Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Kennedy Juma aaminiwe ana kitu!

Kennedy Juma Simba SC.jpeg Kennedy Juma aaminiwe ana kitu!

Wed, 1 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Simba ni moja ya klabu ambazo makocha huwa hawadumu. Spidi ya makocha kuingia na kutoka ni ya hali ya juu. Napata shida sana kuelewa kwanini beki Kennedy Juma siku zote anaanzia benchi. Napata tabu sana kulielewa hili. Labda kuna wachezaji walizaliwa maalumu kuja kukalia Benchi. Labda kuna Wachezaji ambao maisha yao yote ni benchi tu.

Pale kwenye timu yetu ya Taifa Stars nako kumejaa makocha. Wanaingia na kutoka. Kennedy Juma anaitwa timu ya Taifa kila kukicha lakini anakwenda benchi. Hivi ni kweli alizaliwa kukaa benchi? Naomba maoni yako kwa njia ya Ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya Simu hapo juu.

Nimemuona Kennedy akicheza sambamba na Joash Onyango na ameupiga mwingi tu. Nimemuona Kennedy akicheza sambamba na Henoc Inonga, kila siku anaupiga mwingi balaa. Lakini bado anafia Benchi. Tazama matumizi yake pale kwenye Taifa Stars, ni Benchi juu ya Benchi. Pamoja na Makocha kubadilika kila siku lakini Kennedy nafasi yake imeendelea kuwa kwenye Benchi. Akiwa Simba ni Benchi. Alikuwa Taifa Stars ni Benchi tu. Kuna kitu sikielewi hapa. Kuna kitu kinanisumbua hapa kwa Kennedy!

Dunia kote, hakuna mchezaji anayeimarika kwa kukaa Benchi. Wachezaji wote wakubwa huanza kwenye kikosi cha kwanza. Kama akicheza sambamba na Henoc Inonga hafanyi makosa, Kama akicheza sambamba na Che Malone hafanyi makosa, ni kwanini haanzi Wachezaji hawa wakiwa wazima? Maana Mara nyingi yeye huanzishwa pale ambapo moja Kati ya Wachezaji hawa wanaumwa au wana shida nyingine. Sikumbuki siku Kennedy alipofanya kosa la Binafsi lililopelekea Simba au Taifa Stars kufungwa Goli. Kama kuna Mtu anamfuatilia vizuri naomba anisaidie mapungufu ya Kennedy Juma.

Namuona Kennedy Kama mchezaji mwenye nguvu. Namuona Kama Beki mzuri kwa mipira ya juu kutokana na umbile lake. Namuona kama mlinzi asiye na mbwembwe kule nyuma. Namuona kama Mtu mwenye “mapafu ya mbwa”. Kennedy hachoki. Kennedy hana mzaha. Mpaka leo ukiniuliza ni kwanini hachezi kikosi cha kwanza, sina majibu. Soka ni mchezo wa wazi. Kennedy anaonekana kila anapopata nafasi na binafsi huwa sioni makosa ya moja kwa moja ya mchezaji huyu. Ninachokiona ni kukaa Benchi tu. Nimemuona akicheza mechi za ndani. Nimemuona akicheza mechi za Kimataifa akiwa kwenye Klabu. Nimemuona akicheza pia mechi za Kimataifa akiwa na Taifa Stars. Ukiniuliza anakosea nini, sina majibu.

Natamani kumuona akianza hata mechi tano mfululizo. Bado sielewi ni kwanini sio chaguo la kwanza. Sijui ni nini kinafanya aendelee kuaminika kama mchezaji wa Benchi. Sijui nini kinakosekana kwake kuaminiwa kama mchezaji mwenye sifa za kuanza. Ukitazama ule ukuta wa Simba, naona unafungika tu siku hizi. Naona magoli yakitumbukia tu kila siku lakini Kennedy amekalia Benchi. Che Malone na Henoc Inonga ni Wachezaji wazuri lakini bado Kennedy anaweza kuanza pale. Wanachomzidi Kennedy ni ushawishi kwa sababu Wachezaji wakigeni wana nguvu sana na cha pili, Wachezaji hawa wanauwezo mkubwa sana wa kuuchezea mpira kuliko Kennedy. Ni wazuri sana kwenye kuanzisha mashambulizi kutokea nyuma lakini wanafungika. Inonga na Che Malone wanafungika tu kirahisi. Kuna haja ya Mmoja wao kuanza na Kennedy. Naiona kabisa nafasi ya Kennedy.

Anahitajika tu Kocha wa kumuamini. Hana masihara kijana wa Kanda ya ziwa. Beki pekee asiyecheka cheka zama hizi. Kama angekuwa hana kitu, Simba wasingeendelea kuwa naye kikosini. Kama hana kitu asingekuwa anaitwa Taifa Stars. Kama Taifa linafikia hatua ya kumuita mchezaji ambaye sio chaguo la kwanza kwenye Klabu yake, haiwezi kuwa bahati mbaya. Lakini kuna kitu. Kennedy hayupo pale kwa bahati mbaya.

Wakati mwingine wachezaji ni imani tu. Pale Yanga imefika mahali walinzi wao Watatu wote ni Wazawa. Wameletwa wageni pale lakini hakuna mwenye jipya. Bado ukuta wa Bakari Mwamnyeto, Dickson Job na Ibrahimu Bacca unaonekana kuwa bora kuliko chochote. Unaonekana kuwa ukuta wa chuma. Simba kule pembeni kila siku ni Shomary Kapombe na Mohammed Hussein, ni Watoto wa nyumbani na wameupiga mwingi sana kwa miaka yote. Wakati mwingine Wachezaji wanahitaji nafasi tu na kuaminiwa. Sitaki kuamini Kama Kennedy yuko Simba kwa bahati mbaya. Siamini kama Kennedy anaitwa Taifa Stars kwa makosa. Ana kitu kwenye Miguu yake.

Kuna namna anastahili kuaminika zaidi. Najua soka ni mchezo wa wazi. Labda Mimi simtazami vizuri. Labda yuko pale kwa bahati. Naomba maoni yako ya namna unavyomtazama Mlinzi huyu wa Simba. Naomba ujumbe mfupi wa Maandishi kupitia namba yangu ya Simu hapo juu. Nieleze tu kwa ufupi mapungufu ya Kennedy ni yapi anapoanza ndani ya kikosi cha kwanza. Simba inacheza vizuri sana pale nyuma lakini wanafungika. Simuoni Beki mgumu pale nyuma. Che Malone na Henoc ni watu wa Udambwi udambwi. Nadhani Simba Inahitaji Beki wa udambwi mmoja, na mwingine awe Komando Kipensi. Beki katili mwingine pale nyuma. Inaweza kuleta balansi nzuri sana.

Chanzo: Mwanaspoti
Related Articles: