Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kwa Miquissone, hata Yanga wanatetemeka

Luis Miquissone New Kwa Miquissone, hata Yanga wanatetemeka

Mon, 24 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kwa mujibu wa vyanzo vyangu vya uhakika tayari Simba imemalizana na Luis Jose Miquissone. Nyota huyo raia wa Msumbiji atatangazwa Msimbazi muda wowote kuanzia sasa.

Ni yule aliyewahi kuwatetemesha Al Ahly hapo kwa Mkapa. Akafunga bao bora la wiki kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Huku Bongo tunapenda kumuita Konde Boy.

Miquissone ni fundi haswa. Ana sifa zote za mchezaji mkubwa. Ilikuwa kama bahati kwa Simba kuinasa saini yake kwa mara ya kwanza. Unajua kwanini? Yanga ndio waliokuwa wakimpigia hesabu baada ya kumuona kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa UD Songo ilitoing'oa Simba kwa faida ya bao la ugenini.

Mechi ya ugenini iliisha 0-0 na ya hapa Dar Konde aliupiga mwingi na Simba kulazimisha sare ya 1-1 na kung'olewa. UD Songo iliondoka, lakini jina la Konde Boy lilibaki. Yanga wakajiandaa kumpokea, Simba wakafanya umafia na kutibua dili baada ya kumfuata Msumbiji. Ghafla akatua Msimbazi na Yanga kuachwa solemba. Baada ya mwaka mmoja na nusu tu aliuzwa kwenda Ahly kwa zaidi ya Shilingi 2 bilioni. Ni fedha nyingi hata kwa kuzitamka tu. Ni bajeti ya idara fulani fulani za serikali.

Wachezaji wengi hulazimika kucheza sehemu moja kwa muda mrefu ili kuacha alama ila kwa Miquissone alihitaji mwaka mmoja na nusu tu pale Simba kuwaambia juu ya uwezo wake.

Akaionyesha Afrika juu ya uwezo wake. Aliwatetemesha mabeki wa Tanzania na nje. Nani angefurahi kucheza dhidi yake? Hakuna. Hata mabeki wakorofi kama Kelvin Yondani, Juma Nyosso na wengineo waliogopa miguu yake.

Miquissone ni winga wa kisasa. Ana kasi. Ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira. Ana uwezo wa kupiga chenga. Anapiga na miguu yote miwili kwa ufasaha. Ana akili kubwa ya soka. Vipi kuhusu yale mashuti yake? Nani amesahau lile bao la umbali mrefu alilowafunga Ahly kwa Mkapa?

Ama niwakumbushe lile bao lake matata lililokausha sauti ya Mtangazaji wa Azam TV, Nurdin Selemani pale Dodoma? Ni historia kubwa.

Ahly hawakuwa wajinga kuilipa Simba kiasi kile cha fedha kumnunua Miquissone. Ana uwezo mkubwa. Bahati mbaya tu hakuweza kufanya makubwa pale Misri.

Kuna sababu nyinyi ndani yake. Inatokea duniani kote mchezaji mzuri anaweza kwenda timu nyingine na akashindwa kufanya makubwa. Mifano iko mingi.

Philipe Coutinho aliondoka akiwa mchezaji mahiri zaidi pale Liverpool. Akaenda Barcelona kwa rekodi ya ada ya uhamisho. Nini kilitokea? Ni kichekesho.

Coutinho hakuweza kabisa kutamba pale Barcelona. Akawa mchezaji wa kawaida. Watu wakasahau namna alivyokuwa akiibeba Liverpool katika mabega yake.

Vipi kuhusu Eden Hazard kutoka pale Chelsea kwenda Real Madrid? Alikuwa roho ya Chelsea. Alitetemesha viwanja vya soka pale England. Alikuwa tishio.

Lakini baada ya kutua Real Madrid akawa kituko. Usingeweza kuamini ndiye yule Hazard ambaye mabeki wa Manchester United na Arsenal walitetemeka walipomuona.

Hiki ndicho ambacho kimetokea kwa Miquissone pale Ahly. Alikwenda akiwa mchezaji mahiri lakini hakuweza kuonyesha hayo kwa mabingwa hao wa Afrika.

Sababu ya pili ni mabadiliko ya benchi la ufundi. Miquissone alisajiliwa na Pitso Mosimane pale Ahly. Baada ya muda mfupi kocha huyo aliondoka. Wakaja makocha wengine na mipango yao.

Wakati mwingine ni vigumu kwa mchezaji mwingine kuweza kubadilika kwa kile ambacho makocha wapya wanataka. Anatoka kwenye mfumo na baadaye anaonekana hana mchango kwenye timu.

Sababu nyingine zinaweza kuwa za nje ya uwanja. Pengine mazingira ya kuishi, vyakula na vitu vingine vinaweza kumpunguza mchezaji makali. Huwa inatokea duniani kote.

Ndio sababu unaweza kusikia mchezaji fulani anataka kuhama sehemu kwa sababu hana furaha na maisha ya pale. Ni kama ilivyokuwa kwa yule Carlinhos wa Yanga.

Alikuja akiwa mchezaji mahiri lakini maisha ya nje ya Uwanja yakawa magumu kwake. Kwanza lugha. Pili vyakula na hali ya hewa. Baadaye akarudi kwao Angola na anakiwasha kwa kiwango bora mpaka sasa.

Hata Clatous Chama ilimkuta pale RS Berkane ya Morocco alipouzwa sambamba na Miquissone. Alichemsha na kurudi Msimbazi. Ndivyo soka lilivyo.

Hivyo ni ngumu kusema kama Miquissone ameshuka kiwango kwa kuwa ameshindwa kufanya vizuri pale Ahly.

Lakini turejee upande wa pili. Ahly ni klabu namba moja kwa ubora Afrika. Simba ipo nafasi ya saba. Ni kweli mchezaji akishindwa kutamba Ahly atashindwa pia kutamba Simba? Hapana. Ni lazima tukiri kuwa Ahly ipo katika dunia yake.

Pia pale Misri sheria za wachezaji wa kigeni ni ngumu kuliko maeneo mengi ya Afrika. Ni wachezaji wanne tu wa kigeni wanaruhusiwa katika timu moja. Ila wanaweza kuongeza mchezaji wa tano kutoka nchi za Palestina, Syria, Tunisia, Morocco, Algeria ama Libya.

Hii inamaanisha kuwa ushindani ni mkubwa. Ahly ikiona mchezaji mwingine mahiri zaidi Afrika inalazimika kumpunguza mmoja kati ya hawa watano

Hivyo hakuna namna watakusubiri ufike katika kilele cha ubora wako. Wanalazimika kumpunguza yule ambaye hayupo katika kiwango bora kwa wakati huo. Ndicho ambacho kimemkuta Miquissone.

Pale wana Ally Maaloul na Cresto kutoka Tunisia, Ahmed Kendouci kutoka Algeria, Aliou Dieng na Percy Tau. Bado walikuwa na Walter Bwalya ambaye naye walimtoa kwa mkopo.

Ni wazi kuwa kwa sasa ni ngumu kuwagusa Dieng, Kendouci, Maaloul na Tau. Hawa ni wachezaji wao tegemeo wa kigeni. Ingekuwa ngumu sana kwa Miquissone kupenya katikati yao.

Mwisho turejee kwa Simba wenyewe. Ni kweli wanamhitaji Miquissone? Ni kweli. Nafasi ya Miquissone iko wazi kabisa.

Tangu aondoke Simba wamesajiliwa nyota wengi na wameshindwa kufikia hata nusu ya ubora wake. Alikuja Duncan Nyoni kutoka Malawi. Hakuwa na jipya. Akaachwa baada ya muda mfupi tu.

Akachukuliwa pia Bernard Morrison kutoka pale Yanga. Akawa hana jipya. Alicheza vizuri siku ambazo alijisikia tu. Hakuweza kabisa kuvaa viatu vya Miquissone.

Wakaja Pape Sakho na Peter Banda. Wana jipya gani? Hakuna. Sakho anaonekana kuwa na kipaji kikubwa lakini hana jitihada za Miquissone. Hawezi kuamua mechi kama Miquissone.

Banda amekuwa kama gari la mkaa. Safari moja shamba, moja gereji. Majeraha yamekuwa sehemu ya maisha yake. Ni muda mchache sana anakuwa uwanjani.

Simba ikaenda pia kumsajili Augustine Okrah. Akaanza na moto, lakini ukazimika kama umekumbwa na mvua ya El Nino. Akawa wa kwanza kuachwa msimu ulipomalizika tu.

Kwa kifupi, Simba imepoteza fedha nyingi kupata mastaa wa kucheza nafasi ya Miquissone. Hii inawafanya wawe na hamu kubwa kumrejesha.

Mwisho, Simba inakwenda kushiriki African Football League. Ni mashindano yanayoshirikisha timu nane kubwa Afrika. Ili kwenda katika mashindano haya unahitaji wachezaji wakubwa kama Miquissone.

Nadhani wakati huu ambapo taarifa za Miquissone zinakaribia kuwa rasmi. Hata Yanga wanatetemeka wakikumbuka ubora wa staa huyu. Konde Boy.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: