Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Lunyamila azivusha Simba, Yanga nusu fainali CAF

Lunyamila Lunyamila azivusha Simba, Yanga nusu fainali CAF

Thu, 4 Apr 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Staa wa zamani ya Yanga na Simba aliyetamba pia na timu ya taifa, Taifa Stars, Edibily Lunyamila amesema wawakilishi wa Tanzania katika mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitakazocheza Ijumaa hii ugenini zina nafasi ya kutinga nusu fainali bila kujali ukubwa wa wenyeji wao.

Simba ipo Cairo, Misri na Ijumaa hii kuanzia saa 5:00 usiku itashuka kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, kuvaana na Al Ahly, muda mchache baada ya watani wao, Yanga kumalizana na Mamelodi Sundowns mjini Pretoria, Afrika Kusini.

Lunyamila aliyekuwa katika kikosi cha Yanga kilichocheza na Mamelodi mwaka 2001 katika michuano hiyo na kutolewa kwa jumla ya mabao 6-5, amesema timu za Yanga na Simba zina nafasi kubwa ya kushangaza mashabiki wa soka Afrika katika michezo hiyo kama tu zitaamua kupambana kwa nidhamu.

Nyota huyo aliyeibukia Biashara Shinyanga kabla ya kudakwa na Yanga na kuwahi pia kukipiga Malindi ya Zanzibar, amesema Simba na Yanga zinapaswa kucheza kimbinu zaidi ugenini kuliko zilivyocheza nyumbani katika mechi za kwanza ambazo Mnyama alilala 1-0, huku Yanga ikitoka suluhu Kwa Mkapa.

Lunyamila amesema kocha wa Yanga, Miguel Gamondi akitumia mashambulizi ya kushtukiza anaona kabisa ni jambo linalowezekana kumpa matokeo chanya ugenini Sauzi.

Amesema japo 2001 Yanga ilifungwa mabao 3-2 na Mamelodi ugenini kisha kutoka sare ya 3-3 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza, katika mechi ambazo timu ya Wananchi ilionyesha soka la kiwango cha juu, hivyo anaiona Yanga ya sasa ina nafasi ya kufanya makubwa zaidi kwa aina ya kikosi kilichopo.

"Zamani kulikuwa na figisu nyingi sana, tofauti na sasa hivi, tulifika uwanja wa ndege tulikaa kwa saa mbili, tukapewa gari dogo na tulikuwa wengi, hivyo wengine walisimama na tulikuwa tunaenda mbali, tukafika tumechoka," amesema Lunyamila aliyekumbushia kikosi kilichovaana na Mamelodi msimu huo wa 2001.

"Sikumbuki kikosi chote, kipa alikuwa ni Doyi Moke, Mwanamtwa Kihwelo, Abubakar Kombo, Yahya Issa, Ally Mayay Tembele, Wazir Mahadhi, Said Maulid 'SMG', Idd Moshi, mimi Lunyamila, Ally Yusuf 'Tigana' na wengine nimewasahau," amesema, huku akisema hata Simba ina nafasi licha ya kupoteza nyumbani kwa bao 1-0.

Mbali na wachezaji hao aliowataja Lunyamila msimu huo Yanga iliyokuwa chini ya kocha Charles Boniface Mkwasa, ilikuwa pia na majembe ya maana kama Mohammed Abdukadir 'Tash', Mohammed Abubakar 'Phantom', Chibe Chibindu na Yusuf Macho 'Musso' na Paul John Masanja.

Lunyamila pia alitoa ushauri kwa vikosi ambavyo anadhani vikianzishwa timu hizo za Tanzania zinaweza kufuzu akitamani Yanga ingeanza kwa mziki huu wa; Djigui Diarra, Yao Kouassi (atakosekana kwa vile bado ni majeruhi), Joyce Lomalisa, Ibrahim Bacca, Dickson Job, Khalid Aucho, Pacome Zouzoua, Mudathir Yahya, Aziz Ki, Kennedy Musonda na Augustine Okrah

Kwa upande wa Simba ameshauri ipangwe namna hii; Ayoub Lakred, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Henock Inonga, Fondoh Che Malone, Mzamiru Yassin, Fabrice Ngoma, Saido Ntibazonkiza, Kibu Denis, Clatous Chama na Pa Omar Jobe.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: