Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Katiba Simba bado 'lugha gongana'

Simba Katiba Ms Katiba Simba bado 'lugha gongana'

Mon, 22 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwenyekiti wa Klabu Simba, Murtaza Mangungu amesema anawashangaa wanaotaka nafasi ya uenyekiti kuwa na mamlaka ndani ya Bodi ya Wakurugenzi akidai huko ni kukariri na wao walishaondoka huko.

Wakati Mangungu akiona hakuna shida nafasi yake kuwa na majukumu ya wazi ndani ya Bodi, wanachama wa klabu hiyo wamedai baadhi ya mambo yaliyoagizwa na vyombo husika vya serikali hayajafanyiwa kazi na hayamo kwenye rasimu ya ya Katiba iliyojadiliwa na kupitishwa katika mkutano mkuu wa wanachama uliofanyika jijiji Dar es Saalam jana, Jumapili.

Hayo yaliibuka tangu mchakato wa kupokea maoni ya maboresho ya Katiba ambapo jana rasimu ilijadiliwa na wanachama kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa klabu hiyo huku kipengele kimoja kati ya sita kikishindikana kupitishwa.

Kipengele ambacho wanachama hawakukipitisha ni idadi ya wanachama wa kuingia kwenye mkutano mkuu na kupiga kura katika uchaguzi wakiwakilishwa na mwenyekiti wa Simba na katibu mkuu wa wilaya na mkoa, ambapo wanachama wakihitaji ipitishwe kwa kila mwanachama kupiga kura yaani isiwe na kikomo.

Pia wanachama walitaka nafasi ya mwenyekiti iwe na nguvu ya mamlaka kwenye Bodi ya Wakurugenzi, ambapo kwenye hadidu za rejea kipengele hicho hakikuwasilishwa ingawa inadaiwa kwenye maoni yaliyokuwa yakitolewa na wanachama walipendekeza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mangungu amesema, "Simba inaendeshwa na Bodi. Bodi ya Simba hata kama itatamka kuwa mwenyekiti awe na mamlaka yoyote itarudi kuwa Simba inaendeshwa na Bodi na Bodi sio mtu ni kikao kinachohusisha wajumbe na wataalamu mbalimbali ambao tunakutana.

"Kwa hiyo dhana kuwa mwenyekiti lazima awe na mamlaka hiyo ni kukariri tu kwa sababu sisi hatuna mfumo wa kiimra kwamba watu fulani wanasema hivi na sisi twende hivyo."

ALIYEJIUZULU ATOA NENO Aliyekuwa mjumbe wa Kamati ya Maboresho ya Katiba hiyo, Wakili Moses Kaluwa ambaye alijiuzulu amesema maoni ya wanachama hayakuzingatiwa kwenye rasimu iliyojadiliwa na kupitishwa.

"Hata yale ambayo tulipewa na Rita (Wakala wa Ufilisi na Udhamini) pamoja na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) hayajazingatiwa. Kwenye hadidu za rejea Rita ilielekeza ndani ya katiba kiwepo kipengele kinachoonyesha Baraza la Wadhamini limeundwaje na kikomo chao kikoje, kwa maana watakaa madarakani kwa muda gani, ila halijawekwa.

"Pia BMT kuna maelekezo waliyatoa ambayo siyaoni ingawa wanachama walitoa maoni yao ikiwemo kujua majukumu ya mwenyekiti wa Klabu ya Simba anayechaguliwa na wanachama, hivyo ipo kama inavyoeleza katiba inayofanyiwa maboresho."

"Inawezekana kamati imeangalia mambo ambayo yatasaidia kwa haraka kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji ingawa naona maoni mengi hayajapewa nafasi. Ukiachana na hilo la wanachama kugomea idadi ya wanachama wa kuingia kwenye mkutano mkuu wanataka isiwe na kikomo."

Naye mwanachama wa Simba ambaye ni Mweka Hazina wa Tawi la Simba Roho Mbaya, Daud Simba amesema: "Hicho kipengele ndiyo kilikuwa na shida sijui watakipitishaje wakati wanachama hatujakubaliana nacho.

"Nafasi ya mwenyekiti haikujadiliwa kwa sababu haikuwekwa kabisa, hivyo ni ngumu kujadili kitu ambacho hakijaletwa kwetu inabaki kama ilivyokuwa mwanzo ingawa haitendi haki."

BOSI KAMATI HUYU HAPA Mwenyekiti wa Kamati ya Maboresho, Wakili Hussein Kita amesema maoni ya wanachama kuhusu rasimu hiyo yalikuwa mengi na maboresho huwa hayafungwi.

"Hivyo yanaweza kufanyika hapo baadaye kwani tulichofanya na kuboresha vitu baadhi tulivyoelekezwa ambavyo vilikuwa kinyume na sheria na kanuni ili kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji," amesema Kita.

Hata hivyo, rasimu hiyo itapelekwa kwa Msajili wa Vyama vya Michezo aliyepo BMT ambaye ataipitia na kama haitakuwa na kasoro Simba itaruhusiwa kuitumia, ingawa ikibainika kwa na kasoro itarudishwa ili irekebishwe tena.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: