Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa hili.. Simba, Yanga zimepiga bao..

Simba, YANGA Kwa hili.. Simba, Yanga zimepiga bao..

Mon, 9 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba na Yanga zimekuwa zikitambiana sana mtaani hasa pale mmoja anapochemsha kwenye mechi inazocheza, lakini kuna wakati huigana na hata kuungana kwenye mambo ya msingi

Kwa mfano kwa sasa klabu hizo zipo kwenye mchakato wa kutaka kuendeshwa kisasa kwa mfumo wa hisa na kuondokana kuwa chini ya wanachama kama zilivyoasisiwa miaka zaidi ya 85 iliyopita.

Katika kwenda na mfumo huo, klabu hizo zimeanza kuondokana na kadi za kizamani za makaratasi na kuingia kadi za kisasa (smatikadi) ambazo zinawarahisishia kulipa ada zao moja kwa moja kupitia benki na kusaidia kuzinufaisha klabu hizo tofauti na mfumo wa zamani.

Kuanzia kujiandikisha hadi kulipa ada zao kunazifanya klabu kunufaika na wanachama nao kunufaika kupitia akaunti walizofungua kwenye benki wanazodili nazo na hata chini ni namna benki ya NMB ilivyoweza kuwarahisishia kazi klabu na wanachama hao wa Simba na Yanga.

Utamu ni wanachama wana mzuka kwa sasa kutokana na klabu hizo zinavyozidi kufanya vizuri katika michuano ya ndani na ile ya kimataifa zote zikiwa makundi ya Ligi za Mabingwa Afrika, Simba ikiwa Kundi B na timu za Wydad Casablanca ya Morocco, Jwaneng Galaxy (Botswana) na Ases Mimosas (Ivory Coast), ilihali Yanga ikipangwa Kundi D na Al Ahly (Misri), CR Belouizdad (Algeria) na Medeama (Ghana).

SIMBA WATOA NENO

Mkuu wa kitengo cha habari cha Simba, Ahmed Ally anasema kwa kutambua thamani ya mchakato huo kwa klabu yao wamejipanga kutoa elimu kwenye matawi yao mbalimbali hapa nchini.

“Elimu hiyo tumeianza tangu Oktoba Mosi mwaka huu, kwa kusaidiana na benki ya NMB ambao ndio wenye jambo lao, lengo ni kuhakikisha kila mwanasimba anaelewa na kuufahamu mfumo huu ambao utakuwa na manufaa makubwa,” anasema Ahmed. Anasisitiza, Simba walianza kufanya hivyo huko nyuma lakini wanathamini sapoti ya wanachama wao na ndiyo maana wakaona waiweke katika ubora mkubwa ambao NMB inaufanya kwa sasa.

“Jumapili pale Chamazi wanachama wetu wataipata fursa hiyo ya kujisajili itakayokuwepo hapo hapo uwanjani hivyo nawaomba wajitokeze kwa wingi kwani kadi zipo za kutosha na NMB hawana shaka katika jambo hilo,” anasema Ahamed.

YANGA YAITA WANACHAMA

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Arafat Haji anabainisha ni wakati sahihi kwa mwanayanga kujisajili na kupata kadi yake ya uanachama na kuacha kuwa mwanachama jina.

“Mwananchi mwenzangu uanachama wako ni wa kujisajili au mwananchi jina, kama bado upo kwenye kundi la wananchi jina toka huko njoo huku kwa wananchi wenye timu,” anasema Arafat na kuongeza;

“Unaijua faida ya kuwa mwananchi uliyejiandikisha na kutambulika rasmi na klabu, kwanza kabisa unaichangia timu yako moja kwa moja kupitia usajili na ada ya uanachama, utaweza kushiriki shughuli mbalimbali za klabu kama kuchagua viongozi au kuchaguliwa kuwa kiongozi.”

Anasema wananchi wanapofurahia mafanikio ya klabu yao na wao wawe sehemu ya furaha hiyo na fedha hizo zitasaidia katika uendeshaji wa klabu.

“Kujiita Mwananchi wakati haujajisajili ni sawa na kuwaibia furaha wananchi waliojisali,” anasema Arafat.

NMB WAFAFANUA

Meneja uhusiano NMB anayeshughulikia michezo, Hassan Bumbuli aliyekuwa msemaji wa Yanga hivi karibuni anasema mambo yanaenda sawa kuhakikisha wanachama wote wa timu hizo wanapata haki yao ya msingi.

Anasema kitendo cha mwanachama kuchangia kupitia kadi ya uanachama kunawafanya viongozi wao kutotoa macho zaidi katika suala la usajili na ikizingatia timu zote kwa sasa zinasajili wachezaji wazuri ambao wanaleta ushindani mkubwa.

Anasema mwitikio ni mkubwa kwa wanachama na mashabiki wa timu zote, wanajitokeza kwa wingi, pia wengi wanataka kujua zaidi kuhusu utaratibu huu, hivyo elimu inahitajika zaidi kutoka kwa klabu zote pamoja na wao.

SIMBA MAMBO MOTO

Bumbuli anasema, licha ya wote kujisajili kadi za uanachama kupitia benki hiyo lakini viwango vyao viko tofauti.

“Kwa Simba ni rahisi sana maana utaratibu ni mmoja kwa wote, kwa Yanga kuna madaraja na namna tofauti za kulipia hii inaleta changamoto hasa kwa wanayanga wenyewe kuelewa, maana shabiki analipa kiwango chake,” anasema Bumbuli na kuongeza;

“Mwanachama analipa kiwango chake, pia katika hivyo viwango vinatofautiana kati ya wanaotaka kufungua akaunti, wasiotaka akaunti na wale ambao tayari wanaakaunti na benki yetu.”

Aidha Bumbuli anasema suala la kutoa elimu ni endelevu, kwa kuwa ni utaratibu mpya ambao umekuja na mambo mapya na ni muhimu kuendelea kutoa elimu.

“Sisi kama benki tunaendelea kuwaelimisha wanachama na mashabiki kupitia vikao vyetu tunavyokutana nao, pia tunaziomba klabu ziendelee kutoa elimu kwa mashabiki na wanachama wao juu ya zoezi hii ili kuongeza uelewa,” anabainisha.

FAIDA YA KUJISAJILI

Anasema jambo hilo lina tija kubwa kwa klabu, wanachama na mashabiki, hivyo ni muhimu watu wakajisajili kwa kuwa kufanya hivyo ni matunda makubwa kwa klabu zao.

“Tumekuwa na malengo makubwa ambayo yanakwenda kutoa manufaa ya moja moja kwa shabiki na mwanachama kwa upande mmoja, pia kwa klabu yake kwa upande mwingine,” anasema Bumbuli.

ELIMU KUTOLEWA

Bumbuli anasema wameshaanza kutoa elimu na wanaendelea kufanya hivyo kupitia matawi yao ya benki yaliyotapakaa nchi nzima.

“Pia jambo hili kutokana na ukubwa wake tunahusisha vyombo vya habari ambavyo tunaamini kwa nguvu yao, elimu itawafikia wengi sana,” anasema.

MASHABIKI YANGA WATISHA

Ili mwanayanga aweze kupata kadi hiyo ya uanachama anatakiwa kulipia ada hiyo ambayo imegawanyika katika makundi tofauti.

“Ada ya mwanachama jumla ni Sh34,000 (ada ya mwaka Sh24,000, ada ya kadi ya Debit ya Yanga na NMB, Sh5,000, amana ya awali kwenye akaunti ya Sh5,000,” anasema.

“Kundi la pili ni ada ya shabiki jumla ya Sh22,000 (ada ya uanachama kwa mwaka sh 12,000, Ada ya kadi ya Debit ya Yanga sh 5,000, amana ya awali ya akaunti Sh5,000,” anasema Bumbuli na kuongeza;

“Kundi la tatu mchakato kwa wanachama na mashabiki kama anataka kadi ya NMB bila akaunti ada ya uanachama kwa kadi ya Yanga anapaswa kulipa jumla ya Sh29,000 (ada ya mwaka ya uanachama Sh24,000, ada ya kadi Sh5,000.” Aidha Bumbuli alisema, kundi lingine shabiki ada ya kadi ya Yanga ya NMB Sh17,000 (ada ya mwaka ya uanachama Sh12,000 huku ada ya kadi Sh5,000.

Kundi la mwisho kwa upande wa Yanga ni “Mteja wa NMB ambaye si mwanachama wa Yanga, atajaza fomu ya ombi ya kadi ya Yanga na NMB ya kulipia kabla (prepaid) kisha atasajiliwa kwenye tovuti ya Yanga kama mwanachama, atalipa Sh29,000/- (Ada ya mwaka ya uanachama Sh24,000, ada ya kadi Yanga na NMB, Sh5,000).

WANACHAMA SIMBA SHANGWE

Bumbuli anasema mashabiki wa Simba wao ni aina moja pekee tofauti na wenzao na ndio sababu ya kutoa elimu ili waweze kuelewa namna jambo hilo linavyoenda.

“Kwa Simba wote wanatakiwa kulipa Sh10,000 tu, iwe Simba SC, Simba Queens hakuna zaidi ya hapo na hiyo ni mgawanyo na Sh5,000 ni kwa ajili ya kadi ambapo kadi hiyo itatumika miaka mitatu,” anasema.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: