Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kuna ka ufanano kameanza kunitisha kwa Onana

Onana Simba Sd Willy Osamba Onana

Tue, 31 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Jina? Willy Osamba Onana. Uraia? Cameroon. Umri? Miaka 23. Ananikumbusha kitu. Namfananisha na huyu hapa. Jina? Michael Sarpong. Umri miaka 24. Utaifa?. Ghana. Wote hawa wawili wanatokea Afrika Magharibi na waliwasili nchini wakitokea Ligi kuu ya Rwanda wakiwa wafungaji bora.

Kuna mfanano upo na umeanza kunitisha. Mashabiki wa Simba wameanza kulalamikia kiwango na uchezaji wa Onana. Wanasema ni bishoo. Wanasema amelegea. Wanasema hana jipya kwao. Mashabiki wa watani wao pia wameanza dhihaka nyingi dhidi yake.

Sikumtazama Onana katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Power Dynamo. Pambano la Siku ya Simba maarufu kama Simba Day. Lakini hapohapo nikabahatika kuliona bao lake. Lile alitokea upande wa kushoto, akalitafuta boksi la adui, wakati anaingia katika boksi akapiga bonge la shuti. Nyavuni. Pale niliamini Simba imepata mtu wa maana ambaye atapunguza maringo ya kina Chama klabuni.

Nikamuangalia tena Tanga katika mechi za Ngao ya Jamii. Hakuwa na jipya. Nikamtazama tena na tena sikuona jipya. Nilidhani nipo peke yangu. Wakaanza kuongezeka watu waliokuwa wanakiona kitu kama nilichokiona. Hatimaye tumefikia hapa ambapo mashabiki wa Simba wanaamini “Onana tumepigwa.”

Wakati mwingine wachezaji huanza taratibu kisha kuibuka kuwa moto. Wakati mwingine nawajua walionza kwa kasi kama akina Laudit Mavugo halafu baadaye wakawa wachezaji wa kawaida. Onana bado ana muda wa kurekebisha mambo. Hatuwezi kumuhukumu sana lakini kuna kitu tu kinanitisha.

Kuna mzimu unanitisha. Mzimu ambao umesababisha pia nimkumbuke Sarpong. Hivi tuendelee kuiamini Ligi kuu ya Rwanda? Sina uhakika. Sarpong alikuja katika soka letu akiwa mfungaji bora wa Rwanda. Mabao 16. Onana pia amekuja akiwa na mabao 16. Wote walitua nchini kama watu hatari.

Kumbe kuna uwezekano mkubwa walikuwa wanacheza katika ligi nyepesi. Sarpong alirukaruka zake na maji yakaonekana mazito kwake. Walau Onana anaonekana kuwa na akili fulani ya mpira ingawa kuna vitu anakosa. Kwa namna ligi yetu inavyochezwa asipojirekebisha basi hatakuwa na maajabu. Lakini kumbuka kuwa hata Patrick Sibomana alitokea Rwanda kama mchezaji hatari lakini hakuwa na maajabu Yanga.

Hiki kitu ndio kinanitia wasiwasi kuhusu Onana. Si ajabu tukajikuta tunaacha ule mpango wa kuchukua ‘watu hatari Ligi kuu ya Rwanda.’ Kumbe inawezekana hawatoshi katika ligi yetu hata kama tunaidharau ligi yetu. Mifano imeanza kuwa mingi na inanitisha. Naambiwa katika Ligi ya Rwanda wachezaji wanapewa nafasi ya kupishana. Wanacheza kwa nafasi tofauti na ligi yetu.

Mfanano mwingine ambao unanitisha ni huu hapa. Sarpong alikuja nchini akiwa na miaka 24. Sasa hivi ana miaka 27. Onana ana miaka 23 tu. Wote hawa wametoka Afrika Magharibi katika mataifa ambayo yana sifa kubwa ya soka. Mmoja Ghana mwingine Cameroon.

Kama wangekuwa na uhatari huo ambao tumeambiwa siamini kama wangeangukia katika ardhi ya Rwanda. Wote ni wafungaji na soko la wafungaji ni rahisi kuliko la wachezaji wa nafasi nyingine uwanjani. Ilikuaje wakaangukia Rwanda? Huwa inatia wasiwasi. Lakini kuna mahala kulikuwa na shida katika uchezaji wao ndio maana hawakuangukia katika mataifa yanayolipa zaidi kisoka.

Sio kwamba hatupokei wachezaji wa Afrika Magharibi wenye uwezo mzuri kisoka. Hapana. Tunapokea. Hapa tumewahi kuwapokea akina Kipre Tchetche, Kipre Balou, na sasa hivi kina Pacoume. Hata hivyo, naamini kwamba sio kwa wao tu bali ukiwaona wachezaji fulani wa Afrika Magharibi wanacheza hapa kwetu au katika ukanda wetu basi wanakuwa na tatizo fulani hivi.

Inawezekana ikawa umri umekwenda, Inawezekana ikawa wana tabia mbovu kama ya rafiki yangu Ben Morrison, inawezekana wana majeraha waliyoyaficha, lakini pia wengine wana bahati mbaya. Lakini kuna hawa wa kawaida kabisa ambao wana uwezo wa kawaida wasingeweza kwingine.

Hawa akina Sarpong na Onana kwa mataifa wanayotoka ni rahisi kuaminika na kupata timu kwa haraka kuliko Clement Mzize. Kuliko Mbwana Samatta. Kuliko John Bocco wa wakati ule. Kuliko Simon Msuva. Bosi wa timu ya Ligi Kuu ya Ubelgiji au Uturuki akipelekewa mezani jina la Sarpong na Bocco yule basi akili yake ya kwanza itakuwa kwa mchezaji mwenye pasipoti ya Cameroon.

Onana anapaswa kuwaondoa mabosi wa Simba katika bahati mbaya ambayo wanaipitia kwa sasa. Fikiria, katika kikosi cha kwanza cha Simba ni wachezaji wawili tu wapya ambao walau wamepata uhakika wa kucheza. Fabrice Ngoma na Che Malone. Onana ameingia katika orodha ya wachezaji wanaopigwa mkeka. Hata asipopangwa mashabiki hawastuki.

Kwanini asiwaondoe katika bahati mbaya? Kwa sababu kwa hii miaka miwili mabosi wa Simba wamekuwa wakikosea kusajili.

Wanachukua wachezaji wachache wanaoweza kuingia katika kikosi cha kwanza. Vinginevyo Simba inaendelea kurudi kwa wachezaji walewale ambao inawategemea kila siku. Akina Clatous Chama.

Ilitazamiwa mchezaji kama Onana aingie katika kikosi na kuwa muhimu lakini ukiwapelekea mashabiki wa Simba wachague mchezaji wa kuanza pambano la Simba na Yanga wikiendi ijayo kati ya Kibu Dennis na Onana basi asilimia 99 watasema Kibu aanze.

Hili halina ubishi. Hatuhitaji hata hizo kura zipigwe.

Sijataka tamaa na Onana. Hata Aziz Ki msimu uliopita alizingua tu licha ya kutupiga matukio machache. Labda baadaye atazoea na kuwa mgumu. Kipaji kipo pale kwa kila mtu anakiona. Ni maamuzi yake kupambana lakini nahofia tu kwamba huenda hiyo ni aina yake ya mchezo.

Kama ndio aina yake ya mchezo basi hapa hapatakuwa mahala salama sana kwake.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: