Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makipa waliopata vichapo vikali

Manula X Cadena Makipa waliopata vichapo vikali

Wed, 29 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kipa kufungwa mabao mengi inawezekana ni jambo la kawaida kwenye michezo mingine lakini katika soka huacha kumbukumbu mbaya na anayeachiwa rekodi mbovu zaidi ni kipa anayefungwa mabao hayo.

Inawezekana kufungwa kwa mabao mengi kunatokana na ubovu wa safu ya ulinzi ama kipa mwenyewe kutokuwa makini ama imara au mipango ya timu nzima kuharibika.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya makipa na timu zao waliofungwa mabao mengi na hali inakuwaje baada ya vipigo hivyo ambapo baadhi yao wameelezea.

YANGA vs MANULA

Hivi karibuni tumeshuhudia kipa wa Simba, Aishi Manula akifungwa mabao 5-1 dhidi ya watani zao Yanga. Ingawa michuano ya CAF kipa huyo aliwahi kufungwa mabao kama hayo na timu za Al Ahly pamoja na AS Vita.

Mabao hayo yalifungwa na Kennedy Musonda, Maxi Nzengeli (2), Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua upande wa Simba lilifungwa na Kibu Denis.

Hata hivyo, katika historia ya soka ya kufungwa mabao mengi upande wa Manula mazingira yaliyotokea hayana tofauti na kipa wa zamani wa timu hiyo na kocha wa makipa, Idd Pazi.

Pazi ambaye amewahi kuwa kocha wa makipa wa Simba, anasimulia mkasa wake kuwa; “Usipokuwa makini na kukosa mtu wa kukupa ushauri nasaha basi unaweza kuvurugikiwa zaidi, utajihisi upo peke yako wote wamekukimbia, kufungwa mabao mengi kunachanganya akili.

“Nilipotoka Al Hilah kule Sudan, nilitoka kufanyiwa upasuaji wa nyonga yaani kama Manula tu hivi, nilikaa nje ya uwanja miezi nane, niliporejea basi nilipewa mechi ya kwanza kudaka nikiwa Plisner ilicheza na African Sports ya Tanga.

“Tulifungwa mabao 4-0, hapa Manula kanizidi moja ila kufungwa ni kufungwa, namshukuru Marehemu Syllersaid Mziray alitumia muda mwingi sana kunijenga kisaikolojia kwani ilinichanganya sana.

“Nafasi ya kipa ni tofauti na nafasi nyingine, kipa asipocheza muda mrefu anakosa kujiamini anapopewa nafasi, ndivyo ilivyonitokea, hivyo Mziray alinipa wiki mbili ili nikae sawa na kufanya mazoezi ya nguvu, niliporudi tulicheza mechi tatu nikiwa golini na hatukupoteza,” anasema na kuongeza;

“Sina uhakika sana kama Manula yupo fiti kabisa ama alihitaji muda zaidi, lakini hata kuitwa kwake Taifa Stars sio jambo baya ni kwenda kumjengea kujiamini, pia apate mtu sahihi wa kumjenga kisaikolojia.

“Manula kufungwa mabao hayo sio mara ya kwanza, kimataifa amefungwa ishu hapa ni kufungwa kwenye Ligi Kuu ndiko kunaweza kumvuruga zaidi tena na watani wa Jadi.”

SIMBA vs BERKO/NDUDA

Yanga nayo iliwahi kupokea kipigo cha mabao 5-0 kutoka kwa watani zao Simba msimu wa 2012/13, golini alikuwepo Yaw Berko aliyefungwa bao moja huku Said Mohammed ‘Nduda’ akifungwa manne.

Habari za ndani zilidai kuwa matokea hayo ilikuwa ni moja ya njama ya kuuondoa uongozi wa Lyod Nchunga. Na kweli mpango ulifanikiwa kwani baada ya matokeo hayo waliondolewa madarakani.

Katika mechi hiyo, mabao yalifungwa na Emmanuel Okwi (2), Felix Sunzu, Marehemu Patrick Mafisango na Juma Kaseja.

SIMBA vs ABEL

Huu ulikuwa msimu wa 2022/23, Simba ikiwa mwenyeji wa Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkapa, kwenye goli la maafande hao alisimama Hussein Abel ambaye sasa yupo Simba.

Abel na timu yake ya zamani walikubali kufungwa mabao 7-1, mabao ya Simba yalifungwa na Saidi Ntibazonkiza (3), John Bocco (3) na wakati bao lao lilifungwa na Jeremiah Juma.

“Aisee kufungwa kunavuruga, ilinichanganya wiki nzima nilikuwa naona mawenge tu, unapitia kipindi kigumu, nashukuru yalipita na maisha yakaendelea ingawa kuyafuta ni ngumu maana inabaki kwenye kumbukumbu,” anasema Abel

SIMBA vs KADEDI

Golini akiwa amesimama kipa Hamad Kadedi, Mtibwa Sugar ilikubali kichapo cha mabao 5-0 msimu wa 2022/23 dhidi ya Simba.

Mabao ya Simba yalifungwa na Pape Ousmane Sakho (2), Mzamiru Yassin, Augustine Okrah na Moses Phiri.

Kadedi anasema; “Kocha Salum Mayanga alinisaidia kunijenga kisaikolojia pamoja na wenzangu, maana yalinitoa mchezoni kabisa, kwenye mechi ile sikuwemo kikosini lakini baadaye ilinibidi nicheze kwani kipa aliyetakiwa kucheza aliumwa hivyo sikuwa na maandalizi ya kutosha.

“Tangu nifungwe mechi hiyo sikupewa tena nafasi ya kucheza mechi zilizokuwa zimebaki hadi nikaondoka, sasa nipo nyumbani huenda nikarudi uwanjani Januari.”

AZAM vs MAKAKA

Ni mechi ya ligi kuu msimu huu (2023/24), ilichezwa Uwanja wa Azam Complex ambapo Mtibwa Sugar ilikubali kipigo cha mabao 5-0 ambapo golini alisimama kipa Mohamed Makaka.

Mabao ya Azam FC yalifungwa na Kipre Junio aliyefunga matatu (hat-trick), Lusajo Mwaikenda na Feisal Salim ‘Fei Toto’ ambao kila mmoja alifunga bao moja.

Hii ni mara ya pili kwa Makaka kupokea kipigo kikubwa kwani alipokuwa akiichezea Ruvu Shooting aliwahi kufungwa na Simba ingawa ilikuwa mechi ya hatua ya 16 bora michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC).

Kwenye mechi hiyo, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 7-0, alianza Makaka kukaa golini akafungwa mabao matano na mawili alifungwa Benedictor Ticono alipofanyiwa mabadiliko.

Makaka anazungumzia hali aliyoipa baada ya kupokea kichapo hicho kuwa; “Nadhani hii kitu hakuna mtu inaweza mfurahisha hata mara moja wala kumpendeza itaumiza na hali yake ni mbaya sana.

“Mara nying inapotokea hivyo huwa mvuruganiko unatokea na ndo maana kama hampo sawa katika utulivu mnafungwa sana sababu tayari mnakua mmechanganyikiwa akili,” anasema na kuongeza;

“Ni kama kwenye ngumi ukishapigwa unatamani ukurupuke kupiga bila mbinu kumbe ndo unazidi kupigwa zaidi, hii ni rekodi mbaya kiukweli kufungwa bao nyingi lakini inapostaili kuwa hivyo kutokana na makosa yetu ni lazima utaadhibiwa tu.

“Ila kama mchezaja huwezi kukaa hutakiwi kunyongea sana sababu utashindwa kufanya yalio mbele, huwa tunapeana moyo na kutulizana ili kufanya kazi tena.

“Hata ukitamani kutoka golini kama unaona umezidiwa kwa uwingi wa mabao lakini huwezi maana anayefanya maamuzi ni kocha, hata nilipokuwa Ruvu, walinitoa baada ya wao kuona sasa hapana, mwanaume hupaswi kuomba kutoka, mwanaume hufia vitani na hupaswi kuogopa vita,” anasema Makaka

YANGA vs MASEKE (2023/24)

Kipa wa KMC, Wilbol Maseke alikubali kipigo cha mabao 5-0 dhidi ya Yanga mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa, mabao ya Yanga yakifungwa na Dickson Job, Stephane Aziz Ki, Hafidh Konkoni, Mudhathir Yahya na Pacome Zouzoua.

Maseke ameliambia Mwanaspoti kuwa; “Sio kitu chepesi, ni hali inayovuruga ila baada ya pale huwa tunazungumza na makocha, wanatujenga ili kuwa imara kwa mechi ijayo, bila hivyo unaweza kuharibu tena.”

SIMBA vs ARAKAZA (2022/23)

Aliyekuwa kipa wa Geita Gold, Mrundi Mac Arthur Arakaza alifungwa mabao 5-0 na Simba wakiwa uwanja wa nyumbani, ambapo walitumia Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Waliomtungua kipa huyo ni John Bocco, Clatous Chama, Pape Sakho (mawili) na Kibu Denis. Baadaye Geita waliamua kuachana na kipa huyo na hadi sasa hana timu na inadaiwa yupo kwao Burundi.

Hata hivyo, ukiachana na uwingi wa mabao hayo lakini kuna baadhi ya mechi zimekuwa na ushindi mnono pia kwenye ligi misimu tofauti ambapo Yanga iliifunga Tanzania Prisons mabao 4-1 (2022/23), mabao ya Yanga yalifungwa na Clement Mzize (2), Bakari Mwamnyeto na Stephane Aziz Ki wakati Ibrahim Abraham akiifungia timu yake bao hilo pekee.

Pia msimu huu Azam FC iliifunga mabao 4-0, Tabora United huku Feisal Salim ‘Fei Toto’ akipiga hat-trick na lingine likifungwa na Prince Dube.

Mwanaspoti limezungumza pia na makocha wa makipa ambao pia waliwahi kudaka miaka ya nyuma ili kuelezea nini huwapata makipa hao ambapo Ivo Mapunda anasema kuwa; “Kufungwa kunaweza kusababishwa na mambo mbalimbali ikiwemo safu ya ulinzi kama haina utulivu, ubora wa kipa mwenyewe kwa siku hiyo ama timu nzima kuzidiwa mbinu.

“Na baada ya hapo inahitajika utulivu wa hali ya juu kwa kipa vinginevyo anaweza kupotea kabisa, saikolojia yake inapaswa iwe nzuri, akishindwa kuhimili kelele za mashabiki kutoka na kipigo basi atakuwa kipa wa kupoteza.

“Kocha anaweza kuwa na mbinu zake alizompa kipa ama wachezaji wake lakini huwezi kujua mpinzani wako ameingia na mbinu gani, ila ikumbukwe kwamba timu inayofungwa mabao mengi sio kwamba mbovu ila inazidiwa mbinu,” anasema Ivo ambaye ni kocha wa makipa wa Biashara United inayoshiriki Ligi ya Championship.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: