Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kumekucha Manula apewa rasmi Al Ahly

Aishi Manula Is Back.jpeg Aishi Manula

Mon, 16 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kambi ya Simba mzuka umepanda zikiwa zimebaki siku nne tu kabla ya timu hiyo kushuka Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuvaana na Al Ahly katika mechi ya uzinduzi wa Ligi mpya ya Afrika ‘African Football League’, huku kocha wa timu hiyo, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akifichua hiyo ni mechi ya Aishi Manula.

Inaelezwa dakika 40 alizocheza kipa huyo namba moja wa timu hiyo kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Dar City, umemshtua kocha Robertinho aliyeweka wazi anataka kumpa nafasi kwenye pambano hilo la kwanza la AFL litakalopigwa Ijumaa kabla ya kwenda kurudiana nao Oktoba 24, jijini Cairo Misri.

Manula alikuwa nje ya uwanja tangu alipoumia Aprili 7 kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Ihefu, lakini kurejea kwake wikiendi iliyopita kumempa faraja kubwa Mbrazili aliyesema dakika hizo 40 alizocheza Mo Simba Arena, zimempa matumaini ya kumtumia kwenye mechi hiyo ya Afrika.

Kocha Robertinho aliliambia Mwanaspoti ameridhishwa na kiwango cha Manula na moja kwa moja ameamua kumuweka kwenye mipango ya mchezo huo wa Ijumaa unaotarajiwa kuhudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), Gianni Infantino, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika, Dk Patrice Motsepe pamoja na vigogo wengine wa soka ili kushuhudia uzinduzi huo. “Kila kocha anatamani kuwa na wachezaji wote kikosini, tumefurahi kumwona Manula akirejea lakini kwa kuonyesha kiwango bora. Kitu kizuri amerejea wakati tukijiandaa na mechi ya Al Ahly, ni mchezaji mzoefu na tayari tumemjumuisha kwenye mipango yangu kama ilivyo kwa wengine,” alisema Robertinho.

Kocha huyo alisema pia anafurahishwa na jinsi ari kwa wachezaji wa timu ilivyo kabla ya pambano hilo kubwa ambalo Simba inahitaji ushindi kabla ya kwenda ugenini ili ipenye kwenda nusu fainali na itajihakikishia kuvuna mabilioni ya fedha zinazotolewa na wadhamini wa michuano hiyo mipya.

Baadhi ya wadau wamezungumzia juu ya kurejea kwa Manula na kusema itakuwa na faida kwa timu kwani tangu kipa huyo alipoumia, kulikosekana utulivu kwenye eneo hilo licha ya kuwepo kwa makipa wengine na mabeki waliokuwa na kazi kubwa ya kuwalinda iwe katika mechi za ndani na zile za kimataifa.

Nyota wa zamani wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alisema; “Manula ni mkongwe na mzoefu kwa mechi ngumu kama hii, japo sidhani kama atakuwa na utimamu wa mechi (Game Fitness) kwa kiwango kikubwa, ila benchi la ufundi ndilo lina maamuzi,” alisema Julio na kuongeza;

“Hata asipodaka Manula, makipa wengine waliopo Simba wanaweza kudaka na kufanya vizuri, hakuna kipa asiyefungwa duniani, hivyo Simba inachotakiwa kufanya ni kucheza kwa tahadhari na kupunguza makosa kwenye kila eneo.”

Kiungo wa zamani wa Tukuyu Stars, Yusuph Kamba ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka alisema; “Ni jambo jema kuona amerejea katika majukumu yake. Uwepo wake kikosini utaleta hamasa hata kwa wachezaji wengine pia wataongeza hali ya kujiamini kwani ni mzoefu pia akiwa langoni ni kama kiongozi kwa mabeki wake.”

Wachezaji wengine wa Simba waliokuwa timu ya taifa, Taifa Stars huko Saudi Arabia ambako jana ilicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan, Ally Salim, Israel Mwenda, Mzamiru Yassin na Kibu Denis watajiunga na wenzao kesho kambini, wakati Chama aliye Zambia na Inonga wa DR Congo watajiunga keshokutwa.

Mbali na Simba na Al Ahly, ligi hiyo inashirikisha pia Petro Luanda ya Angola, TP Mazembe (DR Congo), Enyimba (Nigeria), Wydad CA (Morocco), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) na Esperance (Tunisia).

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: