Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo 10 usiyoyajua mechi za mwanzo Ligi Kuu 2023/24

Simba Players Chama Mambo 10 usiyoyajua mechi za mwanzo Ligi Kuu 2023/24

Tue, 22 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2023/24, ilianza Jumanne iliyopita kwa timu kadhaa kuanza mbio za kulisaka taji ya ubingwa.

Kama ilivyotarajiwa ligi imeanza kwa kishindo, ugumu na matokeo yaliyotarajiwa na yasiyotarajiwa pia huku timu nyingi zikionekana kujizatiti kisawasawa.

Katika makala haya tumekusanya taarifa, takwimu na rekodi za mechi za ufunguzi wa Ligi Kuu na moja ya raundi ya pili iliyochezwa juzi kati ya Namungo na KMC.

Takwimu na rekodi hizi zimewekwa na wachezaji pamoja na timu zenyewe za Ligi Kuu, twende sasa...

#1. Simba haijapoteza misimu 16

Ushindi wa mabao 4-2 dhidi ya Mtibwa Sugar, unaifanya Simba kutopoteza mechi yoyote ya ufunguzi kwa misimu 16 mfululizo. Mara ya mwisho ilipoteza msimu wa 2007/08 ilipochapwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga dhidi ya Coastal Union ambalo liliwekwa wavuni dakika ya 44 na Sunday Peter.

Katika mechi hizo, Simba imeshinda 13 na kutoka sare tatu. Ulikuwa msimu wa 2013/14 ikitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Rhino Ranger, uliofuata ilitoka sare kwa mara nyingine tena ya mabao 2-2 dhidi ya Coastal Union na msimu wa 2021/22 ilisuluhu dhidi ya Biashara United.

#2. Yashindwa kuweka rekodi ya 2017/18

Pamoja na kushinda idadi hiyo ya mabao, Simba imeshindwa kuweka rekodi iliyoiweka msimu wa 2017/18 ilipoichakaza Ruvu Shooting mabao 7-0 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Emmanuel Okwi akipachika manne, Shiza Kichuya, Juma Luzio na Erasto Nyoni wakifunga bao moja kila mmoja.

Mara ya mwisho timu hiyo kufunga mabao manne kwenye mechi ya ufunguzi kama ilivyofanya dhidi ya Mtibwa Sugar ilikuwa msimu wa 2008/09 ilipoiadhibu Villa Squad mabao 4-1, mawili yakifungwa na Mnigeria Emeh Izuchukwu, Mussa Hassan Mgosi na Ramadhani Chombo 'Redondo', wakifunga bao moja kila mmoja.

#3. Mapro watawala ufungaji

Kwa misimu miwili mfululizo, mabao yote ya mechi zake za kwanza yanafungwa na wachezaji wa kigeni.

Msimu uliopita ilipoifunga Geita Gold mabao 3-0 kwenye mechi ya ufunguzi, mabao yalifungwa na Wazambia Clatous Chama na Moses Phiri, lingine likiwekwa kwenye kamba na Mghana ambaye kwa sasa hayupo kwenye kikosi, Augustine Okrah.

Msimu huu yamefungwa na Wakongomani Jean Baleke na Fabrice Ngoma, Mzambia Chama akiingia tena kwenye rekodi ya kuwa katika orodha ya wafungaji wa mabao ya raundi ya kwanza pamoja na Mcameroon, Willy Onana.

Mara ya mwisho Wabongo kufunga mabao kwenye mechi ya ufunguzi kwa timu hiyo ilikuwa msimu wa 2020/21 ilipoifunga Ihefu 2-1, yakitumbukiwa nyavuni na John Bocco na Mzamiru Yassin.

#4. Azam haijapoteza tangu 2009

Azam FC ilianza Ligi Kuu msimu huu kwa ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kitayosce Jumatano iliyopita katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, ikiweka rekodi ya kutopoteza mechi yoyote ya ufunguzi kwa misimu 14.

Katika mechi hizo, imeshinda 10 na minne ikitoka sare msimu wa 2013/14 ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, 2016/17 sare tena ya bao 1-1 dhidi ya African Lyon, suluhu dhidi ya Simba msimu wa 2017/18 na 2021/22 dhidi ya Coastal Union sare ya bao 1-1.

Azam haijapoteza mechi yoyote ya kwanza tangu ilipofungwa mabao 3-2 mechi ya ufunguzi Agosti 23, 2009, msimu wa 2009/10 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, mkoani Kagera. Yalikuwa ni mabao ya Paul Kabange, Michael Katende na Themi Felix, John Bocco akiifungia Azam mabao mawili.

#5. Dube kama Chama

Wakati Chama wa Simba akifunga bao kwenye mechi ya kwanza kwa misimu miwili mfululizo, Prince Dube ameweka kama hiyo. Dube amefunga bao moja katika mechi ya ufunguzi dhidi ya Kitayosce msimu huu, alifanya hivyo pia msimu uliopita, Azam ikiichapa Kagera Sugar mabao 2-1, lingine likifungwa na Tepsi Evance, Anuary Jabir akiifungia timu yake bao la kufutia machozi.

#6. Fei Toto aweka rekodi ya 'hat-trick'

Kiungo wa Azam FC, Feisal Salum, ameweka rekodi ya kufunga mabao matatu 'hat-trick' ndani ya dakika 13 tu katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu yake dhidi ya Kitayosce, timu yake ikishinda 4-0. Ilikuwa ni hat-trick ya kwanza msimu huu kwenye mechi ya kwanza pia ya Ligi Kuu.

Ni hat-trick ya mapema zaidi kwenye historia ya Ligi Kuu, akivunja rekodi iliyowekwa ya straika wa Simba, Jean Baleke, aliyoiweka msimu uliopita, Machi 11, mwaka huu, kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Turiani, Morogoro ilipocheza dhidi ya Mtibwa Sugar timu yake ikishinda mabao 3-0. Baleke alifunga dakika ya tatu, saba na 34, wakati Fei Toto alifunga dakika ya tatu, tisa na 13.

#7. Ihefu kama msimu uliopita

Ihefu ilianza mechi ya kwanza nyumbani kama ilivyokuwa msimu uliopita na ikapoteza kwa bao 1-0 kwa mara nyingine tena, tarehe ikiwa ile ile na uwanja ule ule, Highland Estates, Mbarali.

Jumanne iliyopita, Agosti 15 ilifungwa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold, likiwekwa wavuni na Elius Maguri. Ilikuwa kama 'kukopi' na 'kupesti' kwa matokeo ya ufunguzi msimu uliopita ilipodunguliwa bao 1-0, Agosti 15, mwaka jana likiwekwa wavuni na Ally Bilal.

#8. Kagera yapoteza mbili tena

Kama msimu uliopita, timu ya Kagera Sugar imepoteza mechi mbili za kwanza msimu huu.

Ilianza kupoteza Jumatano iliyopita ugenini dhidi ya Mashujaa FC kwa mabao 2-0, kabla ya Jumamosi kufunga bao 1-0 dhidi ya Uhefu FC.

Imerudia rekodi mbaya ya msimu uliopita ilipopoteza mechi ya ufunguzi kwa kulala mabao 2-1 dhidi ya Azam FC, kabla ya kubamizwa 2-0 dhidi ya Simba.

#9. Namungo sare misimu miwili

Tangu iliposhinda mabao 2-0 msimu wa 2021/22, timu ya Namungo haijashinda mechi yoyote ya ufunguzi kwa misimu miwili mfululizo, badala yake imetoka sare zote.

Juzi ililazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya KMC Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi ikirudia ilichokifanya mechi ya ufunguzi msimu uliopita ilipotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Mtibwa Sugar, Septemba 27, 2021, Ligi Kuu msimu wa 2021/22.

#10. Mashujaa kama Singida FG

Ushindi wa mabao 2-0 ilioupata Mashujaa FC dhidi ya Kagera Sugar Jumanne iliyopita, umeweka rekodi ya misimu miwili mfululizo kwa timu moja inayopanda daraja kushinda mechi ya ufunguzi.

Msimu uliopita, Singida Fountain Gate ilikuwa timu pekee iliyopanda daraja kushinda mechi ya ufunguzi kwa kuifunga Prisons bao 1-0, Agosti 16, mwaka jana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: