Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo yazidi kuvurugika Simba, Mo agoma kutoa pesa za usajili mpaka..!

MO DEWJI 5?fit=1080%2C720&ssl=1 Mambo yazidi kuvurugika Simba, Mo agoma kutoa pesa za usajili mpaka..!

Wed, 12 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tajiri amemwaga mboga. Mwekezaji wa klabu ya Simba, Mohammed Dewji amesitisha kutoa fedha za usajili na huduma nyingine kwa timu hadi pale wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo watakapojiuzulu, Mwanaspoti limeambiwa.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti limezipata kutoka kwa chanzo cha kuaminika ndani ya Simba ni kuwa uamuzi huo wa MO utaenda sambamba na kuanika kwa umma namna bodi ya Simba ilivyochangia kuiangusha klabu hiyo msimu uliomalizika.

Chanzo hicho kimefichua kuwa Dewji ameamua kuchukua uamuzi huo mgumu baada ya kuona muda alioutoa kwa wajumbe hao kujiuzulu umepita huku wengi hasa wale wa upande wa wanachama wakigoma kufanya hivyo.

“Mwekezaji hajafurahishwa na ufanisi wa bodi katika msimu uliomalizika ambao anaamini ulikuwa duni na umechangia kwa kiasi kikubwa timu kufanya vibaya kwenye ligi ambapo imemaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo.

“Mwekezaji anaamini kuna matumizi mabaya kwenye timu hasa kwenye upande wa usajili ambao umekuwa haufanyiki kitaalam kwa kuzingatia mahitaji ya benchi la ufundi lakini pia kumekuwa hakuna uwazi katika uendeshaji wa masuala ya klabu ambapo kuna kikundi cha watu wachache tu ambao ndio kinafanya maamuzi yaliyopaswa kufanywa na wengi,” kilifichua chanzo hicho.

Mwanaspoti lilifichua sababu tatu zilizomshawishi Dewji kulazimisha wajumbe wa bodi kutoka upande kujiuzulu ambapo wanne walijiweka kando huku mmoja ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ akigoma kufanya hivyo.

Sababu hizo ni usajili wa wachezaji wenye viwango vya chini, matokeo mabaya kwa timu pamoja na kusuasua kukamilika kwa mchakato wa uwekezaji ndano ya timu hiyo.

Deni kubwa lamshtua MO; Mwanaspoti limefahamishwa kuwa miongoni mwa mambo yaliyomshtua MO na kupelekea afanye uchunguzi uliomfanya awashinikize wajumbe wa bodi kujiuzulu ni deni kubwa la fedha ambalo klabu hiyo inalo bila kuwepo na mchanganuo unaoeleweka wa sababu za uwepo wake.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, deni hilo ambalo Simba inalo kwa sasa linakadiriwa kufikia Shilingi 4 bilioni “Timu kwa sasa ina deni linalofikia shilingi bilioni nne na mwekezaji alipotaka kufahamu sababu za hilo deni, uongozi umeshindwa kutoa majibu yanayoeleweka jambo linalomfanya muwekezaji aamini kwamba viongozi waliopo kuna namna wanafanya matumizi yasiyo sahihi.”

“Na kinachomshangaza zaidi mwekezaji ni kwamba klabu ilikuwa katika nafasi nzuri kifedha katika msimu uliopita ambazo zilitokana na udhamini na zawadi za ushiriki kwenye mashindano mbalimbali,” kilibainisha chanzo hicho.

Mwanaspoti linafahamu kuwa hasira ya MO hadi kufikia uamuzi wa kutotoa fedha ya usajili zimechochewa zaidi na uwepo wa mpango wa mmoja wa viongozi wa juu wa klabu hiyo kutumia baadhi ya waandishi wa habari, wachambuzi wa soka na watu wenye ushawishi mkubwa kumchafua Dewji.

“Dewji anao ushahidi wa kampeni inayoendelea mitandaoni na kwenye baadhi ya vyombo vya habari za kumchafua na kupindisha ukweli wa hili jambo ambayo inaratibiwa na kiongozi mmoja ndani ya Simba hivyo ndio maana naye ameamua kumwaga mboga,” kilisisitiza chanzo hicho.

BODI INA KINANI?

Inaundwa na watu 10 kutoka pande mbili kwa Wanachama na Muwekezaji. Upande wa Mo,aliteua wajumbe watano ambao ni Try Again ambaye ni mwenyekiti wa bodi hiyo na Raphael Chageni, Hamza Johari, Zulfikar Chandoo na Rashid Shangazi ndio wamejiuzulu.

Mbunge wa Mlale, Rashid Shangazi ambaye ni mmoja wa wajumbe wa upande wa muwekezaji huyo waliojiuzulu, alisema wameamua kufanya hivyo ili kumpa nafasi Dewji kuingiza sura mpya.

Pamoja na kwamba Dewji aliwateua mwenyewe wajumbe hao, uamuzi wa kuwaomba wajiuzulu ameuchukua ili kutokiuka katiba ya klabu hiyo ambayo inafafanua kuwa mjumbe wa bodi atakoma kutumikia nafasi yake ikiwa mambo manne yatatokea.

“Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi aliyechaguliwa na kuteuliwa kwa mujibu wa ibara ya 27 ya katiba hii atakoma kuwa mjumbe wa bodi ya wakurugenzi iwapo atatenda au kufanya mojawapo ya mambo yafuatayo.

(a) Kujiuzulu kwa maandishi na kuwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa bodi ya wakurugenzi. (b) Hatohudhuria mikutano minne mfululizo ya kawaida ya bodi ya wakurugenzi. (c) Anashindwa kutekeleza majukumu ya mjumbe kutokana na kuumwa au sababu nyingine yoyote kwa kipindi cha miezi 12 mfululizo,” inafafanua ibara ya 29 ya katiba hiyo.

UPANDE WA WANACHAMA ITAKUWAJE?

Presha hiyo ya kujiuzulu inawakabili pia wajumbe wa bodi ya wakurugenzi akiwemo Mwenyekiti, Murtaza Mangungu ambao hawakuteuliwa na Dewji lakini kutokana na kutokuwa na mamlaka ya kikatiba.

Upande huu wanachama walikuwa Seif Muba, Asha Baraka, Issa Masoud, Rodney Chiduo na Seleman Haroub na Mangungu. Wote hao mpaka jana walikuwa wamesisitiza kutojiuzulu ingawa Muwekezaji anataka wote wakae pembeni aanze upya.

Licha ya kwamba amesitisha kutoa mzigo wa kusajili lakini Mwanaspoti linajua MO ameshawaongeza watu wanne wazoefu wa masuala ya usajili kusimamia zoezi hilo litakapoanza rasmi ambao ni Crecensius Magori, Mulamu Nghambi, Kassim Dewji na Sued Mkwabi.

Mwanaspoti linajua pia Barbara Gonzales atarudishwa kama Mwenyekiti wa Bodi. Inaelezwa inasubiriwa Try Again ajiuzulu kisha Barbara akaimu nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na hapo baadae atapigiwa kura na wajumbe kuidhinishwa.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: