Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashabiki 700 Simba Mbeya, Songwe kuliamsha Kwa Mkapa

Mashabiki Simba Mbeya Mashabiki 700 Simba Mbeya, Songwe kuliamsha Kwa Mkapa

Wed, 18 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Hii sasa sifa. Ndivyo unaweza kusema kuelezea mzuka wa mashabiki wa Simba zaidi ya 700 kutoka Mikoa ya Mbeya na Songwe watakavyoliamsha Uwanja wa Benjamin Mkapa, wakati timu hiyo ikiwakabili Al Ahly ya Misri kwenye mechi ya kwanza ya michuano mipya ya African Football League (AFL).

Simba inatarajia kushuka uwanjani katika mchezo utakaopigwa Ijumaa Kwa Mkapa, jijini Dar es Salaam ukiwa ni wa kwanza katika michuano hiyo.

Hata hivyo, timu hizo zinakutana ikiwa Wekundu wanajivunia rekodi ya ushindi wa bao 1-0, walipokutana mara ya mwisho katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, bao likifungwa na Luis Miquissone.

Mashabiki hao wameanza safari leo Jumatano, ambapo kwa Mkoa wa Mbeya ni watu 660 wakiwa katika mabasi 22, huku tawi la Tunduma mkoani Songwe wakiwa ni 70 waliosafiri kwenye mabasi mawili.

Mwenyekiti wa Simba mkoani Mbeya, Edson Abel amesema mchezo huo wanauweka 'level' ya dunia kutokana na ukubwa wake na viongozi watakaoufuatilia.

Kuhusu kuwahi mapema, amesema wameamua kufanya hivyo ili kuweka mazingira mazuri ya ndani na nje ya uwanja kuhakikisha Simba inashinda kwa idadi kubwa ya mabao ili mchezo wa marudio uwe mwepesi ili kufuzu hatua inayofuata.

"Mabasi ni 22 ambayo kila moja ina uwezo wa kubeba abiria 30, tumeona tuwahi ili kuweka mipango mizuri ya ushindi wa mabao mengi, huu ni mchezo mkubwa na wa kidunia"

"Utasemaje ni ndondo wakati kuna viongozi wa dunia tena Rais wa FIFA (Shirikisho la soka duniani) Gianni Infantino lazima tuweke heshima na historia dunia iifahamu Simba," ametamba Abel.

Kwa upande wa katibu wa timu hiyo tawi la Tunduma, Danny Mgavilwa amesema jumla ya mashabiki 70 tayari wameanza safari kuelekea Dar es Salaam kuisapoti Simba akielezea kuwa matarajio yao ni ushindi.

"Tulishawafunga hao Waarabu, lakini mchezo wa Ijumaa utakuwa na heshima yake tunataka ushindi mnono na matarajio yetu ni kupata raha tunaamini benchi la ufundi litafanya kazi yake na vijana watatekeleza," amesema Mgavilwa.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: