiingalia Simba ikiishia hatua ya robo fainali abadilishe mtazamo kwa kuwa huu ni wakati wa kwenda kubadili hii historia ambayo kwa muda mrefu imekuwa.

“Sijui mipango ya mwalimu kwenye mchezo huo lakini mimi binafsi niko tayari kwa ajili ya mechi hii kubwa ambayo itatazamwa na watu wengi barani Afrika,” alisema Onana.

Mshambuliaji Pa Omary Jobe amewaita mashabiki kujitokeza kwa wingi kuwapa sapoti kuelekea mchezo huo huku akisisitiza kuwa wamejiandaa kufanya vizuri na kupata matokeo mazuri ambayo yatatoa picha ya wao kufikia malengo.

“Ijumaa tunacheza na timu bora Afrika tumekiandaa vizuri kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kwenye uwanja wetu wa nyumbani ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua inayofuata,” alisema Pa Jobe.

Licha ya wachezaji hao kula kiapo, lakini Simba inapaswa ijipange kwelikweli mbele ya Al Ahly kwani rekodi zinaonyesha katika misimu mitano mfululizo iliyopita ilipotinga robo fainali ni mara moja tu ilikwama, lakini nyingine zote ilifika hadi fainali na ikabeba mataji mara tatu na kupoteza moja tu.

Pia katika mechi sita baina ya timu hizo, hakuna timu iliyowahi kupata ushindi ugenini dhidi ya mwenzake, kwani mara ya kwanza kukutana msimu wa 2018-2019 Al Ahly ilishinda nyumbani mabao 5-0 kisha ikaenda kupoteza ugenini kwa bao 1-0 na zilipokutana tena 2020-2021 ikiwa pia ni makundi, kila moja ilishinda nyumbani bao 1-0 na katika mechi za African Football League (AFL) ziliishia kutoka sare ya 2-2 jijini Dar es Salaam na 1-1 kule Cairo na Al Ahly ikavuka kwa faida ya bao la ugenini.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: